Mzozo wa DRC: Waasi wa M23 waingia mjini Bukavu

x

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Ambia Hirsi
    • Nafasi, BBC Nairobi
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Waasi wa M23 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wameingia Bukavu, mji wa pili kwa ukubwa katika eneo hilo la mashariki.

Corneille Nangaa, kiongozi wa Muungano unaojumuisha waasi wa M23, ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa waasi hao waliingia katika mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini Ijumaa jioni na wataendelea na harakati zao Jumamosi ya leo.

Waasi wa M23 wa ambao wanaungwa mkono na Rwanda wanaripotiwa kuuteka uwanja wa ndege wa kimkakati wa Kavumba karibu na Bukavu, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini.

Uwanja huo wa ndege upo takribani kilomita 20 kutoka mji wa Bukavu ambapo wakaazi wameileza BBC kuwa kuna hali ya taharuki.

Msemaji wa muungano wa waasi amesema kwenye chapisho kupitia X, waasi wanadhibiti uwanja wa ndege na maeneo jirani.

Hatua hiyo ya waasi inakuja licha ya wito wa kimataifa wa kusitisha mapigano na kuanzishwa tena kwa mazungumzo ya amani.

Maelfu ya watu wamelazimika kuyahama makazi yao katika wiki za hivi karibuni kutokana na hatua hiyo ya waasi.

Akizungumza na BBC Makamu Gavana wa Kivu Kusini Jean Elakano hata hivyo ameiambia BBC kuwa mapigano makali yanaendelea lakini hakuthibitisha wala kukanusha ripoti kwamba waasi hao wameuteka uwanja wa ndege wa Kavumba karibu na mji wa Bukavu.

''Mapambano makali yanaendelea, tunavamiwa kutoka kila upande ardhini na ziwani. M23 pamoja na jeshi la Rwanda wanatushambulia. Tunaomba Umoja wa Mataifa kuingilia kati.

Hali ikoje Bukavu?

Watu waliokimbia makazi yao kutokana na mapigano kati ya waasi wa M23 na Wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Watu waliokimbia makazi yao kutokana na mapigano kati ya waasi wa M23 na Wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Tangu mapema asubuhi ya Ijumaa Februari 14, milio ya risasi na milipuko na ya mabomu ilisikika katika kijiji cha Kaatana na muda mfupi baadae moto mkubwa wa silaha umesikika katika kijiji cha Katana katika eneo la Walungu.

Baadhi ya wakaazi walijifungia majumbani mwao, wengine walikimbilia vijiji vya jirani. Muda mfupi baadaye, M23 waliripotiwa kuuteka uwanja wa ndege wa Kavumu na inaripotiwa wanasonga mbele kuelekea Bukavu ambao ni mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini.

Shughuli katika mji huo zinaendelea kama kawaida, wakaazi wanafuatilia hali ilivyo kwenye mitandao ya kijamii kutoka vijiji jirani na Bukavu vilivyoangukia mikononi mwa M23.

Mmoja wa wa wakaazi wa Bukavu Innocent Saidi, anasema wenyeji wa wako tayari kuwakaribisha waasi kwa amani na kutoa wito kwa wapiganaji hao kuheshimu haki za binadamu.

x

Chanzo cha picha, Reuters

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Rwanda imekuwa ikikabiliwa na shinikizo la kuwaondoa wanajeshi wake mashariki mwa Congo na kusitisha harakati za kuisaidia M23.

Hata hivyo Rais Paul Kagame wa Rwanda anasema kipaumbele chake ni usalama. Kagame anadai kuwa nchi yake inakabiliwa na tishio la mashambulizi kutoka kwa waasi wa Kihutu nchini Congo.

Kagame pia amepuuzilia mbali tishio lolote la kuweiwekea vikwazo nchi yake.

Serikali ya Kinshasa inasema Kigali inanyakua kipande kikubwa cha eneo lenye utajiri wa madini kinyume cha sheria.

Wakati huo huo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi limesema vita hivyo vimewaacha takriban watu 350,000 bila makazi.

Waasi wa M23 waliuteka mji mkubwa zaidi wa mashariki mwa Congo wa Goma mwezi uliopita na wamekuwa wakielekea kusini.

Msemaji wa UNHCR, Eujin Byun aliwaambia waandishi wa habari mjini Geneva kwa njia ya video, wakimbizi wa ndani 350,000 hawana mahali pa kuishi kwani kambi zao za muda zimeharibiwa au kuna mabomu ambayo hayakulipuka na yanafanya kutokuwa salama kwao kurudi nyumbani.

Takriban 70% ya kambi za Goma zimeharibiwa, na zingine huko Minova zimeharibiwa, kulingana na UNHCR.

Shirika hilo pia limeiripoti kuongezeka kwa uhalifu na kusema hatari ya magonjwa inazidi kuongezeka, huku shirika hilo na mashirika mengine yakihangaika kutoa misaada wakati wa mapigano.

Ramani