"Ililipuka usoni mwangu": Je ajali za sufuria ya mvuke hutokea kiasi gani? na vipi unaweza kuziepuka?

Kila wiki, daktari Marcos Barretto, mwenye umri wa miaka 70, hupokea wagonjwa wenye simulizi inazofanana "Daktari, sufuria ililipuka."

Daktari huyo wa upasuaji, ambaye kwa miongo kadhaa amekuwa akisimamia kituo cha matibabu ya watu walioungua nchini Brazili, anasema kwamba angalau mtu mmoja kwa wiki kufika katika hospitali hiyo baada ya kupata ajali zinazosababishwa na aina hizi za sufuria zinazofahamika zaidi kama pressure cooker.

Barretto anakumbuka mifano fulani iliyotokea: wakati ambapo chakula cha kuchemsha kilikwama kwenye uso wa mgonjwa, au wakati mwingine ambapo mgonjwa alipoteza sehemu ya uwezo wake wa kuona.

Vijana wa umri wa miaka 12 au 13 ambao huanza kusaidia kazi za jikoni pia hufika katika hospitali hiyo baada ya kupata majeraha yanayosababishwa na ajali za sufuria hizo.

Licha ya kukabiliwa na mifano mingi ya kutisha kila wiki kazini, Barretto mwenyewe hajawahi kufikiria kuacha kutumia sufuria za mvuke.

“Nyumbani tunakitumia bila shida yoyote. Kupika, nyama, maharagwe," anasema. " Matumizi sahihi hayaleti hatari yoyote ."

Wataalamu wanashauri kuwa sufuria ya haipaswi kuacha kutumika.

" Kwa matengenezo ya kisasa, hatari ya ajali ya sufuria hii ni sifuri,” anasema mhandisi wa Sayansi ya Nyenzo Leandro Possamai.

"Hakuna cha kuogopa, kwa sababu matumizi yake ni salama. Lazima tukumbuke kuwa jikoni kimsingi ni mazingira hatarishi, huwezi kuwasha moto na kwenda kucheza na simu yako ya rununu, "anaongeza mpishi na profesa Zenir Dalla Costa.

Licha ya hayo, ajali zinaendelea kutokea , kama inavyoonyeshwa na video nyingi zinazoshirikiwa kwenye mitandao ya kijamii ambazo hunasa milipuko na hivyo kusababisha hofu miongoni mwa baadhi ya watu.

Idadi kubwa ya ajali, kulingana na wataalam, hutokana na kokosa habari juu ya usalama wa kifaa unachokitumia.

Jinsi ya Kupunguza uwezekano wa ajali za sufuria za mvuke

  • Soma mwongozo wa usalama wa sufuria uliyonunua ili kujua ni mara ngapi utunzaji wa kuzuia unapaswa kufanywa.
  • Daima angalia kwamba valvu ambapo mvuke hutoka ni wazi na safi.
  • Usijaze sufuria zaidi ya kiwango cha juu cha mtengenezaji (kwa ujumla theluthi mbili kamili). na kumbuka kuwa kuna vyakula vinavyoumuka vinapopikwa.
  • Kamwe usitumie sufuria bila maji.
  • Usiwahi kutumia vyombo ndani ya jiko, kama vile makopo ya maziwa ambayo yanaweza kulipuka kutokana na shinikizo la ndani.
  • Angalia ikiwa kifuniko kimefungwa kwa usalama.
  • Unapozima moto, basi sufuria iwe baridi na kutolewa shinikizo kwa kawaida (kamwe usivute valve na uma, kwa mfano, ili usijichome kwa mvuke).
  • Ikiwa unataka kuharakisha mchakato wa baridi na kutolewa kwa shinikizo, unaweza kumwaga maji baridi kwenye sufuria (lakini kuwa mwangalifu usiingize maji kwenye valvu ambapo mvuke hutoka).
  • Kamwe usifungue kifuniko hadi mvuke wote utoke.
  • Ikiwa sufuria haifikii shinikizo, zima moto mara moja na usubiri ili baridi.

"Nilikaa hospitalini kwa siku tisa uso wangu ukiwa umeungua"

Lucileide Maria da Silva, 52, alikuwa akipika chakula cha mchana nyumbani wakati mambo yalipoharibika

Alikuwa akigeuza wali kwenye moja ya majiko huku maharage yakipikwa kwenye sufuria ya mvuke upande mwingine. Hapo ndipo kilipolipuka. Maharage yakaruka na kutua kwenye uso wake .

“Kitu pekee nilichoweza kufanya ni kufunga macho yangu na kuhisi mvuke wa moto usoni mwangu. Nilimfokea mwanangu, ‘Nisaidie hapa,’” anakumbuka.

Paa la nyumba liliharibika na vioo vya madirisha ya nyumba ya mama nyumba vilivunjika.

Familia ya Lucileide ilimpeleka kwenye kituo cha afya. Hakumbuki maumivu mengi, tu kwamba uso wake ulikuwa bado mchafu.

Lakini matokeo yake yalikuwa ni majeraha ya moto pili usoni mwake, kwa hiyo alilazimika kulazwa hospitalini kwa siku tisa.

Baada ya kupigwa sindano ya ganzi , alipitia taratibu za kusafisha uso wake na akapewa dawa.

Kama ilivyo katika hali nyingi, kilichosababisha mlipuko huo ni ukosefu wa uelewa wa jinsi sufuria ya mvuke inavyofanya kazi .

Je! kuna tofauti gani kati ya sufuria "ya kawaida" na sufuria ya mvuke?

"Japo inaweza kuonekana kuwa la kushangaza, hatokuwa na habari kwamba valve inapaswa kufunguka ili mvuke utoke na sio kulipuka.

Nawaambia hapa, ninawahakikishia kwamba watu wengi hawaijui.”

Ukosefu wa habari "huchoma"

Moja ya vidokezo muhimu vya kuzuia sufuria ya mvuke kulipuka ni kuzingatia kila wakati valvu.

Pia ni muhimu kubadili mpira unaofunga kifuniko ikiwa umelegea.

Katika Taasisi ya Shirikisho ya Goiás, ambako anafundisha fizikia, Profesa Leandro Possamai amebuni mradi wa kutumia sufuria ya mvuke kama mfano halisi darasani.

Wazo ni kuonyesha kuwa vitu vya kila siku "havifanyi kazi kwa sababu tu."

"Hatuoni fizikia inayohusika katika vifaa hivi vya kila siku. Na wanafunzi wanakubali sana tunapofundisha kwa mfano huu.”

Mwalimu anaelezea wanafunzi wa shule ya sekondari, kwa mfano, kwamba sufuria inapofikia shinikizo, tunaweza kupunguza joto kwa sababu maji tayari yamefikia joto la juu ndani ya sufuria, na kwamba hii inapunguza muda wa kupika na gharama ya gesi.

Na sio tu kwa uchumi (muda na pesa) kwamba sufuria ya mvuke ni muhimu pia kwa ubora wa baadhi ya vyakula.

Maharage, kwa mfano, yana ubora zaidi ikiwa yamepikwa kwenye jiko hili anasema Dalla Costa. "Ukizipika kwenye sufuria ya kawaida, mbali na kiasi kikubwa cha gesi inayotumiwa, maharagwe yatakuwa meusi zaidi, na hayatakuwa sawa."

Unapaswa kuwa mwangalifu na vyakula vinavyolegeza ngozi, kama vile mbaazi na aina fulani za maharagwe. Ikiwa sufuria imejaa sana, ngozi hii inaweza kuishia kuziba valve.

"Kwa ujumla, hilo linapotokea, maji hutoka kupitia valvu," anasema Dalla Costa. " Chungu daima hutoa ishara kwamba kuna kitu hakifanyi kazi ."

"Hivyo ndivyo ninavyosema kila wakati: huwezi kukiacha chungu au surufia hapo na uende zako. Mapishi jikoni hayafanyiki hivyo ."