Muuza sumu anayehusishwa na vifo vya watu 130 waliojiua Uingereza akabiliwa na BBC

Na Angus Crawford na Tony Smith

BBC News

Mwanamume mmoja wa Ukraine anayeuza sumu inayodhaniwa kuhusishwa na vifo vya watu 130 nchini Uingereza ametambuliwa na BBC.

Leonid Zakutenko alitangaza huduma zake kwenye tovuti inayohimiza watu kujiua na alimwambia mwandishi wa habari za uchunguzi kwamba yeye hutuma vifurushi vitano kwa wiki nchini Uingereza.

Amekuwa akisambaza dawa sawa na raia wa Canada Kenneth Law, ambaye alikamatwa mwaka jana na sasa anakabiliwa na mashtaka 14 ya mauaji.

Bw Zakutenko alikanusha madai hayo alipokabiliwa na BBC na kuulizwa kuhusu biashara yake.

Alifuatiliwa hadi nyumbani kwake mjini Kyiv na kukanusha kuwa aliuza kemikali hiyo hatari, ambayo BBC imeamua kutoitaja jina.

Walakini, uchunguzi wetu uligundua kuwa amekuwa akisambaza sumu hiyo kwa miaka.

Kemikali hiyo inaweza kuuzwa nchini Uingereza kihalali, lakini kwa kampuni zinazoitumia kwa madhumuni halali pekee.

Wasambazaji lazima wasiuze kwa wateja isipokuwa wawe wamekagua kufahamu itatumika vipi.

Inaweza kuwa hatari ikiwa itamezwa hata kwa dozi ndogo.

'Kudharauliwa'

Zakutenko alitajwa kuwa "binadamu wa kudharauliwa na mbaya" na familia ya dada mapacha Linda na Sarah, waliokufa London mwaka jana baada ya raia huyo wa Ukraine kuwapa sumu.

Linda alipewa "ufikiaji rahisi wa 'jia ya kifo' kwa pauni chache" baada ya kujua kuhusu muuzaji kwenye jukwaa maarufu la kujitoa uhai , kulingana na dada yake Helen Kite.

Aliwaelezea dada zake, 54, kama "werevu, wenye kujali na kujieleza".

Ikiwa umeathiriwa na masuala katika taarifa hii, usaidizi unapatikana kupitia BBC Action Line

Bi Kite alisema kuwa kutochukua hatua kwa mamlaka kuzuia dada zake na wengine wengi kupata kemikali hiyo ni "aibu ya kitaifa".

Kemikali inayouzwa na Zakutenko inajadiliwa kwa uwazi kwenye jukwaa linalotumiwa na Linda, huku wanachama wakishauriana jinsi ya kununua na kisha kuitumia.

Kemikali hiyo inaweza kuhusishwa na vifo zaidi ya 130 vya Uingereza tangu 2019, kulingana na mwanasayansi Prof Amrita Ahluwalia, mtaalam wa dawa ya mishipa katika Chuo Kikuu cha Queen Mary cha London.

Alichambua damu na sampuli zingine za watu waliokufa, ambazo zilitumwa kwake kutoka kwa madaktari wa magonjwa na polisi kote Uingereza.

Kati ya vipimo 187 alipata 71% vilionyesha athari nyingi za kemikali hiyo, ikionyesha kuwa takriban watu 133 wanaweza kuwa wamekufa kutokana na kumeza sumu hiyo.

"Hatua inafaa kuchukuliwa," Prof Ahluwalia alisema.

"Kwa kile kinachotumika, lazima kuwe na uchunguzi kamili wa suala hili. Ni lazima kudhibitiwa ili matumizi yake yawe kwa malengo yaliyokusudiwa."

Mashtaka ya mauaji

Mpishi Kenneth Law alikamatwa nchini Canada Mei 2023 na sasa ameshtakiwa kwa makosa 14 ya mauaji na kusaidia kujiua. .

Anakisiwa kuwa aliuza kemikali hiyo zaidi ya mara 1,200 kwa wanunuzi katika nchi 40 duniani kote na anahusishwa na vifo visivyopungua 93 nchini Uingereza.

