Wakenya wanaolaghaiwa na maajenti kuhusu maombi yao ya visa ya Canada

Henry Kathurima

Chanzo cha picha, Henry Kathurima

Maelezo ya picha, Henry Kathurima alitarajia fursa mpya za kazi nchini Kanada
    • Author, Anita Nkonge na Maureen Nyukuri
    • Nafasi, BBC News
    • Akiripoti kutoka, Nairobi
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Maisha mapya, nchi mpya na kazi mpya ndivyo Mkenya, Henry Kathurima alitarajia alipoamua kuhamia Canada.

"Nilikuwa na matarajio makubwa sana. Nilidhani ningeanza maisha yangu kwa kasi ya juu kwa sababu nilitarajia ningeenda huko na kuanza kazi mara moja," anasema.

Henry ni afisa wa zamani wa uchunguzi wa serikali ambaye aliamini kuwa maisha yake nchini Kenya yalikuwa hatarini kwa sababu ya kesi aliyokuwa akiifanyia kazi.

"Nilianza kufikiria ni wapi ninaweza kukimbilia kutafuta hifadhi."

Akiwa na matumaini ya kuondoka nchini haraka, Henry aligeukia kampuni aliyoipata kwenye mtandao wa kijamii - Shirika la Usafiri la SkyPins.

"Ilionekana kuwa halali," anasema.

Mnamo Aprili 2023, Henry aliwasiliana na ajenti ambaye anasema alimuonyesha orodha ya kazi nchini Canada na mishahara yao.

"Kilikuwa kifurushi kizuri, zilikuwa pesa nzuri," anasema.

Henry aliwapa SkyPins hati zake, akiamini watazitumia kufungua akaunti ya maombi ya visa. Alitia saini mkataba na kampuni hiyo, akiwalipa $930 USD mapema na $386 za ziada katika ada zilizofuata za kushughulikia visa.

Henry anasema shirika hilo liliunda akaunti kwa jina lake, lakini hakuruhusiwa kufikia maelezo yake ya kuingia.

A school girl in blue hijab waves a tiny Canada flag across her face

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mnamo 2023 Kanada ilizingatia takriban maombi 30,000 ya visa vya makaazi ya muda kutoka kwa Wakenya.

Mary, sio jina lake halisi, pia alipata kampuni ya SkyPins kwenye mitandao ya kijamii.

Muuguzi anayefanya kazi katika hospitali ya serikali, Mary aliamini ingekuwa bora kuhamia Canada kwa kutumia wakala badala ya kufanya mitihani ya kimataifa ya uuguzi.

"Walikuwa wameniahidi 'kazi iliyo tayari' kama mlezi," anasema. "Nilifikiri 'hii ni njia ya haraka ya kunifikisha huko' kisha [nitakapofika] naweza kujiandikisha kwa ajili ya masomo na kuendesha taaluma yangu. ."

Hakuweza kupata pesa zinazohitajika mwenyewe, Mary alichukua mkopo ili kufidia gharama za SkyPins.

"Nilisaini mkataba. Gharama ilikuwa karibu dola 930 ambapo dola 150 zilikuwa za kushughulikia visa na iliyobaki ilikuwa ada yao, "anasema.

Kama tu Henry, Mary anasema hakupewa ufikiaji wa akaunti yake mwenyewe badala yake Skypins walimuundia moja na kuisimamia kwa niaba yake.

Unaweza Pia Kusoma

Wanaotuma maombi hawawatumii washauri au mawakala

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kuombwa kulipa pesa mapema bila ufikiaji wa moja kwa moja kwa mchakato wa maombi ya visa kunafaa kuwa ishara ya jambo baya au uwovu, kulingana na ubalozi wa Canada nchini Kenya.

"Wateja wote wanaweza kufikia, kuunda akauti na kutuma maombi moja kwa moja. Hawahitaji kuajiri mshauri au wakala kujaza ombi lao au kupata ufikiaji wa tovuti," anasema Marie-Pier Côté, Meneja wa Mpango wa Uhamiaji kwa Wakimbizi na Uraia wa Uhamiaji katika ofisi ya viza ya Kanada jijini Nairobi.

Ubalozi wa Canada pia unaonya dhidi ya wateja kuruhusu mawakala kujaza fomu kwa niaba yao.

"Wateja wanawajibika kwa habari katika maombi yao. Sio wakala, ni wao. Kwa hivyo, kama kuna taarifa za uongo zinazotolewa katika maombi, mteja anawajibika kuitambua na kuirekebisha," anasema Marie-Pier Côté.

