Iran yasema Haniyeh aliuawa kwa ‘kombora la masafa mafupi’
Ripoti za vyombo vya habari vya Magharibi zinaonyesha kuwa idara ya siri ya Israel ilitega mabomu ndani ya jengo alilokuwa akiishi Ismail Haniyeh.
Muhtasari
- Iran yasema Haniyeh aliuawa kwa ‘kombora la umbali mfupi’
- Trump akubali mpango wa Fox News kufanya mdahalo na Harris
- Raia wanaompinga rais wa Urusi walioachiliwa walikataa kutia saini ombi la kutaka huruma kwa Putin
- Watu 37 wauawa katika shambulio Somalia - Polisi
- Marekani kutuma ndege na meli za kivita huku Iran ikitishia Israel
- Mashindano ya soka ya Olimpiki: Morocco na Misri zatinga nusu fainali
- Makubaliano ya kukiri mashtaka ya watuhumiwa wa shambulio la 9/11 yabatilishwa
- Mashindano ya Olimpiki 2024: Joshua Cheptegei wa Uganda ajishindia medali ya dhahabu
- Kamala Harris achaguliwa rasmi kuwa mteule wa chama cha Democratic
Moja kwa moja
Asha Juma
Iran yasema Haniyeh aliuawa kwa ‘kombora la masafa mafupi’

Chanzo cha picha, EPA
Jeshi la Iran Revolutionary Guard Corps (IRGC) limeishutumu Israel kwa kumuua mkuu wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh kwa kutumia "kombora la masafa mafupi" lililorushwa kutoka nje ya nyumba yake ya kulala mjini Tehran.
Kikosi hicho kilisema kuwa kombora hilo lilikuwa na uzito wa kilo 7 (lbs 16) na lilisababisha "mlipuko mkubwa", na kuwaua Haniyeh na mlinzi wake.
Kiongozi huyo wa Hamas alikuwa katika mji mkuu wa Iran kwa ajili ya hafla ya kuapishwa kwa Rais Massoud Pezeshkian.
Kikosi hicho pia kilishutumu Marekani kwa kuunga mkono operesheni hiyo. Israel haijatoa tamko lolote kuhusu kifo cha Haniyeh.
Taarifa ya IRGC ni kinyume na ripoti katika vyombo vya habari vya Magharibi, ambavyo vimedokeza kuwa vilipuzi viliwekwa katika makazi ya Haniyeh ya Tehran na maofisa wa Israeli.
Trump akubali mpango wa Fox News kufanya mdahalo na Harris

Chanzo cha picha, Reuters
Donald Trump amesema amekubali pendekezo la chombo cha utangazaji cha Marekani Fox News kufanya mdahalo na Makamu wa Rais Kamala Harris tarehe 4 Septemba.
Mdahalo kati ya rais wa zamani na rais aliyeko madarakani Joe Biden ulikuwa umeratibiwa kwenye chombo hasimu cha ABC News Septemba 10 na Bi Harris alikubali kuchukua nafasi ya Bw Biden.
Lakini Bw Trump alisema mdahalo wa ABC "ulikatizwa" na kuondoka kwa Bw Biden kwenye kinyang'anyiro hicho. Bi Harris bado hajatoa maoni juu ya pendekezo jipya la Fox News.
Wagombea hao wawili watakuwa debeni kuwania kiti cha urais mnamo tarehe 8 Novemba, baada ya Bi Harris kuchaguliwa rasmi kama mgombea wa chama cha Democratic siku ya Ijumaa.
Raia wanaompinga rais wa Urusi walioachiliwa walikataa kutia saini ombi la kutaka huruma kwa Putin

Chanzo cha picha, EPA
Raia wawili wa Urusi wanaompinga rais walioachiliwa huru katika mabadilishano ya wafungwa siku ya Alhamisi walisema walikataa kutia saini ombi rasmi la kutaka huruma kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin kama ilivyoombwa na maafisa wa magereza.
Wakati wa mkutano na waandishi wa habari nchini Ujerumani, Vladimir Kara-Murza na Ilya Yashin walisema hawakukiri kuwa na hatia wala kuwapa maafisa wa Urusi idhini yao ya kutaka kuachiliwa, na wakaapa kurejea nyumbani siku moja.
Bw Kara-Murza alisema mpango huo umeokoa "maisha 16 ya wanadamu" na kwamba alikuwa ameamini kwamba atafia gerezani.
Aliongeza kuwa Warusi wengi "walipinga vita vya Putin nchini Ukraine".
Wanaume hao wawili waliachiliwa kama sehemu ya mabadilishano ya wafungwa ambayo yalishuhudia watu 24 waliokuwa wamefungwa jela katika nchi saba tofauti wakiachiliwa huru.
Watu 37 wauawa katika shambulio Somalia - Polisi

