Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Shambulio la kambi ya Marekani Jordan: Jeshi la Marekani lina chaguo gani ili kujibu?
Na Frank Gardner
Mwandishi wa usalama wa BBC
Washington sasa inajikuta inakabiliwa na mtanziko.
Rais Joe Biden ameahidi jibu kali kwa shambulio baya la Jumapili kwenye kambi ya kijeshi ya Marekani huko Jordan . Lakini changamoto kwa Marekani ni kupata uwiano sahihi kati ya kuzuia mashambulizi siku zijazo na pia kuepuka kuzidisha mzozo .
Kushindwa kuchukua hatua madhubuti kunaweza kuhatarisha kutuma ujumbe wa udhaifu ambao utahimiza tu mashambulizi zaidi. Kutumia nguvu kupita kiasi kunaweza kusababisha mwitikio wa hali ya juu kutoka kwa Iran na washirika wake.
Kwa hivyo ni chaguzi gani? Na hii inafanyaje kazi?
Marekani tayari itakuwa na idadi ya maamuzi ya kijeshi "kwenye rafu" zake. Hizi zimeundwa na Idara ya Ulinzi ya Marekani kwa maoni ya kijasusi kutoka kwa CIA na Shirika la Usalama wa Kitaifa. Kisha huwasilishwa kwa Baraza la Usalama la Kitaifa la Marekani na watunga sera, na rais akifanya uamuzi wa mwisho na kutia saini uamuzi uliochaguliwa
Chaguo 1: Kushambulia kambi na makamanda wa washirika wa Iran
Hili ndilo chaguo dhahiri zaidi na moja ambalo limetumika hapo awali.
Kuna idadi kubwa ya kambi, na maghala ya silaha kote Iraq na Syria ambayo ni mali ya maelfu ya wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran. Wanamgambo hawa wanapewa mafunzo, vifaa na kufadhiliwa na Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC) Quds Force, lakini si lazima kuelekezwa na wao.
Marekani wanajua wao ni akina nani na wako wapi. Inaweza kufanya mashambulizi zaidi ya makombora yanayoongozwa kwa usahihi katika vituo hivi - lakini hii imeshindwa kuwazuia wanamgambo hao, ambao wameanzisha mashambulizi zaidi ya 170 kwenye kambi za Marekani katika eneo hilo tangu tarehe 7 Oktoba.
Kundi linalojiita Islamic Resistance in Iraq limedai kuhusika na shambulio hilo.
Hili ni neno la 'mwamvuli' kwa makundi ya wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran, ambao baadhi yao, cha kushangaza, wamepigana hapo awali upande uleule wa Marekani dhidi ya adui wao wa pamoja katika kanda: Islamic State. Wanashiriki malengo ya pamoja na Iran, yaani kuliondoa jeshi la Marekani kutoka Iraq na Syria na kuiadhibu Marekani kwa msaada wake wa kijeshi kwa Israel.
Chaguo la 2: Kushambulia Iran
Hili litakuwa ni ongezeko kubwa la mzozo na si jambo ambalo Marekani ingezingatia kirahisi.
Haiwezekani sana, ingawa si jambo lisilowezekana, kwamba kulipiza kisasi kwa Marekani kungejumuisha kulenga shabaha katika ardhi huru ya Irani.
Si Washington wala Tehran wanataka kuingia katika vita kamili na wote wamesema hivyo. Majibu ya Iran yanaweza kujumuisha kujaribu kufunga Mlango-Bahari muhimu wa kiuchumi wa Hormuz, ambapo 20% ya mtiririko wa mafuta na gesi duniani. Hii inaweza kuwa na athari mbaya kwa uchumi wa dunia, kuongeza bei na kwa hakika kuharibu nafasi ya Rais Biden ya kuchaguliwa tena mnamo Novemba.
Njia moja mbadala ni kuwafuata makamanda wakuu wa IRGC nchini Iraq au Syria.
Kuna mfano wa hili, unaojulikana zaidi miaka minne iliyopita wakati Rais wa wakati huo Donald Trump alipoamuru shambulio la ndege isiyo na rubani ambayo ilimuua kamanda wa Kikosi cha IRGC Quds Qassim Suleimani huko Baghdad mnamo 2020. Lakini hii pia ingeonekana kama kuzidisha uhasama na inaweza vizuri kusababisha jibu hatari kutoka Tehran.
Mashambulizi dhidi ya kambi za Marekani nchini Iraq,Syria na Jordan
Idadi ya mashambulizi
Chaguo la 3: Kutojibu
Kuna wale nchini Marekani wanaohoji kuwa, kutokana na mvutano uliopo katika Mashariki ya Kati, itakuwa ni kutowajibika kwa Washington kugusa maslahi ya Iran hivi sasa, hasa katika mwaka wa uchaguzi.
CENTCOM, sehemu ya Idara ya Ulinzi ya Marekani inayoshughulikia Mashariki ya Kati, tayari ina kazi kubwa kupambana na mashambulizi ya Wahouthi dhidi ya meli katika Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden. Pia itasikiliza maombi kutoka kwa washirika wa Marekani katika eneo hilo kutoanzisha mzozo mkubwa wa Mashariki ya Kati.
Lakini maoni haya huenda yakapitwa na wale wanaosema kwamba sera ya Marekani ya kuzuia hadi sasa imeshindwa, na kwamba kusita kwa Washington kuwapiga vikali wale wanaoshambulia vituo vyake kumewahimiza tu kuongeza mashambulizi yao.
Kuna sababu ya wakati katika haya yote - wengine wanaweza kusema kuwa mabadiliko makubwa katika majibu ya kijeshi ya Marekani yanaweza kuwa ya lazima au ya kufaa kwa muda mrefu.
Kwanza, mashambulizi ya wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran yalitangulia vita vya Israel na Hamas huko Gaza - lakini yameongezeka kwa kasi tangu tarehe 7 Oktoba. Mara baada ya mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza kukamilika basi mvutano katika eneo hilo huenda ukapungua, ingawa Israel inaonya kuwa hii inaweza kudumu kwa miezi kadhaa .
Pili, kuna wito mkubwa kutoka kwa baadhi ya watu huko Washington kwa Marekani kupunguza mwendo wake wa kijeshi katika Mashariki ya Kati. Rais Trump alipokuwa madarakani, alilazimika kushawishiwa na wakuu wake wa kijeshi na kijasusi kutoondoa majeshi yote ya Marekani kutoka Syria, ambako walikuwa wakisaidia vikosi vya Wakurdi kuwazuia ISIS kurejea.
Kuna uwezekano mkubwa kwamba iwapo Trump atarejea Ikulu ya White House baada ya mwaka mmoja, basi Iran itapata njia yake kwa vyovyote vile, ikiwa itaamua kudhoofisha uwepo wa Marekani nchini Iraq na Syria.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah