Tarajia kupata lishe ya wadudu hawa karibu na sokoni kwako

Chanzo cha picha, Hargol
Kwa muda mrefu imekuwa ikisemekana kwamba tunapswa kuanza kula wadudu ili kusaidia kuyahifadhi mazingira, lakini kwa wengi wetu sio ladha tunayoifikiria.
Kampuni moja ya Israeli ina matumaini ya kushinda fikra hizi kwa kuwaongezea wadudu ladha tamu.
Dror Tamir anafungua pakiti ya kahawia, yenye pipi laini. "Jaribu moja," anasema mkubwa wa kampuni ya teknolojia ya chakula Hargol.
Pipi hizi ndogo sio pipi za kawaida kwani zimesheheni protini, lakini sio ile ya nyama, soya au maharagwe. Badala yake protini hii inatokana na mdudu anayepaa-nzige, ambaye ni aina ya panzi.
"Panzi wenye ladha ya kama ya uyoga, kahawa na chokoleti ," anasema Tamir. " kwa aina zetu mbali mbali za chakula tunaweza kuongeza ndani ladha mbalimbali … ladha ya machungwa au ladha ya strawberry ."

Chanzo cha picha, Hargol
Mjasiliamali huyu wa Israeli anasema aliwapenda panzi alipokuwa bado angali mtoto, baada ya kusikia hadithi kutoka kwa bibi yake ambaye alikuwa mpishi katika shamba la pamoja.
"Nilijifunza kuhusu miaka ya 1950, wakati Israeli ilipokuwa na tatizo la usalama wa chakula pamoja na wimbi la nzige waliokuwa wakiikumba Afrika na kuharibu mimea ya mazao ," anasema.
Huku wakulima katika shamba la pamoja au kibbutz wakikimbilia shambani kuwafukuza panzi mbali, Wayemen na Wayahudi wa Morocco walikuwa wakikusanya tani za wadudu hao na kuwala.

Chanzo cha picha, Hargol
"Hapo ndipo nilipojua kuwa panzi ni chakula cha mabilioni ya watu duniani."
Wadudu hawa wamekuwa wakiliwa kwa muda mrefu na jamii za watu katika Afrika, Asia, Amerika ya Kati na Mashariki ya kati, lakini kwa wengi barani Ulaya na Amerika ya Kaskazini ulaji wao limesalia kuwa wazo lisilokubalika.
Bw Tamir anatumai kubadilisha yote hayo, na kampuni yake inakaribia kuanzisha bidhaa mbali mbali zinazotengenezwa kwa wadudu hao.
Kando na pipi kutakuwa na kinywaji cha kuongeza nguvu, baga na kashata au (falafel balls).
Kama bado unahisi kwamba wadudu hawatawahi kuwa sehemu ya mlo miongoni mwa wakazi wa nchi za magharaibi, baadhi ya wataalamu wanaamini kuwa hatimaye hakutakuwa na chaguo la kuwakataa kutokana na hofu za mazingira na makadirio ya ongezeko la watu duniani.
Kufikia mwaka 2050 idadi ya watu duniani inatarajiwa kuongezeka hadi bilioni 9.8 juu ya idadi ya sasa ambayo ni bilioni 7.7.

Chanzo cha picha, Hargol
Huku kukiwa na watu bilioni mbili wengine wa kuwalisha, baadhi wanasema kuwa ukulima wa zamani hautaweza kukidhi mahitaji ya chakula.
Na kwamba wakati huo huo, kula protini ya wadudu litakuwa ni jambo jema zaidi kwa uhifadhi wa mazingira kuliko utunzaji wa ng'ombe, kondoo na wanyama wengine.
"Protini ni muhimu katika milo yetu," anasema Profesa Robin May, mshauri mkuu wa kisayansi wa Mamlaka ya viwango vya chakula nchini Uingereza. " Lakini mara kwa mara baadhi ya vyakula vyetu vyenye protini nyingi hupatikana kwa uharibifu mkubwa wa mazingira au uvunjwaji wa maadili - bidhaa za nyama au , kwa mfano.
"Baadhi ya protini za wadudu, kama vile panzi au minyoo ya chakula, ni nafuu, rahisi kuwafuga, wana mafuta kidogo na wana madhara ya kiwango cha chini kwa mazingira kuliko nyama.

Chanzo cha picha, Getty Images
Hatahivyo Profesa Mat pia anatahadharisha kwamba baadhi ya maswali yanasalia kuhusu ulaji wa wadudu wanaofungwa.
Swali muhimu katika hatua hii, anasema ni iwapo baadhi ya protini za mdudu zimethibitisha kusababisha madhara kwa binadamu au kuathiri bakteria na vimelea wengine wanaoishi ndani ya miili yetu -microbiome.
Bw Tamir anaamini kuwa faida za mazingira ni sababu tosha ya kuwafanya wadudu kuwa sehemu ya mlo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mashamba ya kampuni yake ya nzige yaliyomo ndani ya majengo yenye nishati ya jua yanapatikana kaskazini mwa Israel.
"Tunaweza kuwazalisha nzige milioni 400 kwa mwaka katika mashamba yetu,"anasema Bw Tamir, ambaye anaongeza kuwa wadudu huchukua siku 29 tu kukua kikamilifu.
Alidai kuwa ikilinganishwa na uzalishaji wa nyama, ukulima wa nzige hupunguza utoaji wa gesi chafu kwa 99%, matumizi ya maji mara 1,000 na hupunguza kiasi cha matumizi ya ardhi kwa futi 1,500.
Ununuzi wa wadudu hawa unategemea ni nchi gani unayoishi. Nchini Uingereza unaweza kuwanunua kupitia makampuni ya mtandaoni kama vile EatGrub na Horizon Insects, ingawa wauzaji wangependa serikali ya Uingereza iondoe masharti ghali ya mauzo ya wadudu wanaoliwa.
Katika Muungano wa Ulaya, aina mbali mbali za nzige, wanaohama na minyoo wengine wa chakula kama wale wa rangi ya manjano -yellow mealworms walikubalika ma chakula mwaka huu.
Bw Tamir pia anasema kwamba nzige ni Koshel na halal, ikimaanisha kuwa wanaweza kuliwa na Wayahudi na Waislamu kwa pamoja.

Chanzo cha picha, Ynsect
Anasema utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na Chuo kikuu cha Maastricht unaonyesha kwamba protini ya wadudu ni yenye manufaa sawa na protini itokanayo na maziwa "Zote zina uwezo sawa katika umeng'enywaji, kuingia ndani ya mwili na uwezo wa kuchochea utengenezwaji wa misuli ," anasema Bw Hubert.
Hatahivyo Bridget Benelam, meneja wa mawasiliani katika Wakfu wa lishe wa Uingereza, anasema utafiti zaidi bado unahitajika.
Anasema maswali mengi yasiyo na majibu bado yanasalia kuhusu usalama wa ulaji wa baadhi ya aina za wadudu, ambao wanaweza kueneza sumu au dawa za wadudu kwa binadamu. "Hizi ni baadhi ya pingamizi ambazo zinapaswa kuondolewa iwapo kweli wadudu wataingizwa katika milo ."
Nchini Israel, Bw Tamir anakiri kwamba suala la watu kuwaona wadudu kama "wanaotia kinyaa " ni changamoto muhimu ambayo kiwanda chake kinakabiliana nayo. "Lakini ninaimani hivi karibuni kitakubalika, ni kama ulaji wa samaki mbichi katika Sushi ulivyokubalika."














