'Nililipa £30k kumlinda mtoto wangu dhidi ya baba yake mlawiti'

Baba ya binti yake alipopelekwa gerezani kwa unyanyasaji wa kingono kwa watoto, Bethan alishtuka kugundua bado angeweza kuruhusiwa kuwa na mtoto wao baada ya kuachiliwa. Ilikuwa hatari ambayo hakuwa tayari kukabiliana nayo.
Nje ya mahakama ya Cardiff, mwanamke mchanga aliyevalia nadhifu ameketi akisubiri kwa wasiwasi. Bethan hajawahi kuingia katika mahakama ya familia hapo awali, lakini yuko hapa kujaribu kumlinda mtoto wake - ambaye baba yake amehukumiwa kwa makosa ya kulawiti watoto na kwa sasa yuko jela.
Alipohukumiwa, miezi kadhaa iliyopita, alipewa amri ya kumpiga marufuku kuwasiliana na watoto siku zijazo - lakini marufuku hiyo haimzuii kutafuta mawasiliano na mtoto wake mwenyewe.
Yeye na Bethan walifunga ndoa binti yao alipozaliwa na hivyo ana haki za mzazi, akiruhusiwa angalau kuangazia kuhusu afya ya mtoto wake, elimu na mpangilio wa maisha.
Bethan "amefadhaika kabisa" kuhusu kitakachotokea mara tu atakapoachiliwa kutoka gerezani. Anahofia huenda akamtoa shuleni binti yao siku moja bila yeye kujua, na njia pekee ya kumrejesha mtoto itakuwa kupitia mahakama ya familia. Ingawa mume wake wa zamani ana mtoto wao, angeweza kumfanyia kile alichowafanyia watoto wengine aliowatesa.
"Hautawahi kujisamehe," anasema.
Kwa kuungwa mkono na wazazi wake, Bethan amechukua hatua ya kipekee ya kuiomba mahakama iondoe haki za mzazi za aliyekuwa mume wake na kupiga marufuku mawasiliano yote - moja kwa moja, isiyo ya moja kwa moja na kupitia mitandao ya kijamii - hadi binti yao atakapofikisha umri wa miaka 18.
Licha ya ukali wa uhalifu wa mpenzi wake wa zamani, Bethan ameshauriwa kuwa mchakato huu unaweza kuwa mgumu. Anamtaja kama "mdanganyifu" na anahofia kuwa ataweza kuishawishi mahakama kuhusu majuto yake.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hana haki ya kupata msaada wa kisheria, na hata kabla ya kusikilizwa kwa mara ya kwanza, gharama za wakili wake tayari zinaongezeka.
Kesi ya Bethan itasikilizwa katika mahakama ya familia, ambapo mabishano kati ya wazazi - mara nyingi yanahusisha watoto walio katika mazingira magumu - yanashughulikiwa. Hadi hivi majuzi, kesi zimekuwa zikisikilizwa kwa
Lakini tangu Januari, waandishi wa habari walioidhinishwa wameruhusiwa ndani ya mahakama za familia huko Leeds, Carlisle na Cardiff - kuruhusu uchunguzi wa karibu wa hatua za serikali za mitaa na mahakama, kwa kuzingatia sheria kali za kutokujulikana.
BBC News imekuwa ikifuatilia kesi ya Bethan kwa muda wa miezi sita iliyopita.
Mahakamani, Bethan anakaa nyuma ili asionekane. Baba wa mtoto wake - ambaye hana wakili - anaonekana kupitia kiunganishi cha video kutoka gerezani, kinachoonyeshwa kwenye skrini kubwa. Anaonekana mdogo, ameketi nyuma ya meza ndefu, na karatasi zimeenea mbele yake.
Mfanyikazi wa kijamii kutoka Cafcass Cymru, huduma ya ushauri ya mahakama ya watoto na familia ya Wales, pia yuko hapo.
Mpenzi wa zamani wa Bethan anaiambia mahakama kwamba anakubali kuwa yuko gerezani kwa makosa ya "hali mbaya sana" na anasema "anataka kuwepo kwa ajili ya mtoto wake", ikiwa atataka kuwa na uhusiano naye. Amekuwa akimwandikia barua kila wiki, ambazo hawezi kutuma kwa sasa.
Baadaye, anatoa rufaa inayoonekana kuwa ya moyoni - yeye ni baba "ambaye anapenda mtoto wake na hilo halikuwa na mwisho" anasema - sauti yake inavunjika vunjika anapoiambia mahakama kuwa "anatamani kuwa huko" kwa binti yake.
Kwa Bethan "haiwezi kuvumilika" kusikiliza, na "inauma sana" kujaribu kupatanisha mtu huyu na "matishio ambayo aliwaweka watoto".

Mtoto wa Bethan ni mmoja wa zaidi ya 80,000 walionaswa katika kesi za kibinafsi za sheria ya familia.
Mnamo 2022, kesi ya wastani ya sheria ya familia ya kibinafsi nchini Uingereza na Wales ilichukua karibu miezi 10, au karibu wiki 45, kulingana na Jumuiya ya Wanasheria.
Lakini haki za mzazi "zipo moja kwa moja" kisheria na zinaweza tu kusimamiwa kupitia amri ya mahakama, aeleza Hannah Markham KC, mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria wa Familia.
"Hata kama mtu yuko gerezani kwa makosa makubwa sana ya kulawiti watoto, wanabaki na jukumu la mzazi," anasema - akielezea Bethan kama "shujaa" kwa kukabiliana na hili.

Katika wiki zijazo mfanyakazi wa kijamii hutumia muda na Bethan na binti yake, na kumtembelea baba gerezani.
Kesi inaendelea kwa haraka, na Bethan amerejea katika Kituo cha Haki cha Familia cha Cardiff miezi mitatu baadaye.
Ripoti ya mfanyakazi wa kijamii inamkosoa sana mume wa zamani wa Bethan. Anaonekana kuvunjika moyo na kusema "samahani hawezi kuwa baba anayestahili mtoto wake", kabla ya kuishukuru mahakama.
Anatumai kuwa anaweza kutathminiwa tena atakapoachiliwa na kuomba ripoti ya kila mwaka inayoelezea jinsi binti yake anaendelea.
Kwa Bethan, aina hii ya mawasiliano isiyo ya moja kwa moja anahisi kuwa haikubaliki. Kesi hiyo "imechukua" maisha yao yote, lakini ikilinganishwa na kesi nyingine nyingi za mahakama ya familia, inaendelea haraka - tarehe ya mwisho ya kusikilizwa ni chini ya wiki mbili.
Mahakamani, hakimu anatoa mukhtasari wa matokeo ya mfanyakazi wa kijamii. Bethan "amefarijika sana" wanaamua binti yake aishi naye kila wakati, wakati jukumu la mzazi mwenzi wake wa zamani "limezuiliwa kabisa".
Pamoja na uhalifu uliomfanya kuwa gerezani, hakimu huyo anasema mwanamume huyo pia amekiri kutazama nyenzo za unyanyasaji wa kijinsia za watoto zikiwa na kujamiiana na jamaa.
Yeye ni "hatari kubwa sana", hakimu anasema, na haruhusu ombi la baba la ripoti za kila mwaka. Amri ya kuzuia, ambayo itafanya iwe vigumu zaidi kwa mume wa zamani wa Bethan kuomba kubadilisha uamuzi wa hakimu mara tu atakapoachiliwa kutoka gerezani, inakubaliwa.
Atajulishwa ikiwa binti yake ni mgonjwa sana, au ikiwa wamehamia nchi tofauti - lakini sio huko waliko.
Kwa Bethan - ambaye ametumia saa nyingi kutafiti sheria za familia na ambaye amesoma akaunti nyingi kutoka kwa wazazi ambao hawapati uamuzi waliotarajia - ni "afueni kubwa".
"Nilishukuru sana," anasema.
Wazazi wa Bethan wamefurahi sana, pia.
"Kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitatu walimwachilia binti yangu kuweza kumlea mtoto wake kwa njia ya kawaida, yenye furaha, na yenye afya," mamake Bethan asema. "Hatuwezi kueleza jinsi imekuwa chungu sana."
Pamoja na athari za kihisia za kuleta kesi hiyo, pia imekuja kwa bei kubwa - inayogharimu zaidi ya pauni 30,000.
Familia hiyo inaamini kuwa wengine wanaweza kuepuka kesi za gharama kama hizo mahakamani ikiwa sheria itabadilishwa ili kusimamisha moja kwa moja haki za wazazi wanapohukumiwa kwa dhulma dhidi ya watoto, na kuzirejesha tu ikiwa mhalifu atawasilisha ombi kwa mahakama ya familia.
Simulizi hii inatumia jina la uwongo ili kulinda faragha ya Bethan.
Imetafsiriwa na Asha Juma na kuhaririwa na Seif












