Utafutaji wa Titan: Mfahamu bilionea Dawood aliyekwama katika nyambizi hiyo na mwanawe

Nyambizi iliyokwenda kutalii mabaki ya meli maarufu ya kitalii ya Titanic, imepotea tangu siku ya Jumapili na utafutaji unaendelea.

Kati ya abiria watano katika chombo hicho yumo mfanyabiashara - bilionea mzaliwa wa Pakistan, Shahzada Dawood na mtoto wake Suleiman Dawood.

Wengine ni mfanyabiashara bilionea raia wa Uingereza, Hamish Hardin, mvumbuzi wa Kifaransa Paul Henri Nargelet na mkurugenzi mkuu wa kampuni inayohusika na safari hiyo Stockton Rush.

Kabla ya kuanza safari, Harmish Harding aliandika kupitia mtandao wa kijamii, anajivunia kutangaza atakuwa sehemu ya safari ya kuelekea katika mabaki ya Titanic. Pia aliandika, “hii itakuwa safari ya mwisho kwa mwaka huu kwenda Newfoundland, kwa sababu msimu huu baridi imekuwa kali kwa mara ya kwanza tangu kupita kipindi cha miaka 40.”

Safari ya siku nane, kwa tiketi ya dola za kimarekani 250,000. Katika safari hii masalia ya Titanic huonekana kwa kwenda umbali wa mita 3,800 chini ya bahari.

Kwa mujibu wa Walinzi wa pwani ya Marekani, mawasiliano na nyambizi yalipotea baada ya saa moja na dakika 45, tangu safari iyanze. Walinzi wa pwani ya Marekani walisema siku ya Jumatatu usiku, nyambizi hiyo itakuwa na oksijeni ya kuwawezesha kuishi kwa siku nne.

Walinzi hao waliviyambia vyombo vya habari, “tunakadiria kutoka sasa, kutakuwa na masaa 70 hadi 96 yamebaki kukamilisha operesheni ya utafutaji.”

Vilevile walisema, eneo ambalo operesheni inafanyika ni gumu, kwa sababu kuna vikwazo vingi wamekutana navyo.

Prince Dawood ni nani?

Prince Dawood ni mwanaume kutoka familia ya kibiashara ya Kipakistani. Pia, ni mwanachama wa bodi ya Prince Trust - mfuko wa hisani wa Uingereza. Mtoto wake wa kiume, Suleiman pia yumo katika msafara huo.

Taarifa iliyotolewa na familia ya Dawood, “mtoto wetu Prince Dawood na mtoto wake, Suleiman walikwenda safari ya kuona mabaki ya Titanic katika bahari ya Atlantiki.

Wakati huu, nyambizi yao ndogo imepoteza mawasiliano na hatuna taarifa za kutosha kwa sasa. Juhudi zinaendelea zikiongozwa na serikali kadha na mashirika ya uvumbuzi wa chini ya bahari, ili kupata mawasiliano na nyambizi yao na kuwarudisha nyumbani.”

Familia ya Dawood, ni moja ya familia tajiri nchini Pakistan. Pia shughuli zao zimejikita Uingereza. Prince Dawood, ni makamu mwenyekiti wa Engro Corporation. Kampuni ya mbolea, chakula na nishati.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Uingereza, Prince Dawood alizaliwa Pakistan kisha akahamia Uingereza. Huko alisoma sheria katika chuo kikuu cha Backingham. Baadaye alisoma shahada ya pili kuhusu soko la nguo ulimwenguni, katika chuo kikuu cha Philadelphia.

Prince Dawood, ni mdhamini wa taasisi ya SETI, kampuni ya tafiti za anga za juu. Prince Dawood anaishi Uingereza na mke wake, Christine na watoto wao Suleiman na Alina. Ni mpenzi wa picha na wanyama.

Ni makamu mwenyekiti wa Dawood Heracles Corporation, ambayo ni sehemu ya kampuni ya Dawood Group. Familia hii imedumu katika biashara kwa zaidi ya karne moja.

Prince Dawood alianza kuwa sehemu ya biashara ya familia kuanzia 1996. Dawood Heracles Corporation inaendesha na kusimamia viwanda mbali mbali.

Prince Dawood amekuwa kiungo muhimu katika maendeleo na ubunifu katika eneo la nishati, kilimo, chakula, nguo na usafishaji wa mafuta.

Utafutaji umefikia wapi?

Utafutaji wa nyambizi iliyopotea katika bahari ya Atlantiki uliendelea kati ya Jumatatu na Jumanne usiku, lakini haikuonekana. Kutokana na muda kusonga, kasi ya utafutaji imeongezwa kwa vile inaaminika hakiba ya oksjini katika nyambizi haitadumu kwa muda mrefu.

Mbali na vikosi vya Marekani na Canada, kampuni zinazofanya kazi katika kina kirefu cha maji pia zinahusika. OceanGate kampuni inayotajwa kuratibu safari hiyo, inasema, kila liwezekanalo linafanywa ili kuokoa maisha ya watu waliomo katika chombo. Kwa msaada wa ndege mbili za kijeshi, sona na nyambizi.

David Pogue, ripota wa runinga ya CBS ambaye alisafiri kwa nyambizi hiyo mwaka jana, anasema, “pengine hakuna njia ya kuwasiliana na nyambizi kwa sababu redio na GPS hazifanyi kazi chini ya maji,” ameiambia BBC.

“Ujumbe unaweza kutumwa ikiwa meli itakuwa karibu na nyambizi. Lakini hadi sasa hakuna jawabu,” amesema na kuongeza, “hakuna njia nyingine ya kutoka nje ya nyambizi, kwa sababu watu waliomo ndani wanaweza kutolewa tu na watu waliopo nje.”

Safari ya kuifikia Titanic

Kwa mujibu wa tangazo la kampuni ya OceanGate, safari hii ya masaa nane ni nafasi ya kuvumbua vitu vya kuvutia nje ya vitu vya kawaida. Kwa mujibu wa tovuti ya kampuni, kuna mipango ya kufanya safari hizo mara mbili kuanzia 2024.

Nyambizi ndogo imebeba rubani na abiria watatu walionunua tiketi. Mbali na hao, mtaalamu pia yumo katika nyambizi. Safari yao ilianza St. John katika kisiwa cha Newfoundland, Canada.

Uzito wa nyambizi ni kilogramu 10432 na kwa mujibu wa tovuti, ina uwezo wa kwenda umbali wa futi 13100. Kuna oksijeni ya kudumu masaa 96 katika nyambizi.

Meli ya Titanic ilizama wakati wa safari yake ya kwanza kutoka New York 1912. Ilikuwa ni meli kubwa zaidi kwa wakati huo. Kati ya abiria na wafanyakazi wa meli 2200, zaidi ya 1500 walikufa. Mabaki ya meli yaligundulika kwa mara ya kwanza 1985.