Wakunga walioacha kuwaua wasichana wachanga na kuanza kuwaokoa

- Author, Amitabh Parashar
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Mkunga Siro Devi anamkumbatia Monica Thatte, huku akilia. Monica, yuko katika miaka yake ya mwisho ya 20, amerejea mahali alipozaliwa huko India ambako Siro amezalisha mamia ya watoto.
Lakini huu sio muungano wa kawaida. Kuna historia chungu nyuma ya machozi ya Siro. Muda mfupi kabla ya Monica kuzaliwa, Siro na wakunga kadhaa kama yeye walishinikizwa mara kwa mara kuwaua wasichana wachanga.
Ushahidi unaonyesha, Monica ni mmoja ya waliokolewa.
Nimekuwa nikifuatilia maisha ya Siro kwa miaka 30, tangu nilipokwenda kumhoji yeye na wakunga wengine wanne huko vijijini katika jimbo la Bihar nchini India mwaka 1996.
Walitajwa na shirika lisilo la kiserikali kuwa walihusika na mauaji ya watoto wachanga katika wilaya ya Katihar, kwa shinikizo kutoka kwa wazazi wa watoto hao, walikuwa wakiwaua kwa kuwalisha kemikali au kuwakunja shingo zao.
Hakiya Devi, mkubwa wa wakunga niliowahoji, aliniambia wakati huo alikuwa ameua watoto 12 au 13. Mkunga mwingine, Dharmi Devi, alikiri kuua takribani watoto 15-20.
Haiwezekani kufahamu idadi kamili ya watoto ambao wamewaua, kutokana na jinsi taarifa zilivyokusanywa. Wakunga hao wamo katika ripoti iliyochapishwa mwaka 1995 na NGO, katika mahojiano nao na wakunga wengine 30.
Ikiwa makadirio ya ripoti ni sahihi, zaidi ya watoto wa kike 1,000 walikuwa wakiuawa kila mwaka katika wilaya moja, na wakunga 35 pekee. Kulingana na ripoti hiyo, Bihar wakati huo ilikuwa na wakunga zaidi ya nusu milioni. Na mauaji ya watoto wachanga hayakuwa tu yakifanyika Bihar pekee.
Maagizo ya kuuwa wasichana

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kukataa maagizo, Hakiya anasema, kamwe halikuwa chaguo la mkunga.
"Familia hufunga chumba na kusimama nyuma yetu," anasema Hakiya Devi. "Wangesema: 'Tayari tuna mabinti wanne-watano. Hii itafuta utajiri wetu. Tukishatoa mahari kwa wasichana wetu, tutakufa kwa njaa. Sasa, msichana mwingine amezaliwa. Muue.'
“Tungelalamika kwa nani? Tuliogopa. Ikiwa tungeenda polisi, tungeingia kwenye shida. Ikiwa tungezungumza, watu wangetutisha."
Kazi ya ukunga katika maeneo ya mashambani nchini India hutoka katika mila. Wakunga niliowahoji walikuwa wa tabaka la chini katika tabaka la India. Ukunga ilikuwa ni taaluma waliorithi kutoka kwa mama na bibi zao. Waliishi katika ulimwengu ambao kukataa maagizo ya familia zenye nguvu, za tabaka la juu haikuwa jambo rahisi.
Mkunga angeahidiwa nguo, gunia la nafaka au kiasi kidogo cha pesa kwa kumuua mtoto mchanga. Wakati mwingine hata hiyo hakulipwa. Kuzaliwa kwa mvulana kungewafanya kupata hadi rupia 1,000. Kuzaliwa kwa msichana hupata nusu yake.
Sababu ya tatizo hili ilitokana na desturi ya India ya mwanamke kutoa mahari, walieleza. Ingawa desturi hiyo iliharamishwa mwaka 1961, bado iliendelea kuwa na nguvu katika miaka ya 90 - na kwa kweli inaendelea hadi leo.
Mahari inaweza kuwa chochote - pesa, vito, vyombo. Lakini kwa familia nyingi, tajiri au maskini, ukubwa wa harusi ni muhimu. Na hii ndiyo, kwa wengi, hufanya kuzaliwa kwa mwanaume kuwa sherehe na kuzaliwa kwa binti ionekane ni mzigo wa kifedha.
Siro Devi, mkunga pekee kati ya wale niliowahoji ambaye bado yuko hai, alinielezea wazi tofauti hii.
Upendeleo wa wavulana unaonekana hata katika data ya kitaifa ya India. Sensa ya mwaka 2011, ilirekodi uwiano wa wanawake 943 kwa kila wanaume 1,000. Katika miaka ya 1990 - katika sensa ya 1991, uwiano ulikuwa 927/1,000.
Mbinu za kuwaokoa

Nilipomaliza kurekodi ushuhuda wa wakunga mwaka 1996, mabadiliko madogo ya kimyakimya yalikuwa yameanza. Wakunga ambao waliwahi kutekeleza maagizo haya walianza kupinga maagizo.
Mabadiliko haya yalichochewa na Anila Kumari, mfanyakazi wa kijamii ambaye alisaidia wanawake katika vijiji vinavyozunguka Katihar, na alijitolea kushughulikia sababu kuu za mauaji haya.
Njia ya Anila ilikuwa rahisi. Alikuwa akiwauliza wakunga, Je! Mnaweza kumfanyia hivi binti yenu?
Na pia wakunga walipata usaidizi wa kifedha kupitia vikundi vya kijamii na polepole mzunguko wa mauaji ukaingiliwa kati.
Siro, akizungumza nami mwaka 2007, alieleza mabadiliko hayo.
“Kwa sasa yeyote anayeniomba niue, ninamwambia: ‘Sikiliza, nipe mtoto, nitampeleka kwa Anila Madam.”
Wakunga hao waliwaokoa wasichana wasiopungua watano kutoka katika familia zilizotaka wauawe au zilizo watelekeza.
Mtoto mmoja alikufa, lakini Anila alipanga kuwapeleka wanne katika mji mkuu wa Bihar, Patna, kwa NGO ambayo ilipanga kuasiliwa kwao.
Hadithi inaweza kuishia hapo. Lakini nilitaka kujua nini kimetokea kwa wasichana hao walioasiliwa, na maisha yamewapeleka wapi.
Kumtafuta Monica

Nikifanya kazi na timu ya BBC World Service, niliwasiliana na mwanamke anayeitwa Medha Shekar, huko nyuma katika miaka ya 90, alikuwa akitafiti mauaji ya watoto wachanga huko Bihar, muda ambao watoto waliookolewa na Anila na wakunga walipoanza kuwasili kwenye NGO yake.
Cha kufurahisha, Medha alikuwa bado ana mawasiliano na msichana ambaye, anaamini, alikuwa mmoja wa watoto hawa waliookolewa.
Anila aliniambia aliwapa wasichana wote waliookolewa na wakunga kiambishi awali “Kosi.” Medha anakumbuka kuwa Monica alipewa jina na kiambishi hiki cha "Kosi" kabla ya kuasiliwa kwake.
Shirika la kuasili watoto halikuturuhusu kutazama rekodi za Monica, kwa hivyo hatuwezi kuwa na uhakika. Lakini asili ya Monica anatokea Patna, tarehe yake ya kuzaliwa na kiambishi awali "Kosi" vyote vinaelekeza kwenye hitimisho moja: Monica, huenda, ni mmoja wa watoto watano waliookolewa na Anila na wakunga.
Nilipokwenda kukutana naye nyumbani kwa wazazi wake umbali wa kilomita 2,000 (maili 1,242) huko Pune, alisema alijiona mwenye bahati kwa kulelewa na familia yenye upendo.

Monica alijua kwamba alikuwa ameasiliwa kutoka Bihar. Lakini tulimpa maelezo zaidi kuhusu hali ya kuasiliwa kwake. Mapema mwaka huu, Monica alisafiri hadi Bihar kukutana na Anila na Siro.
Anila alitokwa na machozi ya furaha alipokutana na Monica. Na Siro alilia sana huku akimshika Monica nywele zake.
"Nilikupeleka [kwenye kituo cha watoto yatima] kuokoa maisha yako. Nafsi yangu iko katika amani sasa," alimwambia.
Tatizo bado lipo

Jambo ambalo bado lipo ni chuki ambayo wengine wanayo dhidi ya watoto wa kike.
Ripoti za mauaji ya watoto wachanga kwa sasa ni nadra, lakini utoaji mimba kwa sababu ya jinsia bado ni jambo la kawaida, licha ya kuwa ni kinyume cha sheria tangu 1994.
Mtu akisikiliza nyimbo za kitamaduni zinazoimbwa wakati wa kujifungua, zinazojulikana kama Sohar, katika sehemu za kaskazini mwa India, furaha hutokea tu anapozaliwa mtoto wa kiume.
Tulipokuwa tukirekodi makala hii, watoto wawili wa kike waligunduliwa wakiwa wametelekezwa huko Katihar - mmoja vichakani, mwingine kando ya barabara, akiwa na umri wa saa chache tu. Mmoja alikufa baadaye. Mwingine alichukuliwa kwa ajili ya kuasili.
Kabla ya Monica kuondoka Bihar, alimtembelea mtoto huyu katika Kituo Maalum cha Kuasili huko Katihar.

Mtoto huyo sasa amechukuliwa na wanandoa katika jimbo la kaskazini-mashariki la Assam. Wamempa jina Edha, maana yake furaha.
Kila baada ya wiki chache, baba yake mlezi Gaurav, afisa katika jeshi la anga la India hunitumia video ya maisha ya Edha. Wakati fulani nami huzituma video hizo kwa Monica.
Nikiangalia nyuma, miaka 30 kwenye hadithi hii ya kukabiliana na uhalisia unaoumiza. Yaliyopita hayawezi kutenduliwa, lakini yanaweza kubadilishwa.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah












