Mpango wa mabilioni ya dola kwa wanandoa kupata watoto zaidi

Chanzo cha picha, Getty Images
Ama iwe "sasa au isiwezekane milele," alionya waziri mkuu wa Japan, akimaanisha kupungua kwa kasi ya kuzaliana katika nchi yake.
Fumio Kishida alisema wiki chache zilizopita kwamba nchi yake inakaribia kufikia kiwango cha kutoweza kufanya kazi kama jamii kutokana na historia ya kiwango cha chini cha kuzaa: kwa mara ya kwanza katika zaidi ya karne moja idadi ya watoto waliozaliwa Japan ilipungua chini ya 800,000 mwaka jana, kulingana na makadirio rasmi.
Katika miaka ya 1970, idadi hiyo ilikuwa zaidi ya milioni mbili. "Kuzingatia sera zinazohusiana na watoto na malezi ya watoto ni suala ambalo haliwezi kusubiri au kuahirishwa," Kishida aliwaambia wabunge, na kuongeza kuwa ni moja ya masuala muhimu zaidi katika ajenda ya mkutano huu.
Ijapokuwa kupungua kwa kiwango cha kuzaliana ni jambo lililoenea sana katika nchi zilizoendelea, tatizo ni kubwa zaidi kwa Japan, kwa kuwa umri wa kuishi umeongezeka katika miongo ya hivi karibuni, ambayo ina maana kwamba kuna ongezeko la idadi ya wazee na idadi ya wafanyakazi wachache wa kuwasaidia inayoendelea kupungua.
Ukweli ni kwamba, Japan ndio nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu ulimwenguni, baada ya Monaco kidogo, kulingana na data kutoka Benki ya Dunia.
Ni vigumu sana kwa nchi yoyote ile kuendeleza uchumi wake wakati idadi kubwa ya watu inapostaafu, huduma za afya na mfumo wa pensheni unabanwa kwa kiwango cha juu, na idadi ya watu wa umri wa kufanya kazi inapungua.
Akikabiliwa na tatizo hili, Kishida alitangaza kuwa ataongeza maradufu matumizi ya fedha ya serikali kwa programu zinazounga mkono kuzaliana kupitia msaada wa malezi ya watoto.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kipi kinachangia idadi ndogo ya kuzaliana?
Kwa sasa, wastani wa idadi ya watoto ambao mwanamke wa Kijapani anao ni 1.3, mojawapo ya viwango vya chini zaidi duniani (Korea Kusini ina idadi ndogo zaidi na 0.78).

Chanzo cha picha, Getty Images
Kuna sababu nyingi za mgogoro huu wa/ idadi ya watu.
Baadhi yao ni ya kawaida katika nchi zilizoendelea na wengine ni mfano wa utamaduni wa Kijapani. Kati yao:
- gharama kubwa na shinikizo la juu la watoto kupata shule na vyuo vikuu bora
- kukosekana kwa usawa wa kijinsia katika kazi za nyumbani na kulea watoto
- vyumba vidogo katika miji mikubwa ambavyo havitoi nafasi kwa familia iliyopanuliwa
- kupanda kwa gharama ya maisha.
- kuongezeka kwa idadi ya wanawake wanaofanya kazi
- mahitaji makubwa ya kazi na muda mdogo sana wa kujitolea kutekeleza majukumu ya uzazi kikamilifu
- kuongezeka kwa idadi ya wanawake vijana wenye elimu ambao wanapendelea zaidi kubaki bila kuolewa na kutozaa watoto
- kuchelewesha kuzaa hadi umri unapokwenda hivyo basi, kupunguza idadi ya miaka ya kuzaa
Hizi ni baadhi tu ya sababu zinazochangia kupungua kwa idadi ya kuzaliana aeleza Tomas Sobotka, naibu mkurugenzi wa Taasisi ya Demografia huko Vienna, Austria.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Nchini Japani kuna tamaduni ya kufanya kazi kupindukia ambayo inahitaji muda mrefu wa kufanya kazi, kiwango cha juu cha kujitolea na utendaji wa juu kutoka kwa wafanyakazi," na kuacha nafasi ndogo sana ya kutunza watoto.
"Ni wazi kwamba usaidizi wa kifedha kwa familia unaweza kushughulikia sehemu tu ya changamoto za kupungua sana kwa idadi ya kuzaliana nchini," anaongeza.
Pamoja na hatua za kawaida za kifedha, Sobotka anasema, hazitoshi kufidia kwa kiasi kikubwa gharama ya juu ya kuwa na watoto.
Uhamiaji kama suluhisho linalowezekana
Serikali za Japani zimekataa uhamiaji kama suluhisho linalowezekana kwa uhaba mkubwa wa wafanyikazi na shinikizo linaloongezeka la ufadhili wa afya na usalama wa kijamii.
Rupert Wingfield-Hayes, mwandishi wa zamani wa BBC nchini Japani, anasema kwamba "uhasama dhidi ya wahamiaji bado unaendelea."

