Maandamano Tanzania: Kwanini Disemba 9 yameshindikana?

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 5

Katika siku ambayo baadhi ya watanzania walitarajia kushuhudia hatua ya kihistoria ya maandamano ya amani ya Desemba 9, hali ilikuwa tofauti kwa siku nzima.

Hakukuwa na misafara ya waandamanaji, mabango, wala makundi makubwa ya watu kupaza sauti zao. Ilikuwa tofauti na maandamano ya Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata.

Badala yake, kulikuwa na utulivu wa tahadhari katika miji mikubwa iliyokumbwa na maandamano ya awali, utulivu ambao si wa ukimya, bali ulizungukwa na maswali mengi.

Si Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Kilimanjaro, Iringa au Dodoma kulikuwa na maandamano kama yale ya siku tatu kuanzia Oktoba 29, 2025 siku ya uchaguzi Mkuu.

Maandamano yalipangwa kudai mabadiliko ya kimfumo nchini humo, kuanzia katiba mpya, demokrasia, haki za binadamu na hata kurejewa kwa uchaguzi uliompa ushindi wa 97%, Rais Samia Suluhu Hassan

Lakini kundi la wanaharakati Kenya walifanikiwa kwa kiasi kuandamana nje ya Ubalozi wa Tanzania jijini Nairobi, Kenya, ingawa kuna baadhi walidhibitiwa na kutiwa nguvuni.

Swali kuu si tu kwa nini hakukuwa na maandamano, bali ni nini kimeunda mazingira ambayo yalipelekea tukio lililotabiriwa kwa wiki kadhaa kushindikana.

Kivuli cha Oktoba 29

Oktoba 29, 2025, inatajwa kuwa siku yenye madhara makubwa ya kisiasa nchini Tanzania.

Tukio hilo lilileta uharibifu wa mali, vifo vya watu na majeraha ambayo bado yamesalia kuwa kumbukumbu ngumu vichwani mwa wengi. Wengi wanakumbukumbu ya kuona na kusikia kuhusu vifo na majeruhi kadhaa. Kibinadamu inawapa kumbukumbu ya kutisha.

Ingawa kwenye mitandao, ukiwasikiliza vijana wa Gen z, hawaonyeshi sana kujali hili.

Pia watu walikosa huduma muhimu kwa karibu siku tano, wakiwa wameachwa na maumivu ya kihisia na kimaisha. Biashara zilifungwa, huduma zilikosekana na kwa ujumla yalikuwa maisha ya adhabu kwa wengi.

Katika mazingira haya, maandamano yoyote yanayokumbusha tukio hilo yaliweza kuwa na uzito wa kipekee.

Hamasa ya kujieleza kwa baadhi ya wananchi ilikosa kushinda hofu ya matukio yaliyopita, na hali ya kutokuwa na uhakika mara nyingi hushusha uwezekano wa umma kuchukua hatua za pamoja.

Udhibiti wa Dola

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Wiki moja kabla ya Desemba 9, ulinzi uliimarishwa karibu katika maeneo yote ya miji mikubwa. Ulikuwa ulinzi usio wa kawaida, uliozoeleka.

Askari wa Polisi na Jeshi la Wananchi walionekana kupiga doria katika mitaa mbalimbali, jambo ambalo halikuonekana kuelekea maandamano ya Oktoba 29.

Uwepo huu wa doria ulitengeneza mazingira ya udhibiti wa kisaikolojia, ambapo wananchi walihisi kwamba hatua yoyote ya kuandamana inaweza kuleta hatari.

Akizungumzia tukio la Oktoba 29, Rais Samia Suluhu alisema katika mkutano na wazee wa Dar es Salaam, "Nguvu inayotumika inaendana na tukio lililopo… tunapoambiwa kwamba tumetumia nguvu kubwa sana kwenye tukio lile, nguvu ndogo ilikuwa ipi?"

Kauli hii inafafanua kwamba dola ilishinda mapambano kabla hayajaanza, na wengi waliona ni busara kulinda usalama wao binafsi kuliko kuingia kwenye hatari.

Kesi za uhaini

s

Tangu baada ya maandamano ya Oktoba 29, maelfu ya vijana walikamatwa na kushitakiwa kwa makosa ya uhaini, ambayo ni kosa kubwa sana nchini Tanzania na lenye adhabu kubwa ikiwa mtu atathibitishwa. Adhabu ya kifo.

Ingawa wanasheria walikosoa mashtaka hayo wakisema hayana msingi wa kisheria, hali hii imesababisha baadhi ya vijana kujitathmini kabla ya kuandamana.

Ingawa karibu wote wamekwishaachiwa huru na kufutiwa mashtaka hayo na mwendesha mashtaka wa serikali (DPP) baada ya Rais kutoa msamaha, bado tukio hili limeonesha kuwa malalamiko ya kisiasa yanasalia, lakini hatua za kisheria na tahadhari za serikali zinaathiri chaguo la kuchukua hatua za umma.

Kauli na matamko

S

Chanzo cha picha, URT

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Tangu Oktoba 29, kauli mbalimbali zimekuwa zikitolewa na viongozi wa serikali, dini, polisi na mashirika yasiyo ya kiserikali.

Wengine walihimiza kuandamana kama haki ya kiraia, wengine wakionya kuhusu uwezekano wa vurugu.

"Inakuonesha njia muhimu ni kusikiliza, kuruhusu watu waongee bila woga, watoe madukuduku yao, halafu serikali ifanyie kazi", anasema Rehema Mema, mchambuzi

Rehema anatoa mfano wa Zanzibar, ilitumika njia hiyo ya mazungumzo kwa zaidi ya mwaka mzima mara baada ya ghasia za maandanao ya Januari 2001, na kuzaa maridhiano yanayoiweka Zanzibar Pamoja mpaka leo.

Rais Samia aliwahi kuonya kuelekea Desemba 9 kwamba Serikali imejipanga: "Likija wakati wowote, tumejipanga. Tutasimama na kuilinda nchi hii kwa nguvu zote."

Kauli za viongozi na uwepo wa nguvu zilizotumika Oktoba 29 vimechochea tahadhari miongoni mwa vijana waliokuwa na nia ya kuandamana.

Polisi pia waliweka wazi kuwa maandamano hayo yamepigwa marufuku na ni haramu, hali iliyoonyesha wazi kwamba hatua yoyote ya kisheria inaweza kudhibitiwa kabla haijaanza.

Japo ilisema hivyo hivyo Oktoba 29, na bado maandamano yakawepo, pengine mazingira ya sasa, yameyapa uzito kiasi matamko ya aina hii.

Je, Disemba 9 ni mwisho au mwanzo wa mjadala?

Pamoja na kudhibiti maandamano, Serikali haijaweza kudhibiti mijadala ya wananchi. Kupitia mitandao ya kijamii, watu wanaendelea kueleza malalamiko yao, ingawa maandamano yamepigwa marufuku.

Mange Kimambi, mwanaharakati, ambaye ameshitakiwa kwa uhujumu uchumi kwa matukio ya Oktoba 29, na mmoja wa vinara wa maandamano na anashitakiwa na Serikali, alisema: "Haturudi nyuma… safari ya ukombozi haijawahi kuwa rahisi, ushindi ni lazima na tutashinda."

Hii inaonyesha kuwa madukuduku ya wananchi hayakufa; malalamiko bado yapo, ingawa hayana jukwaa la wazi.

Wachambuzi wanasema kutofanyika kwa maandamano hakumaanishi mwisho wa mijadala ya kiraia. Badala yake, inaweza kuwa fursa kwa Serikali na wananchi kufikiria upya njia mbadala za kuwasilisha maoni, kuimarisha majadiliano halali, na kujenga misingi imara ya haki ya kujieleza.

"Mustakabali wa nchi utategemea uwiano kati ya udhibiti na ushirikishaji, kati ya usalama na uhuru, na kati ya sheria na maridhiano", anasema Mema.

Kwa ujumla maandamano ya Desemba 9 hayakushindikana si kwa sababu wananchi hawana malalamiko, wala si kwa woga wa waandaaji pekee. Yameshindikana kutokana na mchanganyiko wa sababu.

Ingawa Desemba 9 haikutoa sauti ya umma barabarani sauti inayotajwa na mamlaka kama haramu na uvunjifu wa amani, hakuna anayejua hatma, je yataitishwa maandamano mengine? hali itakuwaje na nini mustakabali wa taifa hilo? Haya yanasubiri wakati Tume Huru ya Uchunguzi inaendelea kuchunguza matukio ya Oktoba 29, itoe mwanga wa kuondoa misuguano na kuimarisha maridhiano ya kitaifa.