Gereza la Evin: Simulizi ya mwanaume aliyebadili jinsia na kuwa mwanamke katika gereza la Iran

Gereza la Evin katika mji mkuu wa Iran, Tehran, linajulikana kwa ukatili, na ni nyumbani kwa maelfu ya wafungwa, wakiwemo wafungwa wengi wa kisiasa nchini humo. Wanaharakati wa haki za binadamu wanasema wamerikodi dhuluma za mara kwa mara huko.
Mwaka 2021, kikundi cha wadukuzi kilitoa video zilizochukuliwa katika kamera za uchunguzi za gereza, ambazo zinaonyesha unyanyasaji dhidi ya wafungwa na video kutoka katika wadi maalumu ya wafungwa waliobadili jinsia na wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.
Kwa mara ya kwanza, BBC imeweza kuthibitisha picha hizo kwa kuzungumza na mtu aliyeonekana kwenye video hizo. Helma ni mwanaume aliyebadili jinsia yake na kuwa mwanamke (huntha), ambaye alipelekwa mara kadhaa katika gereza la Evin.
Katika mahojiano na BBC, anatoa maelezo ya kukamatwa kwake, kufungwa gerezani na matukio yaliyonaswa katika kamera za gereza.
"Nilikuwa na umri wa miaka 19 nilipofungwa huko Evin kwa [kuvaa] hijabu vibaya na kuvaa nguo za kike. Nilikamatwa na kufungwa jela mara mbili, nimetumia zaidi ya mwaka mmoja wa maisha yangu gerezani," anasema Helma.
Helma aliweza kuthibitisha picha zilizovuja kutoka gereza la Evin, ambazo zinamuonyesha akiwa amesimama huku wafungwa wengine wakipigana.
Kanda hiyo pia inaonyesha walinzi wakiwaburuza na kuwapiga wafungwa. Helma anasema wafungwa pia hunyanyaswa kingono au kushambuliwa.
Pia nasema, alishuhudia huntha mwingine akijaribu kujitoa uhai akiwa gerezani, na anasema hata yeye mwenyewe alijaribu kujiua.
Jela bila ya kosa lolote

Mwaka 2019, gari la polisi wa maadili - kitengo kinachohusika na kusimamia sheria za jinsi wanawake wanavovaa chini ya sheria za Iran - lilisimama mbele ya Helma na kumkamata huko Tehran.
"Niliwaambia mimi ni huntha na nikawaonyesha kibali changu cha matibabu, ambacho kiliniruhusu kuvaa nguo za kike hadharani, lakini hawakujali. Waliniambia nitie saini dhamana, wakiahidi nitaachiliwa - lakini hilo halikutokea. Badala yake, waliniweka gerezani kwa zaidi ya siku 30."
Vitendo vya mapenzi ya jinsia moja nchini Iran vinaadhibiwa kwa kifo, lakini wanazuoni wa huko wanakubali wazo kwamba mtu anaweza kunasa katika mwili wa jinsia isiyofaa.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Helma anasema afisa mwanamke wa polisi wa maadili alimtaka aandike kuwa amelipwa kuvaa hivi au anafanya kazi mitaani (kama kahaba), ili aachiliwe.
Helma anasema: "Ilikuwa mara yangu ya kwanza kukumbana na haya, na nilifikiri ikiwa nitawasikiliza, wangeniacha niende."
Helma alipelekwa katika kituo cha polisi wa maadili katika Mtaa wa Vozara huko Tehran, ambako alilala usiku mmoja.
Hiki ndicho kituo ambacho Mahsa Amini, mwenye umri wa miaka 22, alipelekwa Septemba 2022 kwa madai ya kutovaa hijabu ipasavyo na baadaye kufariki akiwa kizuizini. Kifo chake kilizusha maandamano nchini Iran.
Helma anasema akiwa gerezani alitukanwa na kudhalilishwa, na wakati wa upekuzi wa mwili wake alinyanyaswa kingono na kushikwa shikwa.
"Nililia kwenye seli hiyo hadi asubuhi. Baadhi ya wanawake mahuntha niliowajua walikuwa wamenadika majina yao ukutani."
Siku iliyofuata, alipelekwa mahakamani.
"Jaji ni mwanazuoni, na alikuwa akiniapiza tu. Alisema: 'Kwa nini umevaa nguo hizi? Kwa nini umekuzisha nywele zako? Hati zako zinasema wewe ni wa mwanaume!' Nilimwambia: 'Mimi ni huntha, na daktari amenipa ruhusa ya kuvaa nguo hizi, ili niweze kuuelewa utambulisho wangu wa kijinsia.'
Helma anasema hakimu alimhukumu kifungo cha miaka miwili gerezani kulingana na ushahidi ambalo polisi wa maadili walioutoa, na dhamana ya toman milioni 200 (kama dola 15,000 wakati huo).
Hakuwa na usaidizi wa kifamilia au marafiki - kwani hakutaka familia yake ijue kuwa amekamatwa kwa kuvaa nguo za kike - hivyo hakuweza kupata pesa hizo za dhamana.
Anasema, alipelekwa katika gereza la Evin, ambako alikaa kwa zaidi ya siku 30 kabla ya kuachiliwa kwa masharti, kwani hakuwahi kukamatwa kwa kosa lolote hapo awali na hakukuwa na ushahidi wa moja ya mashtaka.
Baada ya kuachiliwa, alikamatwa tena mara mbili - mara moja akiwa mtaani na mara moja katika nyumba aliyokuwa amepanga na rafiki yake. Kwa kuwa hakuweza kumudu kulipa pesa za dhamana, alikaa gerezani huko Evin muda mwingi zaidi.
"Si mtaani wala nyumbani ambako ni salama. Nilipanga nyumba na rafiki ambaye anajihusisha na mapenzi ya jinsia moja, na majirani walituripoti kwa polisi."
Mashitaka dhidi yake
BBC imechunguza na kuthibitisha ushahidi kuhusiana na kukamatwa kwake na kufungwa huko Evin kupitia hati rasmi ambazo Helma alizitoa na hati zingine zilizovuja kutoka mahakama ya Iran.
Baadhi ya mashtaka aliyokabiliwa nayo ni pamoja na "kuukosea adabu umma kwa kuvaa nguo za wanawake, kujipodoa kupita kiasi, na mavazi ya kubana au yanayoonyesha" na "kuratibu rushwa na ukahaba na kujipatia kipato kwa njia zisizo halali."
Hati moja inaonyesha mahakama ilimwachilia huru kutokana na shtaka la kujipatia mapato kinyume cha sheria.
Maisha ya gerezani

Agosti 2021, kikundi cha wadukuzi kiitwacho Edalat-e Ali kilitoa video zilizochukuliwa katika kamera za uchunguzi za gereza la Evin.
Anasema: "Hii ilikuwa katika wodi namba 240. Tuliruhusiwa kwenda nje kupata hewa safi mara moja kwa wiki kwa dakika 10. Kulikuwa na kamera hata ndani ya vyoo. Mara kwa mara tulitukanwa na kukejeliwa na maofisa wa magereza. Wakati tukiingia gerezani na kwenda mahakamani, maofisa wa kike walikataa kutupekua, hivyo maofisa wanaume walitutaka tuvue nguo mbele yao na kufanya upekuzi."
Anasema wafungwa katika wadi hii mara kwa mara hushikwa shikwa isivyofaa na kunyanyaswa kijinsia na maafisa wa magereza na hata na madaktari ambao walitupa dawa za usingizi na dawa za kupambana na sonona.

Katika video za zilizovuja, jaribio la huntha la kujitoa uhai katika bafu la gereza linaonekana. Helma anasema: "Alikuwa amekamatwa mara 13. Nilijaribu kumzuia, lakini hata hivyo alijaribu kujiuwa. Baada ya jaribio hilo, alikuwa katika hali ya kukosa fahamu kwa muda."
Helma anasema kutokana na shinikizo la kisaikolojia gerezani, alijaribu pia kujiua mara kadhaa. Akionyesha makovu kwenye mikono yake mwenyewe.
Juu ya makovu, amejichora tatuu ya sura yenye tabasamu: "Nimechora tatuu hii juu ya makovu ili kusahau kwamba nilifanya hivi kwenye mwili wangu."
Anasema wafanyakazi wa gereza hawakuzuii ukijaribu kujiua, na wakati mmoja msafishaji anayefanya kazi katika hospitali ya gereza hata alimpa dawa ili ajiuwe.
Sheria za nchini Iran
Mapenzi ya jinsia moja, yanakataliwa nchini Iran, na uhusiano wa mapenzi ya jinsia moja unaadhibiwa kwa kifo.
Katika miaka ya 1960, kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatollah Ali Khomeini (ambaye baadaye alikuwa kiongozi wa Iran baada ya mapinduzi), alitoa fatwa na kutangaza kuwa mabadiliko ya kijinsia yanaruhusiwa kidini.
Kulingana na uamuzi huu, upasuaji wa kubadili jinsia na mabadiliko ya kisheria ya kubadili jinsia yanaruhusiwa kisheria katika Jamhuri ya Kiislamu.
Lakini katika miaka ya hivi karibuni, wanaharakati wa LGBT (wasagaji, wapenzi wa jinsia zote mbili, waliobadili jinsia), wameripoti kwamba serikali ya Iran imejaribu kuwashinikiza au kuwashawishi huntha kufanyiwa operesheni, kama ilivyoripotiwa hapo awali na BBC News Persian.
Upasuaji huu wa kubadili mwonekano, ni mgumu sana na wa gharama kubwa, na wakati mwingine, umesababisha matatizo makubwa ya afya kwa wale wanaofanyiwa.
Wale ambao hawafanyi upasuaji huo ambao lengo ni kubadili mwonekano wa mtu ili kuendana na jinsia anayoitaka, wanakabiliwa na ubaguzi na kufunguliwa mashtaka.
Ushahidi kutoka mahakamani unaonyesha kuwa hata idara ya mahakama imechanganyikiwa kuhusu jinsi ya kushughulikia kesi hizo.
Kukataliwa kwa familia

Wakati huo, familia ya Helma haikujua kwamba alikuwa gerezani. Alipokuwa akizungumza kwa simu na mama yake, Helma alikuwa akifupisha mazungumzo ili kumzuia asisikie ujumbe unaosema, simu hiyo inatoka gerezani.
Lakini hatimaye, watu wa ukoo wa Helma walipata habari kuhusu kufungwa kwake na kutishia kumuua. Anasema, kutokana na vitisho hivyo, alimwomba afisa wa gereza hilo kutoruhusu mwanafamilia yeyote kumtembelea.
Katika miaka ya hivi karibuni, huntha wengi na wapenzi wa jinsia moja nchini Iran wameuawa na wanaume wa familia zao.
Katika baadhi ya matukio, hata wale ambao walihama katika nyumba zao na miji wameuawa - na sababu inayotajwa mara nyingi ni kutunza sifa ya familia.
Watu hao mara nyingi hukosa usaidizi wa kifamilia. Helma anasema: "Nchini Iran, wakati unapoanza kuuelewa utambulisho wako wa kijinsia na kujielewa mwenyewe, familia yako inakataa kukukubali, na unalazimika kuwaacha na kuingia katika miji mikubwa zaidi - ambapo matatizo makubwa zaidi hutokea."
Helma aliamua kuhamia Uturuki. Hata hivyo, hakupata usalama huko. Alivunjwa taya katika shambulio linaloshukiwa kuwa la kibaguzi, hati za korti alizotoa zinaonyesha.
Ameomba hifadhi kupitia Umoja wa Mataifa. Amekuwa akingoja kwa miaka mitatu sasa kesi yake ipitiwe upya.
Licha ya changamoto hizi, bado anashikilia ndoto ya: "Kuhamia nchi ambayo ninaweza kusoma, kufanya kazi, na kuishi maisha ya kawaida - kama watu wengine kwenye sayari hii."
BBC News Persian imepigwa marufuku nchini Iran na serikali. Serikali ya Iran mara kwa mara inakanusha madai ya ukiukaji wa haki za binadamu, ikisema hali ndani ya gereza la Evin inakidhi viwango vyote vinavyohitajika na wafungwa hawadhulumiwi.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












