Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Maandamano ya upinzani Afrika, ni sawa na vuguvugu la`Arab Spring`?
- Author, Mohammed AbdulRahman
- Nafasi, Mchambuzi
Nchi kadhaa barani Afrika zimeandamwa na maandamano ya umma. Licha ya tofauti za mazingira au niseme chanzo na sababu za matukio hayo, lakini moja linalofanana ni malalamiko dhidi ya serikali zilizo madarakani kushindwa kutimiza ahadi zilizo na zinazoendelea kutolewa.
Matumaini ya umma ni kwamba angalau hali zao za maisha zingeweza kuwa bora, lakini badala yake wao walio wengi wanaendelea kuishi maisha magumu na walio wachache wakizidi kunufaika .
Kila uchao pengo kati ya matajiri na masikini linaongezeka. Ukiyaweka yote pamoja ni kwamba yanasababisha demokrasia ambayo ndiyo nguzo muhimu ya kusimamia maisha yao ya kila siku kushindwa kufanya kazi .
Zingatio la Makala haya ni Je,maandamano ya upinzani barani Afrika katika nchi kama Afrika Kusini , Nigeria, Kenya na Tunisia kwa kuzitaja chche yanaweza kufanana na kile tulichokiona 2011na kujulikana kwa kimombo kama `Arab spring´, ambacho mimi ningekiita Vuguvugu la umma la kiarabu. Hili lilikuwa vuguvugu la kupigania mabadiliko katika nchi za kiarabu katika ukanda wa Afrika kaskazini.
Chimbuko la vuguvugu hilo lilikuwa nchini Tunisia dhidi ya utawala wa kiimla wa Rais Zein el Abidine Ben Ali, na kuvuka mipaka hadi nchi jirani za Misri na Libya. Watawala wa muda mrefu wa nchi hizo Mohamed Housni Mubarak na Muammar Gaddafi nao wakaangushwa. Kilichotokea kiliyatia hofu mataifa mengine ya Kiarabu, nje ya Afrika ikiwemo Syria.
Matarajio hata hivyo yamekumbwa na vizingiti vipya. Nchini Misri demokrasia liligeuka kuwa zoezi zoezi la muda mfupi. Utawala wa Rais Mohamed Morsi aliyechaguliwa kidemokrasi kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo 2012 ulidumu mwaka mmoja tu, kabla ya wanajeshi kurudi tena madarakani . Libya baada ya Gaddafi kun`golewa na kuuwawa, hadi sasa nchi imegawika kukiwa na serikali mbili tofauti na ukosefu mkubwa wa usalama.
Katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara, maandamano yana sura tafauti kidogo. Mfano Afrika Kusini ambayo ina historia ndefu ya maandamano tangu enzi za utawala wa kibaguzi wa wazungu wachache, ambapo mamia kwa maelfu walimwaga damu, leo wananchi wake bado wanaandamana kudai sehemu ya uhuru walioupigania na ahadi walioyatarajia.
Chama tawala African National Congress (ANC) kiliahidi mengi ikiwa ni pamoja na kuwapa raia wake elimu, afya na makazi pamoja na maji safi, hasa katika vitongoji vya miji mikubwa wanakoishi wengi wa wakaazi masikini. Miaka thelathini tangu kumalizika utawala wa kibaguzi Àpartheid` kuwa na demokrasia, hali ni ile ile na sehemu nyengine ni mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa awali.
Maandamano yamekuwa ni jukwaa la malalamiko dhidi ya ubadhirifu wa mali ya umma, rushwa na kujitajirisha kunakofanywa na wanasiasa wa chama tawala na kuzidi kwa maisha ya wananchi kuwa magumu.
Maandamano ya maelfu ya raia mwezi Januari mwaka huu kwa mfano, yalikuwa ni kulalamika kuhusu tatizo la umeme ambapo limevuruga sio tu maisha yao ya kawaida lakini pia kuathiri sehemu kubwa ya uchumi wa viwanda vya taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa maliasili barani Afrika.
Kwa kipindi kirefu serikali imelazimika kugawa umeme kwa utaratibu fulani.Rais Cyril Ramaphosa amesema serikali itaagiza umeme kutoka ngambo na kuongeza utoaji umeme kupitia vyanzo mbadala vya utoaji umeme.
Nigeria taifa lenye idadi kubwa ya wakazi barani Afrika wakikaribia 220 milioni, hali nako si nzuri. Mwezi Februari 2023, ulifanyika uchaguzi uliokamilisha muhula wa Rais Muhamadu Buhari.
Malalamiko ya raia katika kipindi cha miaka 8 ya utawala wake yaliohusiana na hali ngumu ya maisha na mashambulio ya kundi la wapiganaji wa itikadi kali Boko Haram, magenge yanayowateka nyara raia na kudai malipo ya fidia ya fedha .
Sambamba na hayo ni kukidhiri kwa rushwa na kujitajirisha kwa kiwango kikubwa kwa wanasiasa .
Nigeria imekuwa ikiangaliwa kuwa gurudumu la kusukuma mbele demokrasia magharibi mwa Afrika, tangu ulipofunguliwa ukurasa mpya 1999 na kumaliza miaka mingi ya tawala wa kijeshi katika nchi hiyo.
Hata hivyo uchaguzi wa Februari umeiwekea alama ya kuuliza demokrasia. Wakati mgombea wa chama tawala All Progressive Congress Bola Ahmed Tinubu akiwa ametangazwa mshindi wa uchaguzi ,wapinzani wa Tinubu wamekwenda mahakama ya juu kupinga matokeo.
Kumefanyika maandamano kupinga matokeo, ingawa katika kiwango kidogo. Kwa sasa hali ni shwari lakini haitoshangaza kuona maandamano yakiibuka kwa nguvu kubwa baada ya uamuzi wa mahakama kuhusu ushindi wa Tinubu na kumpa mtihani Rais huyo mteule katika awamu ya kwanza ya miaka minne ya utawala wake.
Kilichonishtuwa na kuwashtuwa wengi wakati wa kipindi cha kampeni ya uchaguzi ni kauli ya Tinubu kwamba `It is my turn` (Ni zamu yangu). Historia ya siasa za Nigeria imegubikwa na ushawishi wa majenerali wa kijeshi na matajiri wakubwa.
Tinubu ni mmoja wao aliyemsaidia Buhari kuwa kupata ushindi. Fedha hutumiwa na matajiri kama mtaji wa kuwekeza kwa mustakbali wao wa baadae katika kisiasa. Ninakumbuka nilichambiwa na rafiki yangu mmoja wa Kihausa kwamba “ Nigeria baada ya utajiri ni madaraka.” Pengine hakukosea.
Kenya, ni taifa linalotajwa sasa kuwa mfano wa demokrasia na uhuru wa kutoa maoni katika ukanda wa Mashariki mwa Afrika. Miaka ya nyuma hadi inarudi katika mfumo wa vyama vingi vya siasa 1991, ilishuhudia maandamano yakikandamizwa na utawala wa Rais Daniel Arap Moi.
Matukio ya machafuko ya 2007 na 2008 yaliofuatia ushindi uliozusha utata wa mrithi wake Mwai Kibaki, nayo yakasababisha maandamano makubwa ya upinzani ambayo pia yalikandamizwa na vikosi cha usalama.
Malalamiko hayakuhusiana tu na uchaguzi bali pia mizozo ya kibinadamu na matatizo ya kiuchumi. Katiba mpya ilifungua ukurasa mpya 2010 pale wakenya walipoidhinisha katiba mpya iliogeuka nguzo muhimu katika maisha yao.
Wakati huu maandamano ya upinzani yamegeuka jukwaa la kulalamikia matokeo ya uchaguzi wa Agosti 2022 yaliompa ushindi Rais William Ruto.
Mpinzani wake Raila Odinga na wafuasi wake hawakubaliani na matokeo hayo. Wanajaribu kuyapa nguvu madai yao kwa maandamano na mikutano ya hadhara wakiyajumuisha pia masuala ya kupanda bei kwa vitu muhimu kama unga na mahitaji mengine ya kila siku, jambo ambalo limekuwa ni mzigo kwa raia. Serikali ya Ruto inayavumilia maandamano hayo, ingawa kuna wasi wasi kufuatia onyo linalotolewa dhidi ya mpango wa upinzani kufanya maandamano makubwa kushinikiza madai yake.
Tunisia kulikoanzia vuguvugu la Arab spring demokrasia imo hatarani. Vuguvugu hilo linakabiliwa na hatari ya kupigwa kitanzi sawa na ilivyotokea Misri, Libya na hata katika nchi nyengine za kiarabu ikiwemo Syria. Rais wa Tunisia Kais Saied, wa pili baada ya dikteta Ben Ali, sio tu ameamua kuwaandama wanasiasa wa upinzani na vyama vyao vya siasa lakini pia kuisimamisha katiba.
Kibaya zaidi, hivi karibuni ametoa tamko liliowatia hofu wahamiaji kutoka nchi za kiafrika kusini mwa jangwa la Sahara, ilioonekana ya kibaguzi, aliposema wanamiminika kwa wingi na kutishia kubadili sura na mazingira ya Tunisia. Alijitoa kimasomaso kwa kusema yeye ni mwaafrika na anajivunia kuwa mwaanfrika , lakini kauli yake dhidi ya wahamiaji imetafsiriwa kuwa ya kibaguzi. Kwa hiyo Vuguvugu la mabadiliko ya umma la Arab Spring limeishia ukingoni. Huenda Watunisia wameanza kujipanga kuandamana upya huku Saied akivitumia vyombo vya dola kujizatiti madarakani.
Licha ya kuwa Vuguvugu la Arab Spring lilifuatiliwa kwa karibu barani Afrika lakini mazingira yanatafautiana kutoka nchi moja au nyengine. Muhimu ni watawala kutambua kwamba, maandamano ni haki ya kikatiba na kudai mabadiliko si usaliti. Hatimaye uamuzi ni matokeo kwenye sanduku la kura ambapo matarajio ya raia ni kwamba yataheshimiwa pasina udanganyifu. Amani,haki na uwazi ndiyo matunda ya demokrasia ya taifa lolote .