"Tunaona ulaghai mwingi kutoka kwa mawakala," anasema.

Henry anadai kuwa katika kesi yake, shirika hilo liliongeza taarifa ya benki bandia kwenye maombi yake ambayo yalionyesha kuwa alikuwa na dola 40,000 za Canada kwenye akaunti yake. Ulaghai huu unaodaiwa ulikuwa na athari kubwa.

Sio tu kwamba ombi la Henry lilikataliwa, lakini serikali ya Canada ilimpa marufuku ya miaka mitano kutembelea Canada. Pia alizuiwa kusafiri kwenda Australia, New Zealand, Uingereza na Marekani chini ya Muungano wa Ujasusi wa nchi hizo tano(Five Eyes Intelligence Alliance)

"Sikuwa na nia yoyote ya kusema uwongo. Sikujua nilikuwa nikikosea au kufanya ulaghai," anasema.

Kwa Mary, masuala pia yalijitokeza wakati Skypins ilipowasilisha ombi lake, anasema.

"Walikuwa wameongeza jina la ukoo kwa jina langu. Sina jina la ukoo. Walidai lilikuwa kosa la kuandika na kuahidi kulirekebisha, lakini hawakufanya hivyo," anasema.

Mary pia anadai kwamba Skypins waliwasilisha taarifa ya benki bandia kwa niaba yake, ambayo hakuwa ameitoa.

"Taarifa ya benki iliyotumika kwenye maombi si ile niliyotoa. Kwa njia fulani, walipata nyingine tofauti na yangu na sijui waliipataje, "anasema.

Hata hivyo, Mary bado alitumaini maombi hayo yangefaulu.

"Skypins waliendelea kuniambia kuwa mvumilivu. Nilitarajia kupata barua pepe, labda kutoka kwa ubalozi lakini hakuna iliyokuja," anasema.

Baada ya karibu mwaka mmoja, Mary alianza kushuku kwamba alikuwa ametapeliwa. Alikabiliana na Skypins, ambao hatimaye walimwambia kwamba ombi lake la visa lilikuwa limekataliwa.

BBC iliwasilisha madai ya Henry na Mary kwa Dennis Kimotho, Mkurugenzi wa SkyPins Tour Travel Agency.

Kimotho alikanusha madai yote akisema SkyPins sio wakala wa kuajiri na haijasajiliwa chini ya mamlaka ya kitaifa ya uajiri. Badala yake, anasema shirika hilo liko mbioni kujisajili kuwa kampuni ya utalii chini ya Mamlaka ya Kudhibiti Utalii. Alikanusha kuwa walipanga visa za kazi au walituma maombi ya visa kwa kutumia hati za uwongo.

Bw Kimotho alijibu madai ya Henry kwa kumtaka awasiliane na shirika hilo moja kwa moja.

"Namfahamu mteja aliyetajwa hapo juu. Madai yoyote yanayoibuliwa kuhusu mteja wangu nazungumza nao tu. Tafadhali wajulishe wateja wawasiliane nasi kwa taarifa zozote utakazohitaji," alisema kwenye ujumbe mfupi ambao BBC iliuona.

Visa application paperwork
Maelezo ya picha, Ofisi ya Upelelezi wa Jinai katika jijini Nairobi inachunguza mamia ya malalamiko kuhusu mashirika yanayodai kuwatafutia watu ajira

Matangazo kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii

Henry na Mary hawako peke yao katika kupoteza pesa kupitia maombi ya visa ya ulaghai yanayoshughulikiwa na mashirika yanayodaiwa kuwa ya uhamiaji.

BBC imefichua mtandao unaoenea wa zaidi ya kurasa mia moja za mitandao ya kijamii, kila moja ikijionyesha kama lango la Wakenya wanaotamani kuhamia Canada. Majukwaa haya - hasa TikTok, Facebook, na Instagram - ni ngome yenye rutuba kwa mashirika kufikia hadhira pana ya wanaotafuta kazi.

Kulingana na Idara ya Uhamiaji, Wakimbizi na Uraia wa serikali ya Canada, tatizo la ulaghai wa maombi ya visa kupitia mashirika limeenea kote Afrika ya Kusini mwa Jangwa la Sahara. Kesi pia zimeripotiwa Nigeria, Tanzania na Uganda.

Mwaka 2023, Canada ilizingatia maombi 29,577 ya visa za makaazi ya muda kutoka kwa Wakenya, ambapo 47% yaliidhinishwa na 53% kukataliwa. Miongoni mwa yaliyokataliwa, 14% yalionekana kutokubalika kwa upotoshaji.