Chanzo cha picha, EPA
Takriban watu 37 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya mshambuliaji wa kujitoa mhanga na watu wenye silaha kulenga eneo maarufu la ufukweni katika mji mkuu wa Somalia, msemaji wa polisi alisema Jumamosi.
Abdifatah Adan Hassan alisema karibu watu 247 walijeruhiwa, baadhi yao vibaya sana.
Picha za video zilionyesha miili kadhaa na watu waliojeruhiwa katika wilaya ya Abdiaziz mjini Mogadishu.
Vyombo vya habari vya ndani vinasema shambulio hilo lilitekelezwa na wanamgambo wa al-Shabab wanaodhibiti sehemu kubwa za kusini na katikati mwa Somalia.
Marekani kutuma ndege na meli za kivita huku Iran ikitishia Israel

Chanzo cha picha, Getty Images
Marekani itapeleka meli na ndege za kivita za ziada Mashariki ya Kati ili kusaidia kuilinda Israel dhidi ya mashambulizi ya Iran na washirika wake, Pentagon imesema
Mvutano bado unaendelea katika eneo hilo kuhusu mauaji ya kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh nchini Iran na kamanda mkuu wa kundi la wanamgambo wa Lebanon Hezbollah.
Vikosi vya ulinzi wa makombora viliwekwa kwenye hali ya utayari wa kutumwa, Pentagon ilisema, na kuongeza kuwa kujitolea kwake kuilinda Israel ni jambo "lisiloweza kubadilishwa".
Kiongozi wa Iran Ayatollah Khamenei ameapa "adhabu kali" dhidi ya Israel kwa mauaji ya Haniyeh, na kutangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa.
Kiongozi huyo wa Hamas aliuawa mjini Tehran siku ya Jumatano.
Iran na washirika wake huko Gaza walilaumu Israel kwa shambulio hilo, ambayo haijazungumzia lolote.
Haniyeh mwenye umri wa miaka 62, alichukuliwa kuwa kiongozi mkuu wa Hamas na alikuwa na jukumu muhimu katika mazungumzo yaliyolenga kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano katika vita vya Gaza.
Kifo chake kilitokea saa chache tu baada ya Israel kudai kuwa imemuua Fuad Shukr, kamanda mkuu wa kijeshi wa Hezbollah, nchini Lebanon.
Soma zaidi:
Mashindano ya soka ya Olimpiki: Morocco na Misri zatinga nusu fainali

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Achraf Hakimi (kushoto) na Ibrahim Adel (kulia) wote walifunga bao wakati Morocco na Misri zikitinga nusu fainali ya Olimpiki ya Paris 2024. Afrika itakuwa walau na medali moja katika mashindano ya soka ya Olimpiki ya wanaume baada ya Misri na Morocco zote kutinga nne bora.
Morocco ilianza na mafanikio maradufu kwa ushindi murua wa 4-0 dhidi ya Marekani kwenye uwanja wa Parc des Princes mjini Paris.
Mkwaju wa penalti kipindi cha kwanza wa Soufiane Rahimi - bao lake la tano kwenye michuano hiyo - uliipa Atlas Lions fursa ya kuongoza hadi wakati wa mapumziko.
Lakini katika kipindi cha pili ambacho kilionekana kuwa na bahati ya mtende kwao, Ilias Akhomach, nahodha Achraf Hakimi na penalti nyingine iliyofungwa na Mehdi Maouhoub ilimalizia mambo kwa mtindo wa kipekee.
Katika marudio ya mechi ya hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia la Qatar 2022, Morocco sasa itamenyana na Uhispania mjini Marseille Jumatatu (16:00 GMT) kuwania nafasi ya kutinga fainali.
Baada ya mechi hiyo, Hakimi alisifu uungwaji mkono mkubwa wa Morocco ambao umeisaidia timu hiyo nchini Ufaransa.
"Mashabiki wamekuwa wakitufuatilia katika mashindano yote," alisema mlinzi huyo ambaye anachezea soka uwanja wa Parc des Princes klabu la Paris St Germain.
"Natumai wanaweza kutufuata hadi fainali. Tunataka kuwafanya wawe na fahari."
Pia unaweza kusoma:
Makubaliano ya kukiri mashtaka ya watuhumiwa wa shambulio la 9/11 yabatilishwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin amebatilisha makubaliano ya kukiri mashtaka nje ya mahakama yaliyofikiwa na maofisa wa wizara hiyo pamoja na watuhumiwa wa shambulio la kigaidi la Septemba 11, 2001.
Kupitia taarifa aliyoitoa jana Ijumaa, Bw Austin amesema pia kuwa ametengua mamlaka ya ofisa anayesimamia mahakama za kijeshi ambaye alisaini makubaliano hayo siku ya Jumatano.
Makubaliano hayo, ambayo yanaripotiwa kuwa yalikuwa yanawakinga watuhumiwa hao na adhabu ya kifo, yalipingwa vikali na baadhi ya familia za waathirika wa shambulio hilo.
Taarifa ya Waziri huyo imewataja washtakiwa watano ambao wote wanashikiliwa kwenye jela ya kijeshi ya Guantanamo, ikiwemo anayetuhumiwa kusuka mpango wa mashambulizi, Khalid Sheikh Mohammed. Makubaliano yenyewe yalihusisha watuhumiwa watatu tu.
“Nimeamua kwamba, kwa kuzingatia uzito wa kuingia kwenye makubaliano ya nje ya mahakama na washtakiwa…Wajibu wa kufanya jambo hilo inabidi uwe wangu kama mtu mwenye mamlaka ya juu (katika wizara ya ulinzi),” Bw Lloyd alimuandikia Brigedia Jenerali Susan Escallier, ambaye ni kiongozi wa kamisheni inayosimamia mahakama za kijeshi huko Guantanamo.
"Hivyo basi, natengua mamalaka yako. Na kuanzia sasa, kama sehemu ya kutekeleza mamlaka niliyonayo, ninafuta makubaliano yote matatu ya nje ya mahakama.”
Ikulu ya White House ilijitenga na kuhusika kwa namna yeyote katika kufikiwa kwa makubaliano hayo siku ya Jumatano.
Watuhumiwa hao watano waliotajwa kwenye taarifa ya Bw Austin ni: Khalid Sheikh Mohammed, Walid Muhammad Salih Mubarak bin Attash, Mustafa Ahmed Adam al-Hawsawi; na wawili ambao hawakutajwa kwenye makubaliano ya Jumatano ni: Ramzi bin al-Shibh na Ali Abdul Aziz Ali.
Wanaume hao wamekuwa kizuizini bila kufunguliwa mashtaka kwa zaidi ya miongo miwili sasa. Moja ya sababu zinazotia ugumu wa kufunguliwa mashtaka rasmi ni tuhuma za matumizi ya mateso makali katika kuwahoji na kusaka ushahidi.
Kwa pamoja wanatuhumiwa kukeleza msururu wa makosa ya jinai, ikiwemo kushambulia raia, mauji ya kinyume cha sheria za vita, utekaji nyara na ugaidi.
Wanasiasa kadhaa kutoka chama cha Republican ambao walipinga makubaliano ya Jumatano wamempongeza Waziri Austin kwa kuyabatilisha.
Soma zaidi:
Mashindano ya Olimpiki 2024: Joshua Cheptegei wa Uganda ajishindia medali ya dhahabu

Joshua Cheptegei wa Uganda ameshinda mbio za mita 10,000 kwa wanaume - medali ya kwanza kupatikana katika riadha na kuipatia Afrika dhahabu yake ya pili katika mashindano ya Olimpiki ya Paris, 2024.
Cheptegei, mshikilizi wa rekodi ya dunia wa Uganda, alitoka mbio za kufa mtu katika raundi ya mwisho na kuweka rekodi mpya ya saa 26:43.14 akitia kibindoni medali ya dhahabu ya kwanza uwanjani Stade de France.
Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 27, na bingwa wa dunia mara tatu, alimaliza mbele ya Berihu Aregawi wa Ethiopia na mshindi wa medali ya shaba Grant Fisher, wa Marekani.
Pia unaweza kusoma:
Kamala Harris achaguliwa rasmi kuwa mgombea wa chama cha Democratic

Chanzo cha picha, Getty Images
Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris amepita idadi inayohitajika kushinda uteuzi wa kugombea tiketi ya urais kupitia chama chama cha Democratic katika kura ya wajumbe wa chama.
Akiongea kwa njia ya simu, Bi Harris alisema "naichukulia kwa heshima kubwa nafasi ya uwezekano wa kuwa mteule" kabla ya Kongamano la Kitaifa la chama cha Democratic litakalofanyika huko Chicago baadaye mwezi huu.
Bi Harris ndiye mwanamke wa kwanza Mwafrika na mwanamke wa kwanza kutoka Asia Kusini kupeperusha bendera ya kuelekea Ikulu ya White House katika chama kikuu cha kisiasa cha Marekani.
Ikiwa atamshinda Donald Trump, mgombea wa chama cha Republican katika uchaguzi wa mwezi Novemba, atakuwa rais wa kwanza mwanamke Marekani.
Alichaguliwa bila kupingwa katika uchaguzi huo baada ya Rais Joe Biden kujiondoa mwezi uliopita na kumuunga mkono kuwania nafasi hiyo.
Washindani wake kadhaa walifuata mkondo wake.
Siku ya Ijumaa alasiri, Bi Harris akawa mgombea rasmi baada ya kupata uungwaji mkono kutoka kwa wajumbe 2,350, idadi inayohitajika kuteuliwa.
Soma zaidi:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 03/08/2024
