Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ishara 4 zinazoonyesha kuwa unahitaji miwani mpya kwa matatizo ya macho
Dk. Mark T. Dunbar, mkurugenzi wa huduma za macho katika Taasisi ya Macho ya Bascom Palmer katika Chuo Kikuu cha Miami (Marekani) - inayotambuliwa kama mojawapo ya kliniki bora za macho nchini Marekani - anapendekeza kwamba ukaguzi huo uwe wa kila mwaka.
"Katika hali fulani, unaweza kuipata kila baada ya miaka miwili, lakini inapaswa kuwa kila mwaka," Dunbar aliambia BBC Mundo,
Pamoja na umuhimu wa kuhakikisha macho yako yanaona vizuri, wapo wengi wetu ambao huchukulia afya ya macho yetu kuwa ya kawaida, ama kwa sababu tunaona vizuri au kwa sababu, wakati fulani, tulienda kwa daktari wa macho kuchukua miwani na tukaacha kufuatilia tena afya ya macho.
Na pia "Sisi ambao tumekuwa tukiona vizuri kwa maisha yetu yote tumechukulia hili kuwa jambo la kawaida," anasema Dunbar.
"Sisi wenye umri wa miaka 40 au 50 ambao hatujawahi kupimwa macho."
Dunbar anaeleza baadhi ya ishara zinazoonyesha kuwa ni wakati wa kwenda kwa daktari wa macho, ama kwa mara ya kwanza au kubadilisha miwani yako.
1. Ugumu wa kuona wakati wa kuendesha gari
Kwa mujibu wa Dk. Dunbar, "Wakati ghafla unajaribu kusoma ishara za barabarani na huwezi kuiona hadi uwe umeifikia kabisa, kwa kawaida hiyo ni ishara ya onyo."
Kama kamera, macho yako yanahitaji kuelekeza nuru kwenye retina ili kuona vizuri.
Unapokuwa na tatizo kama vile kutoona karibu, mwanga huelekezwa mbele ya retina, ambayo inaweza kufanya vitu vilivyo mbali, kama vile ishara za barabarani, vionekane na ukungu.
Kuendesha gari katika hali hii inaweza kuwa changamoto hasa usiku.
Kile kinachofanywa na miwani kwenye macho yako ni kuongeza sio tu mwanga unaoingia, lakini pia kwamba usambazaji wake unafanywa kwa usahihi katika uso wote.
Kwa kuongeza, teknolojia mpya ya lenzi ya kuzuia kuakisi husaidia kupunguza mwangaza ili uweze kuona kwa uwazi zaidi.
2. Ugumu wa kuona karibu
Ukijipata unapata tabu sana unaposoma vitabu au wakati unaangalia skrini ya simu yako, hata ikiwa umevaa miwani, ni ishara kwamba unahitaji kumuona daktari wa macho ili akupe tiba mpya.
Ugonjwa wa Presbyopia huu hutokea kadiri unavyozeeka na lenzi ya macho yetu hupoteza uwezo wa kunyumbulika, hivyo kufanya iwe vigumu kuzingatia vitu vilivyo karibu.
Dk. Dunbar anadokeza kwamba afya ya jicho inaweza kuwa nzuri, lakini tatizo liko katika kunyumbulishwa kwa mwanga. Ikiwa haijaangaziwa vizuri kwenye retina, picha inaweza kuonekana kuwa na ukungu.
Miwani hurekebisha tatizo hilo na kuzuia kujivuta sana kwa jicho wakati wa kujaribu kusoma.
3. Kuona kunakobadilika-badilika wakati wa mchana
Ikiwa utagundua kwamba uwezo wako wa kuona unabadilika badilika siku nzima, hii inaweza kuwa ishara nyingine kwamba unahitaji kubadilisha lenzi zako.
Dk. Dunbar anaeleza kuwa moja ya sababu kuu ya macho kujivuta sana kwa macho kunaosababishwa na uchovu wa misuli ya macho.
Ukizingatia katika eneo moja kwa muda mrefu, kama vile unapofanya kazi kwenye skrini, macho yako yanaweza kuchoka na uwezo wako wa kuzingatia unaweza kupungua.
"Unapofanya kazi ambayo inahitaji unatuliza akili yako kabisa kwa kazi hiyo, kama kufanya kazi kwenye kompyuta, au kutazama filamu, au kusoma kitabu, kasi yetu ya kupepesa macho hupungua, labda hadi nusu ya kawaida."
Hali hii inaweza kuwa mbaya zaidi, ikiwa macho yako yanajivuta sana, ukijaribu kukabiliana na upungufu fulani wa kuona ulio nao, na kukuacha ukiwa na macho yamechoka, na kuona vibaya zaidi kuelekea mwisho wa siku.
Ikiwa hii ndio hali yako, labda ni wakati wako wa kutembelea daktari wa macho.
4. Kubadilika kwa uwezo wa kuona katika jicho moja au yote mawili
Mabadiliko ya kuono ya haraka katika jicho moja au yote mawili inaweza kuwa ishara kwamba kuna jambo lisilo la kawaida linaloendelea.
Kulingana na Dk. Dunbar, "Ikiwa huoni vizuri, kubadilisha miwani yako inaweza kuwa kitu muhimu zaidi."
Kwa mfano, kupoteza uwezo wa kuona kwa muda mfupi kunaweza kuwa ishara ya mtoto wa jicho, kama Dk. Dunbar anavyosema, inaweza kusababisha ugumu wa kuona vizuri, shida ya kuendesha gari usiku, na ugumu wa kutuliza akili kwa kazi fulani.
“Kwa teknolojia tuliyonayo hivi sasa, upasuaji wa mtoto wa jicho kunaweza kufanya kwa dakika 15,” anasema mtaalamu huyo.
Katika hali mbaya zaidi, afya ya macho inaweza pia kusaidia kutambua matatizo makubwa zaidi kama vile kisukari na shinikizo la damu, ambayo inaweza kusababisha mabadiliko katika mishipa ya damu ya jicho.