Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mwanamume aliyehusika na jaribio la mapinduzi DRC ni nani?
Khadidiatou Cissé
BBC News
Jaribio la kuipindua serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika siku chache zilizopita limezidisha hali ya wasiwasi katika nchi hiyo ya katikati mwa Afrika.
Brig Jenerali, Sylvain Ekenge, msemaji wa jeshi la DR Congo alisema kuwa mnamo Mei 19 watu kadhaa waliokuwa na silaha walishambulia ofisi ya rais, na shambulio la pili lilifanyika karibu na nyumba ya Vital Kamerhe, mkuu wa zamani wa wafanyikazi na mshirika wa karibu wa sasa wa mkuu wa nchi.
Kufuatia mashambulizi hayo, watu 50 wakiwemo raia watatu wa Marekani wamekamatwa.
Wengi hapo awali waliamini kuwa jaribio hilo la mapinduzi lilitoka kwa kundi la wanajeshi wa Kongo wanaohusishwa na walinzi wa rais.
Hata hivyo, ilithibitishwa baadaye hatua hiyo ilichochewa na kiongozi wa upinzani Christian Malanga, mkosoaji wa muda mrefu wa Rais Félix Tshisekedi. Mnamo 2012, alikimbia uhamishoni na kupata uraia wa Marekani.
Jeshi lilithibitisha kuwa Malanga aliuawa kwa kupigwa risasi katika Ikulu ya Rais baada ya kukataa kukamatwa na vyombo vya usalama.
Mara ya mwisho alionekana akiwa hai Jumapili asubuhi kupitia matangazo ya moja kwa moja kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook, akiwa amesimama kando ya watu kadhaa waliokuwa na silaha nzito waliovalia sare za kijeshi.
‘Felix, uko nje. Tunakuja kupambana nawe’, alisema Malanga, akithibitisha nia yake ya kupindua utawala wa Rais Tshisekedi.
Akiwa amesimama karibu na mwanawe Marcel - ambaye pia amekamatwa na vikosi vya usalama - Malanga alihutubia watazamaji kwa lugha za Kifaransa, Kiingereza na Lingala, akisema kuwa wanajeshi 'wamechoka' na 'hawakuweza kuandamana pamoja' na Kamerhe na Tshisekedi.
Akiwa na umri wa miaka 41, Christian Malanga alijulikana kama sauti ya upinzani ya kisiasa kutoka nje Congo
Mzaliwa wa Kinshasa, familia ya Malanga iliondoka nchini alipokuwa mtoto na kukimbilia Swaziland na baadaye kuhamia Salt Lake City, Utah, mwaka wa 1998.
Baada ya kumaliza shule ya upili nchini Marekani, alianzisha biashara kadhaa ndogo ndogo pamoja na Shirika lisilo la faida la Africa Helpline Society, ambalo linasaidia elimu ya watoto katika bara hilo.
Mnamo 2006, alirudi DR Congo kwa utumishi wa kijeshi. Baadaye, alianzisha kampuni iitwayo Malanga Kongo, inayohusika na kazi za umma na miradi ya ununuzi.
Mnamo 2011, aliingia katika siasa akisimama kama mgombeaji katika uchaguzi wa ubunge lakini alikamatwa kabla ya upigaji kura kufanyika na kuzuiliwa kwa wiki kadhaa.
Inasemekana kuwa baada ya kuachiliwa Malanga alikataa ofa ya serikali ya kuwa rais wa vijana kitaifa na badala yake akachagua kufuata njia yake mwenyewe, kuanzisha chama chake cha siasa.
Malanga alirejea Marekani mwaka uliofuata na kuanzisha United Congolese Party (UCP), chama kidogo ambacho kililenga kuunganisha raia wa congo Kongo walioko nje ya nchi duniani kote. Pia alikuwa mwenyekiti wa vuguvugu la ‘Nouveau Zaïre’ (New Zaïre), lenye makao yake makuu mjini Brussels nchini Ubelgiji.
Mwanasiasa huyo pia alikuwa na ushawishi mkubwa katika nyanja ya kidini. Mnamo mwaka wa 2017, alipewa Msalaba Mkuu wa agizo la Ufalme wa Mtakatifu Petro na Paulo huko Vatikani.
Alifanikiwa kujenga ufuasi mkubwa wa kisiasa nje ya Kongo na alijulikana mara kwa mara kuelezea ukosoaji wake wa serikali ya Tshisekedi kwenye mitandao ya kijamii.
Katika chapisho kwenye X - zamani ikijulikana kama Twitter - Balozi wa Marekani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Lucy Tamlyn alisema kwamba 'alishtushwa' na ripoti kwamba raia wa Marekani walidaiwa kuhusika katika jaribio la mapinduzi.
"Tuwahakikishie kwamba tutashirikiana na mamlaka ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kadiri inavyowezekana wanapochunguza vitendo hivi vya uhalifu na kumwajibisha raia yeyote wa Marekani anayehusika," mwanadiplomasia huyo aliongeza.
Rais Tshisekedi bado hajatoa maoni yoyote hadharani kuhusu mashambulizi hayo.
Alichaguliwa tena Desemba mwaka jana kwa muhula wa pili katika uchaguzi uiliozozaniwa, watu 20 waliuawa kutokana na ghasia zinazohusiana na uchaguzi.
Mnamo Aprili, mwanauchumi Judith Tuluka aliteuliwa kuwa waziri mkuu, na kuwa mwanamke wa kwanza wa nchi kushikilia jukumu hilo. Lakini Bi Tuluka bado hajateua serikali yake.
DR Congo ni nchi yenye utajiri wa maliasili na inakadiriwa kuwa na watu zaidi ya milioni 100. Lakini nchi hiyo ina migogoro ya muda mrefu ya vurugu mashariki, migogoro ya kiuchumi na kijamii, na ukosefu wa uaminifu unaoendelea kati ya serikali na upinzani.
Jaribio hili la mapinduzi limesababisha wasiwasi, kwani bara limekumbwa na mapinduzi sita tangu 2020: mawili nchini Mali, mawili Burkina Faso na moja nchini Guinea na Niger mtawalia.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah