Mivutano inayochochewa na wakwe katika ndoa

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Megan Carnegie
- Nafasi, BBC
Utafiti wa 2012 kutoka Chuo Kikuu cha Purdue, Marekani, unaonyesha idadi kubwa ya wanandoa wanaingia kwenye ndoa zao wakitarajia uhusiano mzuri na wakwe zao.
Lakini mifano halisi ya uhusiano mbaya na wakwe ipo mingi - mfano mwanamuziki Zayn Malik na mama mkwe wake Yolanda Hadid, au ugomvi wa Victoria Beckham na mke wa mtoto wake Brooklyn, Nicola Peltz.
Mazingira hatarishi
Profesa wa Chuo Kikuu cha Canterbury, New Zealand, na mwandishi katika jarida la Mahusiano, Gretchen Perry anadokeza kwamba, miundo ya baadhi ya familia kwa kiasi fulani hujenga mazingira ya mvutano na wakwe.
Katika baadhi ya jamii - wazazi huchagua mtoto wao aolewe na nani au amuoe nani na mara baada ya ndoa - mke huhamia katika nyumba ya familia ya mume wake.
Kama mama mkwe ndiye mkuu wa kaya - ndiye anayesimamia kila jambo nyumbani, na kufanya maamuzi juu ya binti-mkwe wake. “Haya ni mazingira hatarishi,” anasema Perry. "Yanaweza kuwa mazingira magumu yenye migogoro mingi."
Aaina hizi za mpangilio wa familia ni nyingi sana katika maisha ya sasa. Na takwimu zinaunga mkono imani kwamba mke na mama-mkwe wana uwezekano mkubwa zaidi wa kugombana kuliko wana familia wa kiume.
Katika utafiti wa Marekani wa mwaka wa 2022, wanaume na wanawake waliripoti kuwa na migogoro mingi na mama wakwe zao wa kike kuliko mama zao wazazi, na akina mama walionyesha kuwa na migogoro zaidi na wakwe zao wa kike kuliko binti za wa kuwazaa.
Terri Apter, mhadhiri na mwanasaikolojia katika Chuo Kikuu cha Cambridge, ambaye alifanya utafiti wa zaidi ya miongo miwili, na kuchapishwa katika kitabu mwaka 2008 , 60% ya wanawake walikiri uhusiano na wakwe zao wa kike ulisababisha ukosefu wa furaha na wasiwasi.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Utafiti unaeleza asilimia 75 ya wanandoa waliripoti kuwa na mivutano na wakwe zao, lakini ni asilimia 15 tu ya mivutano hiyo ndiyo ilielezwa kuwa mibaya mno.
Sababu moja inayoweza kuchangia mvutano na mama mkwe ni ulezi wa watoto - hasa pakiwepo na migogoro yoyote iliyokuwepo hapo awali.
Katika utafiti mwingine watafiti waligundua wanandoa wasio na watoto, mke wa mume waliripoti zaidi kuwa na migogoro na wazazi wao wenyewe. Wana ndoa wengi waliripoti kuwa na mizozo zaidi na wakwe zao baada ya kuzaliwa mtoto wao wa kwanza, kwa sababu ya wakwe kutaka kuwa na "usemi na kuingilia maisha yao."
Katika kipindi cha malezi ya watoto wachanga, mama mkwe na binti mkwe huwasiliana mara kwa mara zaidi kuliko awali. "Wakati wa ujauzito, kunyonyesha na kutunza mtoto mchanga, akina binti mkwe hukabiliana na wakati mgumu. Pale mama mkwe anapovutana na binti mkwe juu ya malezi ya mtoto," anaeleza Perry.
Utafiti wa huo uligundua kadiri mama mkwe na binti mkwe wanavyokuwa karibu katika maisha ya kila mmoja wao, ndivyo fursa nyingi zaidi za kugombana hutokea.
Matukio hatarishi

Chanzo cha picha, Getty Images
Uhusiano wa mama-mkwe na binti-mkwe pia huwa mgumu wakati wa sherehe za kidini na likizo. "Ikiwa familia zote mbili za wakwe wanataka muende kwao kwa Krismasi, shida huanzia hapo," anasema Profesa wa saikolojia wa Chuo Kikuu cha McMaster, Canada - Martin Daly. "Sherehe za Krismasi ni sehemu kuu ya migogoro, kwa sababu ndipo watu wanapotarajiwa kuwa pamoja."
Melanie Booth-Butterfield, profesa wa masomo ya mawasiliano katika Chuo Kikuu cha West Virginia, Marekani, ambaye anaandika kitabu kuhusu mada hiyo, anasema athari mbaya za mivutano zinaweza kudumu kwa muda mrefu. "Ugomvi wa kupita kiasi unaweza kusababisha migogoro na watu wa ukoo, matusi, kuvunjiana heshima na kuacha hisia mbaya za kudumu," anaeleza.
Sikukuu ni wakati ambapo familia huwa karibu zaidi kama ilivyo mila na desturi. Hata hivyo, mila za kila familia zinaweza kuwa tofauti - na wakwe wanapotofautiana na mila na desturi tunazozipenda (au kinyume chake), mivutano inaweza kuzuka.
Utafiti uliofanywa 2016 na taasisi ya Fatherly - ulionyesha kati ya wanandoa wanaogombana na wakwe zao, 29% walisema ni kuhusu mtindo wa malezi, 15% kuhusu siasa, 14% walisema ni pesa na 4% ni maneno ya wakwe zao kuhusu kazi zao.
Bado kuna matumaini

Chanzo cha picha, Getty Images
Pia mivutano inaweza kutokea ikiwa wanandoa hawawezi kumudu maisha ya kujitegemea, babu na bibi hubeba majukumu zaidi ya malezi ya wajukuu.
"Ikiwa changamoto za maisha na upungufu wa fedha vitawafanya watu kutumia muda mwingi zaidi pamoja - migogoro inaweza kuongezeka," anasema Perry.
Ingawa baadhi ya watu wanaweza kuhangaika na uhusiano na wakwe - pia wanaweza kujenga mahusiano mazuri na yenye kuridhisha. Uchunguzi kwa wanawake wa Marekani uliofanywa mwaka 2021 uligundua 51% ya mbinti wakwe wanafurahia uhusiano na wakwe zao, wakati robo tatu ya wakwe wanafurahia uhusiano na binti-wakwe zao.
Hilo linatuacha wapi? Kuna uwezekano baadhi ya maeneo ya migogoro na wakwe yanaweza kupunguzwa - watu hupitia mabadiliko mengi maishani, na kuna fursa nyingi za kurekebisha mahusiano na wakwe - hata wakati wa likizo.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












