Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwanini Tanzania inavutiwa na uchaguzi wa Kenya
Katika mfululizo makala kutoka kwa waandishi wa Afrika, Mwanahabari wa Tanzania Sammy Awami anapendekeza kwamba nchi yake inaweza kuiona Kenya kama mfano wake wa kuigwa kisiasa.
Watanzania wamekuwa wakichungulia katika boma la jirani yao Kenya wakiwa na hisia mchanganyiko za kuvutiwa na wivu kufuatia uchaguzi uliofana na wiki hii kukabidhiwa madaraka kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta hadi kwa mpinzani wake mshirika, William Ruto.
Hatukuweza kujizuia kutazama kwa macho huku mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini Kenya akidhihirisha uhuru wake kwa kumtangaza Bw Ruto kuwa mshindi na Mahakama ya Juu ikathibitisha ushindi wake licha ya kwamba Rais wa wakati huo Kenyatta alikuwa akimuunga mkono mpinzani wake, Raila Odinga.
Ijapokuwa wajumbe wanne wa tume ya uchaguzi walikataa matokeo na Bw Odinga alidai kuwa kulikuwa na udanganyifu mkubwa, Mahakama ya Juu iliamua kwamba Bw Ruto alishinda katika kinyang'anyiro cha uchaguzi huru na haki uamuzi ambao Wakenya wengi wanaonekana kukubali.
Chama tawala cha Tanzania, Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho kimekuwa madarakani kwa zaidi ya nusu karne, lazima kimeshangazwa vile vile kwa matokeo kwenda kinyume na Bw Odinga.
Kabla ya uchaguzi mkuu wa Tanzania 2015, Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM wa wakati huo, Nape Nnauye aliahidi chama chake kitashinda uchaguzi huo kwa njia zote - hata kwa "bao la mkono" ikibidi.
Katika uchaguzi uliofanyika miaka mitano baadaye, Katibu Mkuu wa CCM wa wakati huo, Bashiru Ally, alipendekeza ni jambo la kipuuzi kwa chama hicho kutotumia madaraka ya uongozi kwa manufaa yake na akataja hatima ya vyama nchini Kenya na Zambia vilivyopoteza madaraka baada ya ujio wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa.
"Ukishindwa kutumia faida hiyo, utakuwa kama Kanu [Kenya African National Union]. Kanu iliposhindwa kutumia faida hiyo haikurudi tena madarakani. Au Unip ya Zambia [United National Independence Party]. Unachukua serikali. , halafu utumie serikali kubaki madarakani," Bw Ally alisema.
Nchini Tanzania, uidhinishaji CCM umuhakikishia ushindi mgombea wakati mwingine bila hata kushindana.
Katika uchaguzi mkuu wa 2020, wagombea wengi wa upinzani kugombea viti vya ubunge walienguliwa kwa kile walichoamini kuwa ni mashaka, hivyo kuwatengenezea njia wagombea 18 wa CCM kushinda bila kupingwa.
Ajabu yetu katika mchakato wa uchaguzi wa Kenya ilianza muda mrefu kabla ya siku ya kupiga kura. Tulijiuliza, kwa mfano, ilikuwaje kwa wagombea wa upinzani kuchukua fomu zao za kujiandikisha, kuzirudisha kwa tume ya uchaguzi na mara nyingi, wakaidhinishwa bila shida?
Nchini Tanzania, wagombea wengi wangekuta ofisi za uchaguzi, kwa kutiliwa shaka, zimefungwa kabla ya kupata nafasi ya kuwasilisha fomu zao.
Baadhi ya wagombea wangevunjiwa nyumba zao na "watu wasiojulikana" au wangevunjika miguu na mikono kabla ya kuanza safari ya kuelekea ofisi za tume ya taifa ya uchaguzi.
Ushindani kati ya wagombea wa Kenya kushindana katika mikutano mikubwa pia lilikuwa jambo la kustaajabisha.
Miaka minne kabla ya uchaguzi wetu wa 2020, Rais wa wakati huo John Magufuli alipiga marufuku mikutano ya upinzani.
Upinzani uliporuhusiwa kufanya mikutano hiyo wiki chache tu kabla ya uchaguzi, mara nyingi mikutano hiyo ilivurugwa na maafisa wa usalama ambao waliwatisha na kuwakamata wanaharakati na viongozi.
Katika mkutano mmoja kifaa cha kulipuzi kilirushwa, tena na "watu wasiojulikana", katikati ya mkusanyiko.
Tofauti nyingine ya aibu ilikuwa katika matumizi ya teknolojia. Nchini Kenya, raia yeyote aliye na muunganisho wa intaneti aliweza kupakua hati za uchaguzi katika muda halisi ili kujionea matokeo.
Hapa nchini Tanzania, uchaguzi wa kidijitali ulikatishwa tamaa kwa nguvu: katika uchaguzi uliopita, kukatika kwa mtandao kulimaanisha kuwa kutuma ujumbe mfupi wa simu kumezuiwa, kuingia kwenye mitandao ya kijamii kulikua haiwezekani bila kutumia VPN na hata kupiga simu za kawaida ilikuwa ngumu.
Mgombea aliyeshindwa hana haki ya kupinga matokeo mahakamani, kama Bw Odinga alivyofanya, achilia mbali umma kufuatilia kesi moja kwa moja kwenye runinga.
Hapa, katiba yetu inasema kwamba uamuzi wa tume ya uchaguzi ni wa mwisho hata mahakama zetu za juu haziwezi kuubatilisha.
Tulitatizika kufikiria ikiwa mkuu wa tume yetu aliyeteuliwa na rais, ambaye pia ni kiongozi wa chama tawala kuwa na ujasiri kama mwenzake wa Kenya, Wafula Chebukati, kwa kutangaza hesabu halisi ya kura, hata kama ilikwenda kinyume na CCM na mgombea wake.
Watanzania tunapenda kujivunia kuwa taifa lenye amani na umoja. Pia mara nyingi tunajisifu kuhusu jinsi, licha ya kuwa na zaidi ya makabila 100 tofauti, hii haifafanui mifumo ya upigaji kura, tofauti na Kenya.
Hayati Magufuli alipotembelea Kenya kwa mara ya kwanza kama rais, mwaka wa 2016, alidhihirisha hili waziwazi, akisema: "Ikiwa Kenya inaweza kuondokana na ukabila, itakuwa nchi bora zaidi."
Lakini katika uchaguzi wa hivi karibuni nchini Kenya, ukabila haukuwa muhimu kwani Bw Ruto aliweka uchumi kuwa kiini cha kampeni yake.
Kwa hiyo wakati Watanzania wakiangalia kiwango cha uwazi na jinsi Kenya ilivyopevuka katika mfumo wa demokrasia, wengi wanajiuliza iwapo kutokuwepo kwa ukabila ni sababu tosha ya kukubali mfumo mbovu wa uchaguzi.
Kwa hakika hatupaswi kuichukulia kuwa amani tuliyo nayo kirahisi, lakini swali la msingi ni: Je, tunahitaji kuafikiana kuhusu uchaguzi huru na wa haki? Hatuwezi kuwa na zote mbili? Je, tunahitaji kubadilishana?
Jambo lililo wazi ni kwamba uchaguzi wa Kenya umethibitisha matakwa ya Watanzania wengi ya kuwa na sheria mama mpya, au katiba.
Hata sisi ambao tulikuwa hatujaamua kabisa suala hilo sasa tunatambua jinsi katiba mpya inaweza kuwa muhimu katika kujenga na kuimarisha taasisi muhimu kama vile tume ya uchaguzi na mahakama ambazo zinatakiwa kufanya kazi bila woga au upendeleo.
Rais Samia Suluhu Hassan ambaye aliingia madarakani kufuatia kifo cha Magufuli mwaka wa 2021 ameahidi kushughulikia madai ya upinzani kwamba katiba mpya iandaliwe, lakini hakuna dalili ya lini hilo litafanyika.
Wala hakuna dalili yoyote kwamba CCM iko tayari kulegeza kamba madarakani kabla ya uchaguzi wa 2025.