Uchunguzi wetu uligundua kuwa Zakutenko amekuwa akiuza kemikali hiyo tangu angalau Novemba 2020.

Pia hutoa dawa tatu tofauti na maagizo, zinazoeleza katika miongozo ya kujiua mtandaoni.

Hata kwa ufupi alitangaza huduma yake kwenye kongamano lile lile la watu waliojiua kama Bw Law.

Tangu wakati huo, watumiaji wamepitisha maelezo yake ya mawasiliano kupitia ujumbe wa moja kwa moja.

Tulimtafuta Zakutenko hadi kwenye gorofa ndogo katika eneo la mnara wa enzi ya Sovieti katika mji mkuu wa Ukraine, Kyiv.

Tulimkabili kwa maswali nje ya ofisi yake ya posta ambako alikuwa akituma vifurushi zaidi.

Tulimuuliza kwa nini alikuwa akituma kemikali yenye sumu kwa watu wanaotaka kukatisha maisha yao.

"Huo ni uwongo," alituambia, kabla ya kuweka mkono wake juu ya kamera yetu na kujaribu kuondoka.

Tunajua kwamba takriban kifurushi kimoja kilikuwa na kemikali hiyo kwa sababu tuliagiza siku hiyo na tukapokea nambari ya kufuatilia muda mfupi baada ya Zakuetenko kuondoka posta.

Alipoulizwa atakachosema kwa familia za wafu, alijibu: "Sielewi unachozungumzia".

Hatua thabiti

Mtoto wa David Parfett Tom, 22, alinunua kemikali hiyo kutoka kwa Kenneth Law, na akaitumia kukatisha maisha yake mnamo Oktoba 2021.

Bw Parfett sasa anafanya kampeni ya kuzima kongamano la watu waliojitoa mhanga na kukomesha wauzaji kama Zakutenko.

Mamlaka ya Uingereza imejua kuhusu kemikali na biashara ya mtandaoni tangu angalau Septemba 2020, walipotahadharishwa na daktari wa maiti aliyechunguza kifo cha Joe Nihill mwenye umri wa miaka 23.

Mchunguzi wa maiti aliwaandikia polisi, mchunguzi mkuu wa maiti na msambazaji kemikali akiwaonya kuhusu biashara hatari ya sumu hiyo.

Tangu wakati huo, wachunguzi wa maiti kote Uingereza wameandikia idara tofauti za serikali wakipendekeza hatua zichukuliwe kuhusu kemikali na jukwaa hilo la kujitoa uhai.

Bw Parfett alinunua shehena kutoka kwa Zakutenko mnamo Desemba 2023 kwa sababu alitaka kujaribu mfumo huo ili kuona ikiwa mamlaka ingezuia kifurushi hicho.

"Bado siamini kuwa hilo lilikuwa likifanyika leo, kwa kila kitu tunachojua sasa kuhusu idadi ya vifo," alisema Bw Parfett.

Ukaguzi kama huo wa ustawi wa wanunuzi wa Uingereza ulifanyika baada ya Kenneth Law kukamatwa nchini Kanada.

Shirika la Kitaifa la Uhalifu limethibitisha kuwa kuna visa vya watu - ambao walinunua dawa hiyo kutoka kwa Law - wanaokufa baada ya polisi kufanya ukaguzi .

"Kesi kama hizo hushughulikiwa na vikosi vya polisi kulingana na sera zao na miongozo ya kitaifa," msemaji alisema.

Bw Parfett na Bi Kite wote wanataka hatua madhubuti zichukuliwe dhidi ya jukwaa ambapo wapendwa wao Tom na Linda waligundua kuhusu kemikali hiyo.

Bi Kite alielezea tovuti hiyo kama "chukizo, usiozuiliwa na mamlaka, kwa walio hatarini zaidi na kusababisha taabu na mateso makubwa kwa wale walioachwa."

Serikali inasema Sheria mpya ya Usalama Mtandaoni, ambayo imekuwa sheria mwaka jana inapaswa kusaidia kuzuia ufikiaji wa aina hii ya jukwaa kama hilo.