Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwanini maparachichi yana utata na ni mabaya kwa mazingira?
Mahitaji ya parachichi barani Ulaya na Amerika Kaskazini yameongezeka mara tatu uzalishaji wa kimataifa katika kipindi cha zaidi ya miaka 20.
Hata hivyo, tunda hili maarufu linazidi kuleta utata kutokana na athari za kimazingira zinazotokana na kilimo na usambazaji wake duniani kote.
Matatizo haya si asili ya parachichi zenyewe, ambazo zinaweza kuwa sehemu ya lishe endelevu na yenye afya, lakini badala yake huakisi baadhi ya matatizo ya kina yanayohusiana na uzalishaji wao.
Parachichi asili yake ni Amerika ya Kati na Kusini, ambapo hali ya hewa ya joto na baridi hutoa hali bora ya kukua.
Kuna mamia ya aina za parachichi , hata hivyo, moja ambayo wengi wetu tunaijua leo ni aina ya Hass, ambayo humea hadi kwenye mti mmoja uliopandwa karibu miaka 100 iliyopita.
Sehemu ya kuongezeka kwa umaarufu wa parachichi katika miongo ya hivi karibuni ni kutokana na uuzaji wake kama "vyakula bora zaidi."
Ingawa madai fulani kuhusu manufaa yake ya kiafya yanaweza kuwa yametiwa chumvi, ni kweli kwamba parachichi ni chanzo kizuri cha vitamini, madini, na mafuta yasiyokolea , ambayo huzipa mwonekano wa rangi ya maziwa au krimu.
Mbona maparachichi yana utata sana?
Kama ilivyo kwa kilimo cha kisasa, mashamba mengi ya parachichi yanategemea sana mbolea na mafuta, na hivyo kuchangia kuongezeka kwa uzalishaji wa gesi chafuzi.
Yana mavuno kidogo kuliko mazao mengine mengi na kwa hivyo yana kiwango kikubwa cha kaboni kwa kila kilo ya matunda.
Kwa wastani, parachichi lina alama ya kaboni ya karibu kilo 2.5 ya CO₂ (kg CO₂e) kwa kilo; yaani, gesi chafuzi zote zinazotokana na uzalishaji na usafirishaji wa parachichi, kama vile kaboni dioksidi , methane na nitrojeni okside , iliyojumuishwa katika kaboni(CO₂) sawa na ongezeko la joto.
Kiwango cha kaboni ya parachichi ni zaidi ya mara mbili ya ndizi (0.9 kg CO₂e kwa kilo) na zaidi ya mara tano ya tufaha (0.4 kg CO₂e kwa kilo), ingawa ni mbaya kidogo tu kuliko ile ya nyanya (kilo 2 za CO₂e kwa kila kilo).
Lakini idadi hizi ni ndogo ikilinganishwa na kiwango cha wastani cha kaboni duniani cha bidhaa nyingi za wanyama.
Kilo moja ya mayai ina alama ya kaboni ya kilo 4.6 ya CO₂, kilo moja ya kuku ina alama ya kaboni ya kilo 9.8 ya CO₂e na kilo moja ya nyama ya ng'ombe ina alama ya kaboni ya kilo 85 ya CO₂ kwa wastani.
Kwa wale wanaoishi nje ya Amerika, umbali mkubwa ambao parachichi husafiri kwa kawaida huenda usiwe muhimu kama inavyoaminika kawaida, angalau katika maneno ya kaboni.
Idadi kubwa ya parachichi husafirishwa kwa meli, ambayo ina maana ya utoaji wa hewa ya chini ya kaboni kutokana na kiasi kikubwa kinachoweza kusafirishwa kwa safari moja.
Hata wakati wa kusafiri maelfu ya kilomita, usafiri wa baharini hutoa kilo 0.2 tu ya CO₂e kwa kila kilo ya parachichi, ambayo kwa kawaida ni chini ya kiwango cha kaboni cha kuikuza.
Usafiri wa baharini huleta matatizo mengine.
Msongamano wa magari na vikwazo (kwa mfano, kuziba kwa Mfereji wa Suez na meli ya kontena mwaka wa 2021), njaa au vita katika sehemu moja ya dunia vinaweza kusababisha usumbufu au upungufu wa chakula katika nchi nyingine nyingi.
Shida inaweza kuwa mbaya zaidi kadiri mzozo wa hali ya hewa unavyozidi kuongezeka.
Tatizo hili si la parachichi pekee, lakini kuhamia kwenye uzalishaji zaidi wa chakula kutoka ndani kunaweza kujenga ustahimilivu zaidi na kusaidia kujilinda dhidi ya uhaba wa chakula siku zijazo.
Mzigo wa mazingira
Miti ya parachichi ni mimea yenye kiu sana, inayohitaji wastani wa lita 1,000 za maji kwa kilo.
Kiasi hiki ni kikubwa kuliko matunda na mboga nyingi, lakini ni cha chini kuliko nafaka zingine kama vile mchele.
Tatizo kuu ni kwamba parachichi hupandwa katika maeneo ambayo yanakabiliwa na shida ya maji.
Mexico, mzalishaji mkubwa zaidi wa parachichi duniani, inakabiliwa na vipindi virefu vya ukame, kwa hivyo umwagiliaji wa mashamba ya parachichi unaweza kuwa unadhoofisha upatikanaji wa maji kwa wenyeji.
Tatizo hili la usambazaji wa maji wa haki linaweza kuwa baya zaidi katika miongo ijayo.
Athari kwa asili lazima pia zizingatiwe.
Kijadi, miti ya parachichi ilipandwa katika mashamba mchanganyiko na mazao mengine na kuvunwa kama chakula cha kujikimu, na mazao ya ziada pekee ndio yaliyosafirishwa nje ya nchi.
Zoezi hili lilibadilika kadiri mahitaji yalivyoongezeka nchini Marekani na Ulaya.
Parachichi sasa hukuzwa kama bidhaa ya kuuza nje, na uzalishaji unahamia kwenye mashamba makubwa ya kilimo kimoja ili kuongeza tija.
Kilimo hiki kimoja kimehamisha mazao mengine asilia na huathirika zaidi na wadudu na magonjwa kuliko mashamba mchanganyiko.
Yote hii ina maana kwamba kiasi kikubwa cha dawa za kemikali na mbolea za synthetic zinahitajika kutumika, ambazo, kwa upande wake, huathiri vibaya viumbe hai, ubora wa udongo na afya ya binadamu.
Mbaya zaidi, katika baadhi ya maeneo mashamba mapya ya parachichi yanasababisha ukataji miti.
Hadi heka 25,000 za misitu hukatwa kila mwaka katika jimbo la Michoacán, eneo kuu la Mexico linalozalisha parachichi, ambalo huzalisha parachichi nyingi zinazouzwa Marekani.
Michoacán ina msitu mkubwa ambao ni makao ya wanyama kadhaa walio hatarini kutoweka, kama vile jaguar, puma, na koyoti.
Kwa hivyo, kuongezeka kwa uzalishaji wa parachichi katika eneo hili kunaweza kuwa tishio kubwa kwa bioanuwai.
Hatimaye, athari za binadamu lazima zizingatiwe.
Ingawa biashara ya parachichi inaweza kusaidia wakazi wa eneo hilo kwa kutoa mapato kwa wakulima, wao pia ndio wanaobeba mzigo mkubwa wa matatizo ya kimazingira.
Zaidi ya hayo, mashamba ya parachichi yamehusishwa na uhalifu uliopangwa na ukiukaji wa haki za binadamu, na baadhi ya miji na miji imechoshwa na matatizo hivi kwamba imepiga marufuku parachichi kabisa.
Kwa bahati mbaya, hakuna majibu rahisi.
Kutafuta biashara ya haki au parachichi zinazozalishwa kwa njia ya kikaboni kunaweza kusaidia katika suala la athari za binadamu na viumbe hai, lakini michakato ya uidhinishaji si kamilifu na mara nyingi huwa ghali sana kwa wakulima wadogo katika nchi zinazoendelea.
Zaidi ya hayo, huenda zisitoe hewa chafu kidogo kuliko mashamba ya kilimo kimoja.
Parachichi sio chakula pekee chenye mzigo wa mazingira.
Zina kiwango kidogo zaidi cha kaboni kuliko bidhaa nyingi za wanyama na ni moja tu ya mazao mengi ambapo aina moja hutawala soko.
Lakini hatupaswi kudharau uharibifu ambao uzalishaji wa parachichi unasababisha kwa asili na wakazi wa eneo hilo.
Ushauri bora kwa watumiaji unaweza kuwa kuzingatia aina mbadala za parachichi inapowezekana ili kupunguza mahitaji ya mashamba ya kilimo kimoja.
Wakati hazipatikani, chaguo bora zaidi labda ni kujaribu kuona parachichi kama tiba badala ya chakula kikuu cha kawaida.
imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi