Kwanini nchi za Kiarabu haziwaungi mkono Wapalestina kama zamani?

    • Author, Paula Rosas
    • Nafasi, BBC News World
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

“Waarabu wako wapi?! Waarabu wako wapi?!”

Wakitoka kwenye kifusi, wamebeba watoto waliouwawa, wakipiga kelele bila msaada mbele ya kamera. Swali hilo limerudiwa na wananchi wa Gaza - wanaoshangaa kwa nini majirani zao nchi za Kiarabu hawawatetei kutokana na mashambulizi ya Israel.

Baada ya shambulio la Hamas kusini mwa Israel mwezi Oktoba 7, 2023, ambapo Waisraeli 1,200 waliuawa na wengine 250 kutekwa nyara - macho yote yalielekezwa Mashariki ya Kati.

Mashambulio ya mabomu ya Israel yameharibu Ukanda wa Gaza na kugharimu maisha ya Wapalestina zaidi ya 42,500, na bado mashambulizi hayo hayajamaliza.

Ikiwa mtu alitarajia maandamano makubwa katika miji mikuu ya nchi za Kiarabu atakuwa amekatishwa tamaa. Ingawa wengi katika nchi za Kiarabu wana mshikamano na kadhia ya Palestina, lakini maandamano yamekuwa machache na yamedhibitiwa.

Walid Kazziha, profesa wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha American University in Cairo (AUC), anasema.

“Zaidi ya ukosoaji dhidi ya Israel, na jukumu la upatanishi ambalo serikali ya Qatar na Misri zimechukua, hakuna nchi yoyote ya Kiarabu ambayo imevunja uhusiano na Israel au imetoa shinikizo la kidiplomasia au kiuchumi kujaribu kumaliza vita.”

Pia unaweza kusoma

Raia na Serikali za Kiarabu

Uhusiano kati ya Wapalestina na nchi za Kiarabu haujakuwa rahisi, haswa katika zile nchi zilizopokea idadi kubwa ya wakimbizi baada ya kutangazwa kwa nchi ya Israeli mwaka 1948.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Lebanon au mapigano kati ya wanamgambo wa Kipalestina na utawala wa kifalme wa Jordan ni ukumbusho wa historia yenye migogoro.

Lakini kadhia ya Palestina, kwa miongo kadhaa ilikuwa sababu ya kuungana kwa nchi za Kiarabu.

“Katika kipindi hicho, taifa la Israel lilionekana "kama upanuzi wa madola ya zamani ya kikoloni, ambayo yalijiondoa Mashariki ya Kati lakini yaliiacha Israel kama wakala wa kulinda maslahi yao, yaani Uingereza na Ufaransa na sasa maslahi ya Marekani,” anaeleza Tamer Qarmout, Profesa wa sera katika Taasisi ya Doha Institute for Graduate Studies.

Vita ambavyo nchi ya Misri, Syria au Jordan vilipigana dhidi ya Israel hapo awali vilitetea masilahi ya kitaifa, lakini pia maslahi ya Wapalestina.

Lakini vita hivyo ni vya zamani. Misri na Jordan zilitia saini mikataba ya amani na Israel miongo kadhaa iliyopita. Morocco, Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain zimerejesha uhusiano wao na nchi hiyo ambayo hadi miaka michache iliyopita, ilikuwa imetengwa katika eneo hilo.

Hata Saudi Arabia ilikuwa karibu kuanzisha uhusiano na Israel kabla ya Oktoba 7 na uvamizi wa ardhini wa Israel huko Gaza.

Dov Waxman, mkurugenzi wa kitivo cha masomo ya Israel, katika Chuo Kikuu cha California anasema, "tangu mwanzo wa mzozo hadi leo, kila moja kati ya nchi za Kiarabu imefuata masilahi yake.”

"Wanazungumzia kuhusu mshikamano na kuunga mkono Wapalestina, na sio kwamba hisia hizo si za kweli, ni za kweli lakini mwishowe zinafuata maslahi yao ya kitaifa."

“Maoni ya umma katika nchi za Kiarabu yanaonyesha watu kukasirishwa sana na Israel,” anasema Elham Fakhro, mtafiti juu ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini katika taasisi ya Chatham House.

"Kuna huruma kubwa kwa maafa ambayo watu wa Gaza wanakabiliwa nayo, na wanataka serikali zao kufanya zaidi. Wanataka uhusiano wa kidiplomasia ukatishwe. Wanataka mabalozi waondoshwe, lakini serikali zao hazifanyi hivyo."

Kulingana na Imad K. Harb, mkurugenzi wa Utafiti na Uchambuzi katika Kituo fikra huria cha Arab Center huko Washington, DC, anasema, "serikali za nchi za Kiarabu zimewatelekeza Wapalestina muda mrefu uliopita."

Maandamano ya nchi za Kiarabu

Tamer Qarmout, anaamini kuna mabadiliko ambayo yamebadilisha mwelekeo mzima wa eneo hili; uasi na maandamano maarufu ambayo yalitikisa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini kati ya 2010 na 2012.

"Tangu wakati huo, nchi nyingi bado zimezama katika migogoro ya wenyewe kwa wenyewe, kama vile Yemen, Syria na Iraq. Hizi mbili za mwisho, zilikuwa na nguvu na mawazo ya kisiasa ambayo yalitoa changamoto kwa Marekani, zimetoweka.”

"Libya imetoweka, Misri imetumbukia katika machafuko ya kiuchumi, Sudan iko kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe..." anasema Qarmout.

Katikati ya hali hii ya misukosuko, Waarabu, ingawa wanawahurumia Wapalestina, “wanajihisi hawana msaada, wao wenyewe wanaishi chini ya dhuluma, utawala wa kimabavu na udikteta. Ulimwengu wa Kiarabu uko katika hali ya kusikitisha, watu hawana uhuru au uwezo wa kuishi kwa heshima,” anasema.

Hata hivyo, mwitikio wa kijamii umekuwa mkubwa zaidi kuliko ule wa serikali, ingawa unaonekana zaidi kwenye mitandao ya kijamii.

Tangu kumalizika kwa maandamano ya nchi za kiarabu, kumekuwa na marufuku ya kufanya harakati katika mitaa ya nchi nyingi za eneo hilo, kama vile Misri.

Kuna wakati ambao serikali za kimabavu ziliruhusu watu kutoa dukuduku lao katika maandamano ya kuwatetea Wapalestina, leo serikali mpya zinahofia maandamano haya yataleta jambo jingine.

Uhusiano na Israel

"Machipuo ya Kiarabu yalikuwa tetemeko la ardhi na yalibadilisha hali ya mambo. Na serikali nyingi za Kiarabu ziliingia kwenye wazo la Marekani kwamba Israel, mshirika wao katika eneo hilo, inaweza kuwalinda,” anasema Tamer Qarmout.

Miaka michache baadaye, chini ya upatanishi wa Marekani - na Donald Trump - Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu zilitia saini Mkataba wa Abraham, kuunda uhusiano na Israel na baadaye Morocco na Sudan zilijiunga.

Matokeo ya uhusiano huo yakazaa matunda, kwa mfano Marekani ikatambua mamlaka ya Morocco juu ya Sahara Magharibi, eneo ambalo linataka kujitawala.

"Tunapochunguza uhusiano ambao nchi hizi zimeanzisha na Israel, tunaona kimsingi unahusiana na Israel kuwauzia mifumo ya kupeleleza watu wao wenyewe," anasema Walid Kazziha.

Kesi zinazohusisha udukuzi wa Pegasus, programu iliyotengenezwa na kampuni ya Israel ya NSO Group, zimetokea Morocco, Emirates na Bahrain, na hata Saudi Arabia, licha ya hii ya mwisho kutokuwa na uhusiano rasmi na Israel.

Kwa mujibu wa gazeti la The New York Times, Riyadh ilinunua programu hiyo mwaka 2017, lakini ikaipoteza huduma hiyo kufuatia mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul mwaka uliofuata.

Lakini mtoto wa mfalme, Mohamed bin Salmán, alifanikiwa kuirejesha huduma hiyo baada ya kumpigia simu Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ambaye aliingilia kati kuiruhusu Saudi Arabia kutumia programu hiyo tena, kulingana na gazeti la hilo la Marekani.

Hofu juu siasa kali za Kiislamu

Mbali na maslahi yao ya kitaifa, sababu nyingine ya nchi za Kiarabu kujiweka mbali na kadhia ya Palestina; ni kuongezeka kwa wanamgambo wa Kiislamu.

Wimbi la kwanza la upinzani wa Wapalestina baada ya vita vya 1967, lililokuwa chini ya uongozi wa Yasser Arafat, linaweza kuhesabiwa kuwa la kitaifa, kulingana na profesa na AUC, lakini wimbi la leo lina mizizi ya kidini zaidi.

"Wale wanaopigania kadhia hiyo leo - kimsingi ni Waislamu wa siasa kali, iwe ni Hamas au Hezbollah."

Uhusiano wa Hamas na Muslim Brotherhood, vuguvugu la Kiislamu ambalo limepambana na serikali kadhaa za eneo hilo, unasababisha serikali nyingi kuiona Hamas kama tishio.

"Wanaiona Hamas kama ngome ya mwisho iliyosalia ya Muslim Brotherhood, fauka ya hilo ni ngome ya kijeshi, yenye nguvu," anasema Qarmout.

“Na Israel, kwa namna fulani, inaonekana inafanya kazi yake chafu ya kuiharibu Hamas,” anaongeza profesa wa Taasisi ya Doha.

Wasiwasi juu ya Iran

Uhusiano wa Hamas, Hezbollah na Iran pia unazifanya nchi za Kiarabu kuwa na mashaka. Kwa nchi za Ghuba, Iran ni tishio kubwa kuliko Israel.

Serikali nyingi za Kiarabu "zimekubali simulizi ya Israel na Marekani kwamba makundi haya ni silaha za Iran katika kanda hiyo na yameundwa kuhujumu amani ya eneo hilo kwa kupitia Wapalestina," anaeleza Qarmout.

Hii ni simulizi inayotetewa kwa sehemu kubwa na vyombo vya habari katika ulimwengu wa Kiarabu, eneo ambalo hakuna vyombo vya habari huru.

"Kwa vyombo vya habari vya Saudia, wasiwasi wao mkubwa sio Palestina, lakini jinsi Iran inavyozidi kuimarika," anasema Kazziha.

Leo hii Hamas inapata uungwaji mkono na ufadhili kutoka Iran, lakini wakati kundi la hilo lilipozaliwa, lilikuwa na uhusiano mzuri na nchi kadhaa za Kiarabu, mataifa hayo baadaye yalikosa imani na nguvu ambayo harakati hiyo ilikuwa ikiipata.

"Unapoiweka Iran mbele, huzioni tena nchi za Kiarabu kwenye kadhia hiyo, na hasa kwa kuwa kuna mavuguvugu ambayo yana nia ya dhati ya kuwaunga mkono Wapalestina na hata kuwafia, kama vile Hezbollah, Houthis huko Yemen na baadhi ya makundi ya kishia nchini Iraq," anasema mtafiti wa AUC.

Mabadiliko ya kizazi

Mbali na maslahi ya kijiografia na migogoro katika nchi za Kiarabu, muda nao unaongeza kusahaulika kwa kadhia ya Palestina. Dhana zilizowahi kuiunganisha Mashariki ya Kati, kama vile pan-Arabism, kwa sasa ni dhana za zamani.

"Watu wengi katika kizazi kipya katika eneo hili wanahisi huruma kwa Wapalestina, lakini hawajui maendeleo ya mzozo huo kwa sababu hawafundishwi tena shuleni. Katika miaka ya 60 na 70 nchi nyingi za Kiarabu zilikuwa na mtaala kamili wa shule juu ya Palestina, lakini leo utandawazi na utambulisho umebadilisha mambo," anaeleza Qarmout.

"Katika nchi za Ghuba, kwa mfano, kuna kizazi kipya cha viongozi kama Mohamed Bin Salman huko Saudi Arabia, ambao wengi wao wamesoma katika nchi za Magharibi na malengo na vipaumbele vyao ni mbali na kadhia ya Palestina," anahitimisha Profesa Qarmout .

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah