Je, unaweza kupata magonjwa kupitia choo cha kukalia?

fc

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 6

Unapoingia kwenye choo cha kukalia kinachotumiwa na mamia ya watu wengine, unaweza kuwa unajiuliza; vimelea vya magonjwa huishi kwa muda gani kwenye choo hicho? Utapata magonjwa kwa kukaa na kujisaidia?

"Kinadharia, ndiyo [unaweza kupata magonjwa kupitia choo cha kukalia], lakini hatari hiyo iko chini sana," anasema Jill Roberts, profesa wa afya ya umma na vijidudu katika Chuo Kikuu cha Florida, Marekani.

Mfano magonjwa ya zinaa (STDs). Wengi wa bakteria na virusi vinavyoweza kusababishia magonjwa hayo, kuanzia kisonono hadi klamidia, hawawezi kuishi kwa muda mrefu nje ya mwili wa kiumbe, achilia mbali kwenye sehemu yenye baridi, ngumu kama juu ya choo cha kukalia.

Ndiyo maana mengi ya magonjwa ya zinaa huambukizwa tu kupitia mguso wa moja kwa moja wa sehemu za siri na kubadilishana maji maji ya mwili.

Ili kuwa hatarini, labda itokee bahati mbaya ya mtu kuhamisha majimaji ya mwili ya mtu mwingine kutoka kwenye choo cha kukalia hadi kwenye sehemu ya siri kupitia mkono au karatasi ya choo, anasema Roberts.

Ingawa ni vyema kuwa waangalifu na kudumisha usafi, kama vile kuepuka vyoo vichafu, lakini si jambo ambalo linapaswa kukukosesha usingizi.

“Kama ingekuwa rahisi kupata maambukizi ya magonjwa ya zinaa kupitia vyoo vya kukalia, tungeona maambukizi ya mara kwa mara kwa watu wa rika zote, hata ambao hawana historia ya kufanya ngono," anasema Roberts.

Vile vile, Roberts anaongeza, hakuna uwezekano wa kupata ugonjwa unaoambukizwa kwa damu kupitia choo cha kukalia, hata kama utaikuta damu chooni. Damu hiyo haiwezi kusambaza vimelea vya magonjwa kwa urahisi bila kufanya ngono au kudungwa sindano chafu, anasema.

Pia ni vigumu kupata maambukizi ya mfumo wa mkojo yaani UTI kupitia choo cha kukalia, anasema Roberts. Utapata UTI ikiwa tu utahamisha kinyesi kutoka kwenye choo cha kukalia hadi kwenye njia ya mkojo, lakini ni kiasi kikubwa cha kinyesi kitahitajika kwa maambukizi kutokea, anafafanua Roberts.

Ni rahisi zaidi kupata UTI kwa kufuta kinyesi chako karibu sana na sehemu zako za siri kuliko kukaa juu ya choo, anaongeza.

Pia unaweza kusoma

Maambukizi unayoweza kupata

rf

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Katika vyoo vya umma, uchafu unaweza kuwa katika kitasa cha mlango sawa na bakuli la choo
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Lakini kuna baadhi ya magonjwa ya zinaa ni tofauti kidogo. Mfano, Virusi vya papiloma (HPV), ambavyo husababisha masundosundo (warts) katika sehemu ya siri, hivi vinaweza kukaa choni hadi wiki.

"Virusi hivi ni vidogo sana na vina ngome ya protini imara ambayo huwapa 'maisha ya marefu katika mazingira magumu," anasema Karen Duus, profesa wa vijidudu na kinga ya mwili katika Chuo Kikuu cha Touro huko Nevada.

Virusi vya HPV vina uwezo wa kustahimili vitakasa mikono ama sabuni, na inahitaji sabuni yenye 10 % ya kemikali ya sodium hypochlorite ili kuharibu ganda hilo gumu, anasema Duus.

Virusi hivi vinaweza kuingia mwilini mwako moja kwa moja, ikiwa tu ngozi yako ina tatizo, kama ina upele au jeraha, na ukaketi kwenye choo chenye virusi hao.

Kwa kawaida, HPV huambukizwa kupitia mgusano wa ngono wa ngozi kwa ngozi, kama vile kunyonyana mdomo, na kuingiliana mbele au nyuma.

Vile vile, mtu aliye na ugonjwa wa zinaa wa malengelenge (genital herpes) katika sehemu za siri, anaweza kumwaga virusi kwenye choo cha kukalia, watumiaji wanaofuata wanaweza kuwa katika hatari ya kuambukizwa ikiwa ngozi zao zina jeraha au wana kinga dhaifu ya mwili, anasema Daniel Atkinson, mkuu wa kliniki ya mtandaoni ya Treated.com nchini Marekani.

Nifunike choo au nichuchumae?

f

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kufunika choo kwa karatasi hakutazuia kuenea kwa vijidudu kwa sababu karatasi inapitisha maji maji

Kulingana na utafiti wa kikundi cha utafiti cha YouGov wa 2023, karibu 63% ya Wamarekani huketi wanapotumia choo cha umma - nusu ya hao hufunika karatasi kabla ya kuketi. Utafiti huo huo uligundua pia, karibu 20% wanachuchumaa juu ya choo cha kukalia.

Hata hivyo, karatasi au mfuniko wa kufunika choo huenda visikulinde dhidi ya vimelea vya magonjwa – kwani vimetengenezwa kuruhusu maji maji yapite, haviwezi kuzuia vijidudu kutopenya na kutogusa sehemu zako za siri.

Na kuchuchumaa kunaweza kusababisha madhara zaidi kuliko manufaa, kulingana na Stephanie Bobinger, mtaalamu wa afya ya nyonga katika Kitivo cha Matibabu katika Chuo Kikuu cha Ohio.

Wanawake wanapochuchumaa juu ya choo cha kukaa ili kukojoa, huikunja sakafu ya fupanyonga na misuli ya nyonga. Hii inazuia mtiririko wa mkojo kutoka katika kibofu, na hupelekea kusukuma mkojo kwa nguvu na kuipa fupanyonga kazi isiyo ya lazima.

Hali hiyo inamaanisha wanaweza wasitoe mkojo wote, na hilo wakati mwingine linaweza kusababisha maambukizi ya njia ya mkojo.

Charles Gerba, profesa wa magonjwa ya virusi katika Chuo Kikuu cha Arizona, anasema, "ni salama zaidi kutumia choo cha umma kuliko cha nyumbani katika maeneo mengi."

Katika maeneo mengi, wafanyakazi wa usafi husafisha vyoo vya umma mara kadhaa kwa siku, wakati vyoo vya vyumbani husafishwa mara moja kwa wiki, unasema utafiti wa Gerba. Ratiba bora ya kusafisha choo cha nyumbani, kulingana na Gerba, inapaswa kuwa kila baada ya siku tatu.

Kuna vijidudu vinavyosafiri pia. Kwa hiyo hatari haipo tu kwenye bakuli la choo unalokalia, pia ipo kwenye vitasa vya mlango, vitufe vya kusukuma maji, bomba za kujisafishia, karatasi za kujisafishia, hivi ni vitu ambavyo unavigusa moja kwa moja na mikono yako. Na sehemu hatari zaidi ni sakafu ya choo, anasema Gerba.

Kwa bahati mbaya, choo mara nyingi huwa na vijidudu vya maradhi ambavyo si lazima uvihusishe na mkojo au kinyesi cha mtu, bali kwa kupiga chafya na kukohoa. Kwa mfano, virusi vya mafua wakati mwingine vinaweza kupatikana kwenye kuta za choo.

Jinsi ya kujikinga

gfv

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wataalamu wanapendekeza choo chako cha nyumbani kinapaswa kusafishwa kila baada ya siku tatu

Elizabeth Paddy, mhandisi wa usafi wa maji katika Chuo Kikuu cha Loughborough nchini Uingereza, anapendekeza kugusa vitu kidogo kadiri iwezekanavyo ukiwa chooni.

Kwa kweli, njia moja watengenezaji wa vyoo wanaweza kukifanya choo kuwa salama zaidi ni kubuni njia za kutumia choo bila kugusa vitu vingi, mfano kutogusa chupa za sabuni, vikaushio vya mikono n.k anasema Paddy.

Paddy anashauri kwamba watengenezaji wa vyoo wanapaswa kuondoa vitufe vya kubonyeza kwa mkono, ili kuepuka watu kugusa gusa.

Pia kuna dawa za kupuliza ambazo zimethibitishwa kuwa na ufanisi katika kusafisha hewa na kuta za choo na maeneo ya choo, hivyo husaidia kukabiliana na vimelea kutoenea.

Chaguo jingine ni kuflashi na kisha kuondoka. "Kwa kawaida mimi husafisha na kukimbia," anasema Gerba. Pia anapendekeza kungoja dakika 10 kabla ya kwenda kwenye choo cha umma baada ya mtu mwingine kutoka, ingawa hilo linaweza kuwa gumu.

Simu za mkononi. Haipendekezwi kutumia simu yako ukiwa chooni, anasema Roberts – simu yako tayari ni chafu sana, kwani unaipeleka kila sehemu, na kuiweka kila sehemu, na kuigusa kila wakati.

Ikiwa utaipeleka chooni, utahatarisha kuiongezea bakteria, kisha utawabeba hata baada ya kuosha mikono yako.

Jambo rahisi zaidi unaloweza kufanya ni kunawa mikono mara tu baada ya kwenda chooni, anasema Gerba. Inapendekezwa kunawa mikono kwa sekunde 20.

Ili kuzuia kuambukizwa ugonjwa katika choo, osha mikono yako. Ongeza na kupaka kisafisha mikono pia, kwa kuwa mchanganyiko huo ni ulinzi zaidi. Na ondoa hofu juu ya bakteria wa chooni - kwani hatari huenda iko chini kuliko unavyofikiri.