Je, utakula wadudu ikiwa ni watamu?

cx

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Panzi wamekuwa wadudu wa majaribio katika ulaji wa wadudu
    • Author, Kelly Ng
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Zaidi ya wanasayansi 600, wafanyabiashara na wanamazingira kutoka kote ulimwenguni walikuwa Singapore katika safari ya kampeni ya kufanya wadudu kuliwa. Kauli mbiu ya mkutano huo ni - Wadudu wa Kulisha Ulimwengu.

Watu wapatao bilioni mbili, karibu robo ya idadi ya watu ulimwenguni, tayari wanakula wadudu kama sehemu ya lishe yao ya kila siku, kulingana na Umoja wa Mataifa.

Watetezi wa wadudu wanataka watu zaidi wale wadudu, na wanatetea kula wadudu kama chaguo bora kwa afya na kwa mazingira.

Pia unaweza kusoma

Wapishi wanasemaje?

qwxz

Chanzo cha picha, Insects to Feed the World.

Maelezo ya picha, Nicholas Low (wa tatu kulia) na Joseph Yoon (wa nne kulia) waliongoza timu iliyotayarisha chakula cha panzi na nyenje kwa ajili ya washiriki wa Insects to Feed the World.

"Lazima tuwafanye wadudu kuwa watamu," anasema mpishi anayeishi New York, Joseph Yoon, ambaye pamoja na mpishi wa Singapore, Nicholas Low walitengeneza nyenje wa kutafuna katika mkutano huo.

Tukio hilo liliruhusa matumizi ya jamii ya panzi pekee.

"Ni kweli wadudu wana dumu, wana virutubisho vingi, wanaweza kupambana na usalama wa chakula, na kadhalika, lakini hilo halitoshi kuwafanya wawe na ladha nzuri, achilia mbali mtu kuwa na hamu ya kula,” anasema Yoon.

Uchunguzi umegundua kuwa panzi wana protini nyingi. Na ufugaji wao unahitaji maji kidogo na ardhi ndogo, ikilinganishwa na mifugo ya wanyama.

Baadhi ya nchi zinaruhusu lishe ya wadudu. Hivi karibuni Singapore iliidhinisha aina 16 ya wadudu, wakiwemo nyenje, chavi, panzi na nyuki wa asali, kama chakula.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ni miongoni mwa nchi chache, ikiwa ni pamoja na Umoja wa Ulaya, Australia, New Zealand, Korea Kusini na Thailand, ambazo zinaruhusu polepole wadudu wanaoweza kuliwa.

Katika mkutano huo, Low alifanya ufundi kwenye mapishi maarufu ya tambi za supu ya samaki na kuweka nyenje wa kusaga balada ya samaki wa kusaga.

Low anasema, nyenje walikaangwa kwa wingi hadi waweze kuvunjika, na kisha husagwa hadi unga laini, hawawi tofuati na nyama.

"Sifikirii kupika nyenje kila siku, ni nkama sahani maalumu ambayo ni sehemu ya chakula kikuu."

Tangu Singapore iidhinishe upishi na mende, baadhi ya mikahawa imekuwa ikijaribu kupika mende. Wadudu jamii ya panzi wanakuwa ni mbadala wa nyama katika chakula chako pendwa.

Mgahawa wa Takeo Cafe wenye makao yake Tokyo, umekuwa ikiwahudumia wateja wake wadudu kwa miaka 10 iliyopita. Chakula hichi kinajumuisha mende na panzi.

Lakini mgahawa huo una vyakula vingine pia visivyokuwa wadudu. Kwani hawataki watu wasiokula wadudu wajisikie vibaya. Hakuna haja ya kula wadudu kwa lazima.

Chakula cha muda mrefu

cx
Maelezo ya picha, Wadudu kama kitafunio

Kwa karne nyingi, wadudu wamekuwa chanzo cha chakula katika sehemu mbalimbali za dunia.

