Tatmadaw: Jeshi la Myanmar linalojulikana kutekeleza vitendo vya ukatili

Tangu lilipoipindua serikali iliyochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia ya Aung San Suu Kyi mwaka mmoja uliopita, jeshi la Myanmar - linalojulikana kama Tatmadaw, limeendelea kuushangaza ulimwengu kwa kuua mamia ya raia wake, ikiwa ni pamoja na makumi ya watoto, katika msako wa kikatili dhidi ya waandamanaji.

Kwa raia wa Myanmar, umekuwa mwaka wa mauaji ya kiholela mitaani na uvamizi wa umwagaji damu vijijini. Mnamo Desemba 2021, uchunguzi wa BBC uligundua kuwa Tatmadaw ilifanya misururu ya mashambulio ambayo yalihusisha mateso na mauaji makubwa ya wapinzani.

Zaidi ya watu 1,500 wameuawa na vikosi vya usalama tangu mapinduzi ya Februari 2021, kulingana na Chama cha Msaada kwa Wafungwa wa Kisiasa (Burma).

Lakini jinsi gani Tatmadaw ikawa na nguvu sana na kwa nini ni ya kikatili sana?

Tatmadaw ni nini?

Tatmadaw ina maanisha "vikosi vya jeshi" katika lugha ya Burma, lakini jina limetumika sana dhidi ya mamlaka ya sasa ya kijeshi, kutokana na nguvu zake kubwa nchini na kujulikana duniani kote.

Kwa karne nyingi utawala wa kifalme wa Burma ulikuwa na jeshi lakini ulivunjwa chini ya utawala wa Uingereza.

Mizizi ya Tatmadaw inaweza kupatikana nyuma tangia Jeshi la Uhuru wa Burma (BIA), ambalo lilianzishwa mnamo 1941 na kikundi cha wanamapinduzi kilichojumuisha Aung San, anayechukuliwa na Waburma wengi kama "Baba wa kiroho wa Taifa". Alikuwa babake Aung San Suu Kyi.

Aung San aliuawa muda mfupi kabla ya Burma kupata uhuru kutoka kwa Uingereza mnamo mwaka 1948. Lakini kabla ya kifo chake, BIA lilikuwa tayari imeanza kuungana na wanamgambo wengine kuunda jeshi la kitaifa. Baada ya uhuru, hatimaye liliunda kile tunachokijua leo kama Tatmadaw.

Baada ya uhuru, lilipata nguvu na ushawishi haraka. Kufikia mwaka 1962, lilikuwa limechukua udhibiti wa nchi kwa mapinduzi na lingetawala bila kupingwa kwa miaka 50 iliyofuata. Mnamo 1989, lilibadilisha jina la nchi kuwa Myanmar.

linashikilia hadhi ya juu nchini, na kujiunga na jeshi ni lengo linalotarajiwa kwa wengi, ingawa mapinduzi hayo yamewaacha baadhi ya wanachama wake wakiwa wamekata tamaa.

"Nilijiunga na jeshi kwa sababu ninataka kushika bunduki, kwenda mstari wa mbele, na kupigana. Ninapenda kujitolea kwa ajili ya nchi," alisema Lin Htet Aung*, kapteni wa zamani katika jeshi.

Aliacha kujiunga na Vuguvugu la Uasi wa Kiraia nchini humo (CDM), ambalo liliibuka kupinga mapinduzi ya Februari 1 linalohusisha madaktari, wauguzi, vyama vya wafanyakazi na wengine wengi kutoka tabaka tofauti za za maisha.

"Lakini sasa najisikia aibu sana. Nilifanya makosa kjiunga na jeshi. Waandamanaji wa amani wameshambuliwa kikatili, katika baadhi ya matukio, kwa mabomu, na walenga shabaha. Hili si Tatmadaw (jeshi) tulilotarajia ndio sababu nimejiunga na CDM."

Mfano wa nchi

Myanmar inaundwa na zaidi ya makabila 130 tofauti, huku Wabamar wa Buddha wakiwa wengi.

Wabamar wa Buddha pia ni miongoni mwa wasomi wengi wa nchi hiyo - na wataalam wanasema jeshi linajiona kama wasomi wa wasomi hawa.

LIkiwa na historia iliyofungamana sana na ile ya Myanmar ya kisasa, Tatmadaw limejitambua kama waanzilishi wa taifa na mara nyingi linajionyesha kama kielelezo cha kuwa Mburma wa kweli.

"Wamezama sana katika itikadi hii ya utaifa," anasema Gwen Robinson, mtaalam wa Myanmar katika Chuo Kikuu cha Chulalongkorn huko Bangkok.

"Siku zote wameona vikundi vya makabila madogo kama vitisho ambavyo havistahili kuwa sehemu ya Myanmar, kama vikundi vinavyotaka kuvuruga umoja na utulivu wa nchi na hilo lazima liondolewe."

Hii ina maana kwamba kwa miongo kadhaa, Myanmar imekuwa nchi ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Ni kama dhehebu la dini

Kulingana na Bi Robinson, kila mtu anaweza kuwa mwasi machoni pa Tatmadaw: "Wanawaona waandamanaji hawa kama wasaliti."

Muda mrefu mbali na kazi, kutengwa na jamii nyingine, husaidia kuchochea maoni haya kati ya askari. Baadhi wanaishi katika vikundi vilivyofungiwa, ambapo wao na familia zao wanafuatiliwa sana na kulishwa propaganda za kijeshi, kulingana na wataalam na ushuhuda kutoka kwa maafisa wa zamani.

Wataalamu wanasema hii inakuza hali ya familia kati ya jeshi, na watoto wa maafisa wakati mwingine huoa watoto wa maafisa wengine.

"Jeshi limefananishwa na dhehebu la kidini," asema Bi Robinson. "Hawana mawasiliano mengi na watu wa nje."

Mwanajeshi mmoja ambaye baadaye alijitenga na kujiunga na vuguvugu la Civil Disobedience anathibitisha hilo.

"Askari hawa wamekuwa jeshini kwa muda mrefu kiasi kwamba wanajua lugha ya jeshi tu. Hawaelewi kinachoendelea nje ya jeshi," Luteni Chan Mya Thu* alisema.

Mikataba ya kuzuia uhasama iliyosimamiwa kwa uangalifu imesaidia majenerali kuweka udhibiti wa rasilimali muhimu kama vile jade, rubi, mafuta na gesi. Faida kutoka kwa rasilimali hizi - wakati mwingine halali, wakati mwingine haramu - zimekuwa chanzo muhimu cha mapato kwa jeshi kwa miongo kadhaa. Pia wanasimamia sekta kubwa zenye uwekezaji katika kila kitu kuanzia benki hadi bia na utalii.

Lakini miaka ya ufisadi na usimamizi mbovu wa kiuchumi umegeuza maoni ya umma dhidi ya uongozi wa kijeshi na kuelekea utawala wa kidemokrasia chini ya Aung San Suu Kyi, ambaye chama chake cha National League for Democracy (NLD) kimeshinda kwa kishindo katika chaguzi za hivi majuzi.

'Nchi ndani ya nchi'

Mengi ya mawazo ya Tatmadaw bado yanabaki kuwa kitendawili. "Kwa kweli ni nchi ndani ya nchi," anasema Scot Marciel, ambaye alihudumu kama balozi wa Amerika nchini Myanmar hadi 2020.

"Hawaingiliani na jamii nyingine. Wamejiwekwa kwenye chumba kikubwai ambapo wote wanaambiana jinsi walivyo muhimu, jinsi tu wanaweza kuiweka nchi pamoja, na jinsi bila wao madarakani nchi itasambaratika."

Wakosoaji kwa mfano, wanaashiria jinsi majenerali walifanya gwaride la kifahari la kijeshi na karamu ya chakula cha jioni katika mji mkuu wa Nay Pyi Taw mwezi Machi, huku wanajeshi wakiwauwa zaidi ya raia 100 nchini kote katika siku ambayo ilikuwa mbaya zaidi tangu mapinduzi.

"Maafisa wa ngazi za juu ni matajiri na utajiri haukuwahi kugawanywa na wale wa vyeo vya chini," Meja Hein Thaw Oo*, mwanajeshi wa zamani, aliambia BBC Burma.

"Nilipojiunga na Tatmadaw, nilifikiri ningelinda mipaka na mamlaka yetu. Badala yake nilikuta vyeo vya chini havithaminiwi na vinaonewa na wakubwa."

Wanajeshi hao hatimaye huchukua maagizo yao kutoka kwa kiongozi wa mapinduzi Jenerali Min Aung Hlaing.

Meja Oo aliambia BBC Burma kwamba Jenerali Hlaing alipochukua mamlaka alipata kukubalika katika jeshi baada ya kuboresha silaha na sare.

"Lakini muda wake ulipoisha akaongeza, kulikuwa na makamanda wengi ambao ni bora kuliko yeye katika njia tofauti, lakini alikataa kung'atuka, ndiye aliyevunja kanuni kwa manufaa yake binafsi," alisema.

Licha ya hayo, hata hivyo, watu kama Meja Oo ndio wachache - wanajeshi wengi wanamuunga mkono Jenerali Hlaing na mapinduzi yake.

Sasa, zaidi kuliko awali, inaonekana Tatmadaw linaonyesha picha yake halisi, jeshi ambalo ni la siri, lenya nguvu na linalowajibika yenyewe tu.

Au kama Bw Marciel anavyosema - sidhani kama wanajali sana juu ya kile ulimwengu unafikiria kuwahusu."