Katika miezi sita ya kwanza ya 2024, kiwango hiki cha idhini kilishuka hadi 8% tu na 26% ya maombi ya visa za makazi ya muda yalikataliwa kwa upotoshaji - karibu mara mbili ya kiwango cha mwaka uliopita.

Tatizo sio tu kwa visa zilizokataliwa.

Mwaka jana, mitandao ya kijamii ilionyesha video za Wakenya waliokwama katika mitaa ya Canada. Duru za habari ziliarifu kuwa wengi wao walikuwa wamefika nchini kwa visa za muda za kitalii wakiamini kuwa watapewa ajira. Kazi ziliposhindwa kutekelezwa, waliachwa bila chaguo ila kujaribu kutafuta hifadhi.

Afisa wa Upelelezi wa Jinai wa Canada mjini Nairobi, Benson Kasyoki, amethibitisha kuwa ofisi yake inachunguza mashirika mengi ya uajiri kwa madai ya udanganyifu.

"Tumepokea zaidi ya malalamiko 615 yanayogusa mashirika 263 ambayo tunayachunguza kwa sasa," anasema.

"Waathiriwa wanalalamika kwamba wameibiwa pesa zao kama walipaswa kusafiri kwenda nchi kama Kanada, lakini hawajaenda, na hati zao hazijashughulikiwa."

Bw Kasyoki anasema changamoto kubwa kwa timu yake ni kwamba baadhi ya kampuni hizo aidha zimefungwa, kubadilisha majina, au kurudi sokoni zikiwa na majina tofauti.

Kusubiri kwa muda mrefu kurejeshewa fedha

Henry na Mary walifanikiwa kurejesha baadhi ya pesa zao baada ya kuripoti malalamiko yao kwa polisi. Hata hivyo, Paul, si jina lake halisi, hakuwa na bahati hiyo

Mkenya huyo mwenye umri wa miaka 37 alikuwa akiishi maisha mazuri kama dereva wa lori la masafa marefu. Lakini maisha ya Paul yalibadilika baada ya njia mpya ya treni kufunguliwa, na kufanya kazi yake kuisha.

"Rafiki yangu aliniambia kwamba hakuna haja ya kubadili kazi yangu," asema.

"Alinielekeza kwa wakala maarufu mjini, akisema naweza kuhamia Iraq, au Kanada kwa sababu kuna uhaba wa vibarua na kwamba watu wengi wanaohitajika huko ni madereva wa lori."

Shirika hili lilitangaza huduma zake kama kampuni ya ushauri wa uhamiaji.

Paul anasema walimwambia kwamba madereva wa lori nchini Kanada wanaweza kutengeneza $4,000-$7,000 za Kanada kwa mwezi.

Lakini ili kulipia mchakato wa uhamiaji kupitia shirika hilo, Paul alilazimika kuuza mali zake.

"Akaunti yangu ya benki ilikuwa haina chochote . Kwa hivyo, chaguo pekee nililokuwa nalo ni kuuza kipande changu cha ardhi," asema.

Paul alilipa shirika hili $5,454 USD kwa tikiti za ndege, ada za visa, na mipango ya malazi nchini Kanada. Lakini hakusaini nao mkataba.

Paul hakupewa ufikiaji wa akaunti yake au maelezo ya kuingia na Ubalozi wa Canada. Badala yake, mchakato mzima ulidhibitiwa na wakala.

"Nilikuja kujua kuwa unapojaza viza kuna baadhi ya vitu unatakiwa kutoa labda kama akaunti ya benki, hali ya ndoa." Anasema alikuwa na taarifa zote hizo lakini hakuombwa na wakala kutoa maelezo hayo.

Hatimaye Paul alipokea viza na kuanza kupanga mipango ya kusafiri. Aliaga familia yake na kuelekea uwanja wa ndege akitarajia kupanda ndege kuelekea Canada. Lakini alipofika kwenye dawati la ukaguzi, aliambiwa viza yake ilikuwa imefutwa na Ubalozi wa Kanada ambao uliiweka alama kwa makosa katika maombi.

Baada ya kuomba kurejeshewa fedha kutoka kwa shirika hilo bila mafanikio, aliamua kuripoti suala hilokwa polisi. Hadi sasa, kesi hiyo haijasonga mbele ya hatua ya upelelezi na Paul bado anasubiri haki.

"Niliahidiwa kazi na mwanzo mpya. Nilichopata ni akaunti tupu ya benki na ahadi iliyovunjika," asema.