“Huku Japani panzi, chavi, jamii ya nyuki, kwa kawaida walikuwa wakiliwa katika maeneo ya nchi kavu ambapo nyama na samaki zilikuwa chache. Ulaji wa wadudu uliibuka tena wakati wa uhaba wa chakula katika Vita vya Pili vya Dunia,” anasema meneja wa Takeo, Michiko Miura.

Leo hii, nyenje na chavi huuzwa kama vitafunio katika masoko ya usiku nchini Thailand, na huko Mexico City watu hulipa mamia ya dola kwa ajili ya mabuu ya mchwa, chakula ambacho hapo awali kilichukuliwa kuwa muhimu kwa Waazteki, watu waliotawala eneo hilo kuanzia Karne ya 14 hadi 16.

Kasumba

SD

Chanzo cha picha, Insects to Feed the World.

Maelezo ya picha, Singapore ni miongoni mwa nchi chache ambazo zinaruhusu mapishi ya wadudu wanaoliwa

Lakini wataalamu wa wadudu wana wasiwasi kwamba mila hizi za upishi zimekuwa zikibadilika, kwani watu wanaokula wadudu sasa wanahusishwa na ukosefu wa lishe na umaskini.

“Kuna hisia ya aibu inayoongezeka katika maeneo yenye historia ndefu ya utumiaji wa wadudu, kama vile Asia, Afrika na Amerika Kusini,” anasema Joseph Yoon, mpishi wa New York.

"Sasa wanapata mwanga wa tamaduni za kigeni kwenye mtandao na wanaona aibu kula wadudu kwa sababu hiyo ni desturi ambayo haipatikani mahala pengine."

Katika kitabu chake Edible Insects and Human Evolution, mwanaanthropolojia Julie Lesnik anasema, ukoloni ulizidisha unyanyapaa wa kula wadudu.

Aliandika kwamba Christopher Columbus na watu wa msafara wake walielezea ulaji wa Wamerekani wa asili wa wadudu kama "uhayawani mkubwa, kuliko uhayawani wa mnyama yeyote aliye juu ya uso wa dunia".

Bila shaka, mitazamo ya watu inaweza kubadilika.

Chakula cha Kijapan, Sushi kilianza kama cha wafanyakazi katika maduka ya barabarani. Na kamba, wanaojulikana kama "kuku wa mtu maskini," waliwahi kulishwa wafungwa na watumwa kaskazini-mashariki mwa Amerika kwa sababu ya wingi wao,” anasema mtafiti wa chakula Keri Matiwck kutoka Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Nanyang cha Singapore.

Lakini usafiri ulipokuwa rahisi na uhifadhi wa chakula kuboreshwa, watu wengi zaidi walianza kula vyakula. Na kadiri mahitaji yalivyoongezeka, ndivyo bei yake ilivyoongezeka.

“Vyakula vilivyowahi kuonekana kama vya kigeni, au visivyochukuliwa kuwa chakula, vinaweza kuwa vya kawaida kwa watu wengi,” anasema Dk Matwick.

“[Lakini] imani za kitamaduni huchukua muda kubadilika. Itachukua muda kubadili mitazamo ya wadudu kuwa ni wabaya na wachafu.”

Baadhi ya wataalamu wanahimiza watu kulea watoto wao kwa vyakula vya kigeni, wakiwemo wadudu, kwa sababu vizazi vijavyo vitakabiliwa na matokeo mabaya kutokana na madiliko ya tabia nchi.

Wadudu wanaweza kuwa "vyakula bora" vya siku zijazo, vinavyotamaniwa. Wanaweza kuliwa kwa huzuni, badala ya kutafutwa kwa furaha.

Kwa sasa, mpishi wa Singapore Nicholas Low anaamini hakuna kitu kinachowasukuma watu kubadilisha milo yao, hasa katika maeneo tajiri ambapo karibu chochote unachotaka ni kubofya tu.

Wateja wa kizazi kipya wanaweza kuwa tayari kuoja kutokana na udadisi, lakini haitokuwa rahisi. Kwani bado tunapenda nyama zetu kama nyama, na samaki wetu kama samaki."

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhanririwa na Yusuf Jumah