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ni takriban 3% tu ya wakazi wa Japani walizaliwa nje ya nchi, ikilinganishwa na 15% katika nchi nyingine kama Uingereza.
"Katika Ulaya na Marekani, vuguvugu za mrengo wa kulia zinaieleza kama mfano kwenye suala la ubaguzi wa rangi na maelewano ya kijamii. Lakini Japani si kwamba inaweza kukubali hilo moja kwa moja kama unavyoweza kufikiria," Wingfield-Hayes anaelezea.
"Ikiwa unataka kuona kitakachotokea kwa nchi ambayo inakataa uhamiaji kama suluhisho la kupungua kwa idadi ya kuzaliana, Japan ni mahali pazuri pa kuanzia," mwandishi wa habari anahitimisha.
Giovanni Peri, mwanzilishi na mkurugenzi wa Kituo cha Uhamiaji Ulimwenguni katika Chuo Kikuu cha California na mshirika wa utafiti katika Ofisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Kiuchumi huko Cambridge, Massachusetts, anasema uhamiaji ni muhimu kwa changamoto ya Wajapani.
"Idadi kubwa ya wahamiaji itakuwa njia mwafaka ya kukabiliana na kupungua kwa idadi ya watu na wafanyakazi.
"Hata hivyo, anaonya, "Sioni serikali ziko tayari kukubali wimbi kubwa la wahamiaji wanaohitajika kuruhusu idadi ya watu kuongezeka nchini Japani."
Kinachotokea Japan ni sehemu ya hali ya kimataifa inayoathiri nchi zilizoendelea.

Chanzo cha picha, Getty Images
Je, pesa ndiyo suluhisho?
Serikali ya Japan tayari imeweka wazi kuwa uhamiaji sio suluhisho lao na kuamua kutafuta pesa.
Mpango wa Waziri Mkuu Kishida ni kuongeza maradufu matumizi ya umma katika mipango inayojitolea kusaidia malezi ya watoto.
Lakini baadhi ya wachambuzi kama vile Poh Lin Tan, msomi katika Shule ya Sera ya Umma ya Lee Kuan Yew katika Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Singapore, wanasema kwamba katika nchi nyingine za Asia, kama vile Singapore, matumizi zaidi ya kifedha ili kuchochea viwango vya kuzaliana hayajafaulu.
Katika nchi hiyo, serikali inakabiliana na hali ya kushuka kwa kasi ya kuzaliana tangu miaka ya 1980.
Mnamo 2001, ilianzisha kifurushi cha motisha kiuchumi ili kuongeza kiwango cha kuzaliwa ambacho kilibadilika kwa muda.
Kwa sasa, Poh anasema, kifurushi hicho kinajumuisha likizo ya uzazi yenye malipo, ruzuku ya kulea watoto, mapumziko ya kodi na punguzo, zawadi za pesa taslimu na ruzuku kwa kampuni zinazotekeleza mipango ya kazi inayoweza kunyumbulika.
“Licha ya jitihada hizo, kiwango cha uzazi kiliendelea kupungua,” anasema mtaalamu huyo. Na kama vile imekuwa ikipungua nchini Japani na Singapore, inafanyika pia Korea Kusini, Taiwan, Hong Kong na miji ya Uchina yenye mapato ya juu kama Shanghai.















