Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Watu kadhaa wauawa katika shambulio la risasi katika jumba la maduka la Copenhagen
Watu kadhaa wameuawa kwa kupigwa risasi katika kituo kimoja cha maduka katika mji mkuu wa Denmark Copenhagen, polisi wamesema.
Akitangaza vifo hivyo, mkuu wa polisi Soeren Thomassen alisema mwanamume wa Denmark mwenye umri wa miaka 22 amekamatwa kuhusiana na shambulio hilo.
Bw Thomassen alisema nia ya kitendo hicho haijulikani, lakini hawezi kupinga kuwa "kitendo cha kigaidi".
Walioshuhudia tukio hilo wamezungumza kuhusu hofu miongoni mwa wanunuzi huku milio ya risasi ikisikika ndani ya jumba la maduka la Field's kusini mwa jiji hilo.
Emilie Jeppesen aliliambia gazeti la Jyllands-Posten: "Huwezi kujua kilichokuwa kikiendelea. Ghafla kulikuwa na fujo kila mahali."
Shahidi mwingine, Mahdi Al-Wazni, aliiambia TV 2 kwamba mshukiwa alikuwa amebeba "bunduki ya kuwinda".
Akizungumza katika mkutano na wanahabari Jumapili jioni, Bw Thomassen alisema ni mapema mno kubaini ni watu wangapi waliojeruhiwa katika shambulio hilo.
Lakini aliwaambia waandishi wa habari kwamba hakuna dalili kwamba washambuliaji wengine walihusika.
Field's ndio kituo kikuu cha ununuzi nchini Denmark, chenye maduka na mikahawa zaidi ya 140.
Mwimbaji wa Uingereza Harry Styles anatarajiwa kutumbuiza katika ukumbi uliopo maili moja kutoka eneo la tukio baadaye jioni.
Waandalizi waliandika kwenye Facebook kwamba tamasha hilo lingeendelea baada ya ushirikiano wa karibu na polisi.