Iran na Hamas: Mauaji ya Haniyeh yalifichua nini kuhusu usalama na ujasusi wa Iran?

Mauaji ya Haniyeh yalifichua nini kuhusu usalama na ujasusi wa Iran?

g

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Haniyeh na Khamenei takriban mwezi mmoja baada ya shambulio la Oktoba 7

Na Ahmad AL khateeb

BBC Arabic

Mauaji ya mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas Ismail Haniyeh mjini Tehran yameibua maswali kuhusu mfumo wa usalama na ujasusi wa Iran, hasa kwa kuwa tukio hilo ni sehemu ya orodha ndefu ya mauaji ya viongozi wa Iran au takwimu zinazohusishwa na Iran ndani na nje ya nchi.

Haniyeh aliuawa Jumatano, tarehe 31 Julai, wakati akiwa katika mji mkuu wa Tehran, kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa rais mpya, Masoud Pezeshkian.

Iran na Hamas walikuwa wepesi kuishutumu Israel, ambayo haikutoa maoni juu ya tuhuma hizo, wakati baadhi ya tafsiri zilielekeza kidole cha lawama moja kwa moja kwa shirika la ujasusi la Israeli (Mossad).

Hii ni pamoja na tovuti ya Marekani ya Axios, ambayo ilinukuu vyanzo viwili vya habari vikisema kuwa Mossad "ililipua bomu lililotegwa katika chumba cha Haniyeh" katika makazi yake rasmi katika mji mkuu wa Iran, Tehran.

Mauaji ya Haniyeh mjini Tehran yamekuja saa kumi na mbili tu baada ya Israel kumuua kiongozi maarufu wa Hezbollah Fouad Shukr katika uvamizi uliofanywa na ndege isiyo na rubani ya Israel katika kitongoji cha kusini mwa mji mkuu wa Lebanon, Beirut.

Hii si mara ya kwanza kwa Israel kujaribu kumuua Haniyeh, kwa mujibu wa Kylie Moore-Gilbert, mtafiti wa sayansi ya usalama katika chuo kikuu cha Macquarie nchini Australia.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika makala iliyochapishwa katika jarida la sera za kigeni, Moore-Gilbert alirejelea kauli za wanasiasa wa Israel kufuatia mashambulizi ya Oktoba 7 kwamba viongozi wa Hamas walikuwa "watu waliokufa wakitembea."

Mossad kwa kawaida hufanya mauaji nje ya Israeli. Mwezi Januari, mkuu wa Mossad David Barnea alithibitisha kuwa shirika hilo lilikuwa "limepewa jukumu" kuwasaka viongozi wa Hamas, akisema "inaweza kuchukua muda, lakini mikono yetu itawafikia popote walipo."

Akizungumza na BBC, Sayed Ghoneim, profesa anayeizuru NATO na Royal Military Academy mjini Brussels, alisema: "Mafundisho ya mauaji ya Mossad yamekuwepo na sio jambo jipya, ingawa yameongezeka katika miaka ishirini iliyopita."

"Lakini mauaji ya viongozi wa Iran yalifanywa nje ya Iran, iwe kwa mikono ya Israeli au kwa wengine," Ghanem aliongeza.

Labda maarufu zaidi ya operesheni hizi ni ile ambayo kamanda wa Kikosi cha Wakurdi cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran, Qassem Soleimani, aliuawa Januari 3, 2020, katika shambulio la ndege ya Marekani isiyo na rubani karibu na Uwanja wa Ndege wa Baghdad.

Katika mji mkuu wa Syria, Damascus, tarehe 1 Aprili, 2024, shambulio la anga liliharibu jengo karibu na ubalozi wa Iran na kuwaua watu 16, akiwemo Mohammad Reza Zahedi, kamanda mwandamizi katika kikosi cha Wakurdi cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran.

Syria imeishutumu Israel kwa kuhusika na operesheni hiyo, lakini msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari alikataa kuzungumzia shambulio hilo.

Unaweza pia kusoma:
Hakuna mtu aliye salama katika nchi hii"
Muda wa kusoma: Dakika 7

Uzito wa mauaji ya Haniyeh sio tu kwamba ni kwasababu ni mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, lakini pia kutokana na eneo na muda wa mauaji hayo, ambayo yamekuja saa chache tu baada ya kuapishwa kwa rais mpya wa Iran, na ambapo mji mkuu ulikuwa umejaa maafisa waandamizi wa Iran, wajumbe wa kigeni, viongozi wa Jeshi la Mapinduzi ya Iran, na kwa mujibu wa Kylie Moore-Gilbert.

Kwa operesheni hii, Israel sio tu iliiweka Iran katika hali ya aibu, lakini kwa mujibu wa Moore-Gilbert, iliweza kutuma, kutoka Tehran, ujumbe kwamba "hakuna mtu aliye salama katika nchi hii."

Waangalizi waliona mauaji ya Haniyeh katika ardhi ya Iran kama "aibu kubwa" kwa Jamhuri ya Kiislamu, ikiwa ni pamoja na Haleh Esfandiari, mwenzake katika Kituo cha Woodrow Wilson, ambaye alisema kuwa "c kwa vyovyote majibu ya Iran, kuhusu mauaji ya Haniyeh ni doa kwa Iran, kwani kumlinda Haniyeh kunapaswa kuwa muhimu sana kwa mamlaka husika."

Katika ripoti yake kwenye tovuti ya kituo cha Wilson, Esfandiari alijiuliza ni nini mauaji ya Haniyeh yanaweza kusema kuhusu mifumo ya ulinzi wa anga ya Iran, pamoja na huduma zake za ujasusi, akisema: "Haya ni maswali ambayo yatahitaji majibu kutoka kwa utawala wa Iran."

Nchini Iran, vidole vya shutuma havikuacha kuielekeza Israel na kama kawaida, vilienea hadi Marekani, au "Shetani Mkuu," kama utawala wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ulivyozoea kuliita.

Waziri wa Ujasusi wa Iran Esmail Khatib amesema kuwa "mauaji ya Haniyeh yalifanywa na Israel kwa ruhusa kutoka Marekani," lakini Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amekanusha "uhusiano wowote" wa nchi yake na mauaji hayo, akiongeza kuwa Marekani "haikupokea taarifa zozote za awali" kuhusu mpango wa kumuua Haniyeh.

Katika suala hili, Sabah Zanganeh, mchambuzi wa Iran na mwanadiplomasia wa zamani, alisema, "Haniyeh alikuwa na dhamana ya usalama wa Marekani kwamba Israeli haitamuua katika tukio hili, na kwa hivyo alikuwa akisonga kati ya maeneo wazi bila kujaribu kujificha mbele."

Akizungumza na BBC, Zangana alisema, "Kama hakungekuwa na hakikisho la Marekani kwa Haniyeh, angeweza kuwa mwangalifu zaidi, hasa katika mawasiliano yake."

"Lakini kwa hakika haiwezi kusemwa kwamba hakukuwa na uzembe wa usalama," Zangana aliongeza, lakini operesheni hii "si ngumu sana wala sio uvunjaji mkubwa wa usalama kwa kiwango ambacho Waisraeli wanataka kuonyesha. Badala yake, ni operesheni rahisi kwa huduma za usalama na ujasusi."

Israel inatuhumiwa kuhusika na mfululizo wa mauaji ya wanasayansi wa nyuklia wa Iran tangu mwaka 2007, ikiwa ni pamoja na Majid Shahriari, Dariush Rezaei Nejad, na Mohsen Fakhrizadeh, lakini Israel inakanusha madai hayo na kukataa kutoa maoni kuwahusu.

"Tusi la makusudi"

Mauaji ya Haniyeh yamekuja siku chache baada ya mkuu wa ujasusi wa Iran kusema katika video iliyosambazwa sana kwamba "silaha zote za Mossad ndani ya Iran zimezuiliwa." Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Sayed Ghoneim aliyaona mauaji hayo kama "tusi la lililo kusudiwa" kwa ujasusi wa Iran.

Iwapo mauaji hayo yalifanywa na ndege isiyokuwa na rubani kutoka ndani ya Iran au kwa kifaa cha kulipuka kwa mbali, "kwa hali yoyote kuna ukiukaji mkubwa," kwa mujibu wa Ghanem, ambaye anaeleza: "Ikiwa mauaji hayo yalifanywa na kifaa cha kulipuka, hii inaonyesha udhaifu wa usalama wa ndani wa Iran, na pia ikiwa lilifanywa kwa kombora la moja kwa moja lililiopigwa kutoka ndani ya Iran, au kwa ndege isiyo na rubani iliyobeba kifaa kidogo cha kulipuka."

Ikiwa Mossad iliweza kufanya hivyo katika eneo salama sana, sio tu inaonyesha uwezo wa kupenya kwa ujasusi wa Israeli ndani ya Iran, lakini pia udhaifu wa huduma za ujasusi na usalama za Irani, kulingana na tovuti ya Marekani Axios.

Lakini Sabah Zangana anaamini kuwa taasisi za usalama katika nchi zote zina uwezo wake; "Kama vile Israel ina uwezo ndani ya Iran, Iran pia ina uwezo ndani ya Israeli, lakini hadi sasa uamuzi wa kisiasa haujatolewa kwa huduma za usalama za Iran kujibu shambulio hilo."

Zanganeh anathibitisha uwezo wa idara za usalama za Iran kujibu kwa namna yake, akisema: "Labda kama uamuzi kama huo wa kisiasa ungetolewa, tungeona viongozi wengi wa kisiasa, usalama na hata kisayansi wakiuawa."

Mnamo Agosti 2023, Waziri wa Ujasusi wa Irani Esmail Khatib alitangaza kuwa "nguvu ya huduma za ujasusi za Iran ni kubwa sana kiasi kwamba ina majasusi nchini Ufaransa, Sweden, Uingereza na nchi nyingine nyingi," kwa mujibu wa tovuti ya Iran.

f

Chanzo cha picha, The New York Times

Maelezo ya picha, Bango mjini Tehran laonyesha makombora (Aprili 2024)

Gazeti la New York Times limewanukuu maafisa watatu wa Iran wakisema kuwa ukiukaji huu unaonyesha "kushindwa kwa hali ya hatari kwa idara za ujasusi na usalama za Iran, na kuliweka jeshi la Iran katika hali ngumu sana."

Mamlaka za Iran pia zimewakamata watu 20, wakiwemo maafisa wa ngazi ya juu wa ujasusi, maafisa wa kijeshi na wengineo, kufuatia ukiukaji huu wa usalama, kwa mujibu wa gazeti la New York Times, likinukuu maafisa wawili wa Iran.

Iran inajulikana kuwa na mifumo ya ulinzi wa anga ya Urusi ya S-300, na hivyo sahmbulio hilo limezusha joja kwamba kulikuwa na uwezekano wa mipaka ya Iran kukiukwa kutoka nje siku ya kuapishwa kwa rais mpya, kwa mujibu wa Kylie Moore-Gilbert.

Mifumo ya ulinzi wa anga ya S-300 inaweza kuzuia ndege kubwa au ndege zisizo na rubani, lakini haiwezi kuzuia ndege ndogo zisizo na rubani au quadcopters, ambazo ni ndogo kwa ukubwa, kwani vifaa vya rada haviwezi kuzitambua, kulingana na Sayed Ghoneim.

Wizara ya Ujasusi na Usalama wa Taifa nchini Iran, ilianzishwa mwaka 1983 kama njia ya kuunganisha baadhi ya vitengo vya ujasusi kutoka enzi za mapinduzi. Mwaka 1989, ilikuwa na jukumu la kuratibu idara zote za ujasusi, ambazo zinajumuisha mashirika 16 yanayofanya kazi katika ujasusi kwa mujibu wa Taasisi ya Washington ya Sera ya Mashariki ya Karibu.

Wizara ya Ujasusi na Usalama wa Taifa inafanya kazi chini ya mamlaka ya rais, lakini waziri mwenye dhamana lazima achaguliwe kwa idhini ya Kiongozi Mkuu.

"Udhaifu wa kushangaza"

Wakati baadhi ya waangalizi wakiyaona mauaji hayo kama aibu kwa utawala wa Iran, wengine wanaona wazo kwamba Iran haiwezi kulinda eneo lake na washirika wake wakuu kama "uwezekano wa utawala wa Iran," kwa mujibu wa Ali Vaez, mtaalamu wa masuala ya Iran katika Kundi la Kimataifa la Mgogoro.

"Inaashiria kwa maadui kwamba kama hawawezi kuiangusha Jamhuri ya Kiislamu, wanaweza kukata kichwa chake," Faiz aliliambia gazeti la New York Times.

Lakini kwa upande mwingine, waangalizi wanakumbuka kile operesheni ya Oktoba 7 ilifichua kuhusu udhaifu wa huduma za ujasusi za Israeli.

Katika toleo lake la Novemba, gazeti la Jerusalem Strategic Tribune lilichapisha ripoti yenye kichwa cha habari "Kushindwa kwa Ujasusi wa Oktoba 7 - Mizizi na Masomo," ikisema kuwa shambulio la kushtukiza la Hamas katika maeneo ya Israeli "liliteka kabisa jeshi la mwisho na huduma za kijasusi mbali na walinzi."

Gazeti hilo lilisema kuwa "kukosekana kwa onyo la mapema siku hiyo kulisababisha machafuko, mkanganyiko na mashambulio ya kisasi yasitokuwa na uratibu."

Sayed Ghoneim aanaamini kwamba "Israel huenda ilitaka kuaibisha huduma za kijasusi za za Iran kumuua Haniyeh nchini Iran na kufichua matatizo yake, kama ilivyotokea kwa ujasusi wa Israeli mnamo Oktoba 7, ambayo iliacha uongozi wa ujasusi wa Israeli katika hali ya mshtuko na aibu kubwa."

Kwa upande wake, Iran inatishia kujibu kwa uchungu Israel. Je, kisasi hiki kitahesabiwa katika mfumo wa mizani ambayo imekuwepo kwa miaka, au itaenda zaidi ya mfumo huu wakati huu kwa kuzingatia kuongezeka kwa mvutano wa kikanda amb ao haujawahi kushuhudiwa kwa miongo kadhaa? Je, Israel itajibu hatua hii ya Iran? Ni jambo la kusubiri kuona.

Unaweza pia kusoma:

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi