Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Nyota 6 wa kutazama AFCON 2025
Toleo la 35 la Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) litaanza Desemba 21, 2025 nchini Morocco, huku fainali ikipangwa kuchezwa mjini Rabat Januari 18, 2026.
Wenyeji Morocco watakuwa wakisaka taji lao la kwanza tangu mwaka 1976, wakati huo huo Mohamed Salah akiwa na nafasi ya kuweka pembeni mustakabali wake wa klabu ya Liverpool ili kuiongoza Misri kutwaa ubingwa wao wa kwanza tangu 2010.
Miongoni mwa nyota wengi wakubwa watakaoshiriki, BBC Sport Africa inawasilisha wachezaji sita wanaotarajiwa kung'ara na kuvutia macho ya mashabiki.
Azzedine Ounahi (kiungo wa kati, Morocco)
Nahodha na Mwanasoka Bora wa Afrika, Achraf Hakimi, anaweza kulazimika kupambana na muda ili awe tayari kwa hatua za mwishoni za mashindano. Hali hiyo inaweza kuwafanya wenyeji kutafuta msukumo kutoka kwa nyota wengine.
Brahim Diaz wa Real Madrid alikuwa mfungaji bora wa michuano ya kufuzu akiwa na mabao saba, lakini Azzedine Ounahi, anayesimamia kasi na mwelekeo wa mchezo katikati ya uwanja wa Simba wa Atlas, ndiye anayetarajiwa kuangaza zaidi.
Ounahi, aliyekulia katika Chuo maarufu cha Mohammed VI, alipitia kipindi kigumu alipohamia Marseille baada ya kung'ara kwenye Kombe la Dunia 2022. Hata hivyo, tangu ajiunge na Girona ya Hispania Agosti iliyopita, kiungo huyo mwenye umri wa miaka 25 ameanza kurejea kwenye kiwango chake bora.
Morocco, watakaokutana na Comoros, Mali na Zambia katika Kundi A, wana hazina ya viongozi uwanjani akiwemo kipa mahiri Yassine Bonou na mshambuliaji mkongwe Youssef En-Nesyri.
Swali linabaki, je, Ounahi ataweza kubeba jukumu kubwa endapo Hakimi atakuwa nje kwa sababu ya majeraha?
Mohamed Amoura (mshambuliaji, Algeria)
Akiwa mfungaji bora wa Afrika katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia, mwaka 2025 kwa sasa ni wa Mohamed Amoura.
Mshambuliaji huyo wa Wolfsburg amefunga mabao 11 katika mechi nane tangu Machi, yakiwemo mabao matatu katika ushindi dhidi ya Msumbiji.
Kiwango hicho kimefanya kijana huyo wa miaka 25 kujihakikishia nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha Algeria.
Ingawa Riyad Mahrez bado ndiye mhimili wa mabingwa wa AFCON 2019, Amoura ameunda maelewano mazuri na nyota huyo.
Licha ya urefu wake wa mita 1.70, wapinzani wao wa Kundi E ambao ni Sudan, Burkina Faso na Equatorial Guinea wanapaswa kufahamu kuwa Amoura ni tishio hata katika mipira ya juu.
Victor Osimhen (mshambuliaji, Nigeria)
Ni chaguo lisiloepukika. Hatima ya Nigeria inaonekana kufungamana kwa karibu na upatikanaji na kiwango cha mshambuliaji huyo wa Galatasaray.
Super Eagles walikusanya pointi nne pekee kati ya 15 zinazowezekana alipokosekana katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2026, kampeni iliyomalizika kwa mafanikio duni.
Osimhen ni mhimili wa mfumo wa kocha Eric Chelle, na Nigeria ilipoteza mwelekeo ilipolazimika kucheza bila yeye baada ya kuumia katika mechi ya mchujo dhidi ya DR Congo.
Akielezwa na mwenzake Frank Onyeka kuwa yuko "kiwango cha juu kabisa," Osimhen atalazimika kuwa katika ubora wake iwapo Nigeria inataka kufanya vyema kuliko nafasi ya pili waliyoipata AFCON iliyopita nchini Ivory Coast.
Mabingwa hao mara tatu wataanza dhidi ya Tanzania katika Kundi C, kabla ya kukutana na Uganda na Tunisia, mabingwa wa mwaka 2004.
Ibrahim Mbaye (mshambuliaji, Senegal)
Sadio Mané bado ndiye nyota mkuu wa mabingwa wa AFCON 2021, wakisaidiwa na Iliman Ndiaye na Ismaila Sarr kuunda safu kali ya ushambuliaji.
Hata hivyo, ulimwengu wa soka unaweza kugundua kipaji kipya cha Simba wa Teranga kupitia Ibrahim Mbaye.
Kijana huyo mwenye umri mdogo, aliyewahi kuiwakilisha Ufaransa katika ngazi za vijana, ameanza kucheza soka la wakubwa akiwa na Paris Saint-Germain msimu huu.
Alianza katika mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Barcelona, baada ya kuanza msimu kama mchezaji wa akiba kwenye ushindi wa Super Cup ya Ulaya dhidi ya Tottenham.
Mbaye aliichezea Senegal kwa mara ya kwanza dhidi ya Brazil, na siku chache baadaye akaweka historia kwa kuwa mfungaji mwenye umri mdogo zaidi nchini humo, akiwa na miaka 17 na siku 298, baada ya kufunga katika ushindi wa mabao 8–0 dhidi ya Kenya.
Rogers Mato (mshambuliaji, Uganda)
Cranes wanarejea AFCON kwa mara ya kwanza tangu 2019 walipotolewa katika hatua ya 16 bora, huku pia wakijiandaa kuwa wenyeji wa fainali ya 2027.
Chini ya kocha Paul Put, Uganda ilimaliza nafasi ya pili katika kundi lao la kufuzu Kombe la Dunia nyuma ya Algeria, huku Rogers Mato akiwa mfungaji bora kwa pamoja akiwa na mabao matatu.
Winga huyo wa kushoto mwenye umri wa miaka 22 alifunga mabao mawili maridadi dhidi ya Msumbiji Septemba na anaendelea kung'ara na klabu yake ya Vardar nchini Macedonia Kaskazini.
Uganda itakutana na mabingwa wa zamani Nigeria na Tunisia katika Kundi C, pamoja na Tanzania, mwenyeji mwenza wa AFCON 2027, katika dabi ya Afrika Mashariki.
Mato anaweza kuwa mhimili muhimu katika safari ya Cranes kutinga hatua ya mtoano.
Reinildo (beki, Msumbiji)
Msumbiji inaelekea Afrika Kaskazini bila kuwahi kuvuka hatua ya makundi katika ushiriki wao tano zilizopita AFCON. Hata hivyo, kwa mara ya kwanza, wana mchezaji anayecheza katika Ligi Kuu ya England.
Reinildo aliweka historia kwa kuwa Msumbiji wa kwanza kucheza Ligi Kuu ya England baada ya kujiunga na Sunderland kutoka Atlético Madrid Julai.
Akiichezea nafasi ya beki wa kushoto, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 amesaidia Sunderland kuanza msimu kwa kasi.
Nguli wa soka la Msumbiji, Tico Tico, alimuelezea Reinildo kama mhimili wa timu ya Mambas, akisema ni jasiri, huunganisha wachezaji wenzake na ana dhamira inayosaidia timu kupata matokeo mazuri.
Ikiwa katika Kundi F pamoja na mabingwa watetezi Ivory Coast, Cameroon na Gabon, Reinildo na Msumbiji watalazimika kucheza soka la kiwango cha juu ili kuandika historia mpya.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Ambia Hirsi