Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Hezbollah iko njia panda baada ya kipigo katika vita vilivyowadhoofisha
- Author, Hugo Bachega
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Mwaka jana, tarehe 17 Septemba, kifaa cha mawasiliano cha pager ambacho muuguzi anayeitwa Adam alipewa mwanzoni mwa zamu yake katika hospitali ya Lebanon kilipokea ujumbe.
Vifaa hivyo vilisambazwa na Hezbollah, kundi la Waislamu wa Shia, kwa maelfu ya wanachama wake, akiwemo Adam, kwa ajili ya kupokea taarifa ya dharura au maafa.
"Pager ilianza kulia bila kuacha, na kwenye skrini ilisomeka 'alert' (tahadhari)," anasema Adam, ambaye hakutaka kutumia jina lake halisi kwa sababu za usalama.
Ujumbe huo ulionekana kutumwa na uongozi wa kikundi hicho. Ili kuusoma, alilazimika kubofya vitufe viwili kwa pamoja, kwa mikono yote miwili. Adamu alifanya hivyo mara nyingi, lakini milio iliendelea. Anasema, "kisha ghafla, nilipokuwa nimeketi kwenye dawati langu, pager ililipuka."
Kwenye simu yake, Adam alinionyesha video ya chumba hicho, iliyorekodiwa na mwenzake dakika chache baada ya mlipuko. Kulikuwa na damu kwenye sakafu. "Nilijaribu kutambaa hadi mlangoni kwa sababu nilikuwa nimeufunga wakati nabadilisha nguo zangu," anasema.
Mlipuko huo ulisababisha shimo kwenye dawati la mbao na niliona vidole vyangu.
Hezbollah ni wanamgambo wenye nguvu na wameorodheshwa kama shirika la kigaidi na nchi nyingi za Magharibi zikiwemo Uingereza na Marekani. Lakini nchini Lebanon, pia ni vuguvugu muhimu la kisiasa lenye uwakilishi bungeni na shirika la kijamii.
Nchini Lebanon kuwa mwanachama wa Hezbollah haimaanishi kuwa wewe ni mpiganaji. Kwa hakika, wengi wao sio wapiganaji. Adam aliniambia hajawahi kuwa mpiganaji. Watu hufanya kazi katika taasisi za kikundi hicho kama hospitali na huduma za dharura.
Hezbollah iliwapa wanachama wake pager za teknolojia ya chini kwa ajili ya kuwasiliana badala ya simu za kisasa ambazo ilihofia zingeweza kudukuliwa na Israel, adui wake mkuu, ili kukusanya taarifa nyeti kuhusu kundi hilo.
Hata hivyo, ilibainika kuwa vifaa ambavyo Hezbollah ilivisambaza vilikuwa sehemu ya mpango wa miaka mingi wa Israel. Kilipuzi kilikuwa kimefichwa ndani ya pager, kikisubiri kulipuliwa - na ndivyo ilivyotokea siku hiyo.
Katika shambulio hilo, Adam, mwenye umri wa miaka 38, alipoteza kidole gumba na vidole viwili kwenye mkono wake wa kushoto, na sehemu ya kidole kwenye mkono mwingine. Amepofuka katika jicho lake la kulia, na anaona kwa jicho moja tu.
Alinionyesha picha yake akiwa katika kitanda cha hospitali, iliyochukuliwa saa moja baada ya mlipuko huo, uso wake ukiwa umeungua, ametapakaa damu, akiwa na bandeji.
Licha ya majeraha yake, Adam aliendelea kujitolea kwa Hezbollah. Nilimuuliza anajisikiaje alipojitazama. "Vizuri sana," alisema kwa Kiingereza. Kisha, kwa Kiarabu, aliniambia: "Kwa sababu tunaamini majeraha ni aina ya medali kutoka kwa Mungu. Ni heshima kwa kile tunachopitia katika kupigana haki."
Pigo kwa Hezbollah
Lakini kundi hilo halina tena nguvu ambazo lilikuwa nazo baada ya kupata pigo kubwa katika vita - ambapo Israel ilipiga mabomu na kuivamia Lebanon, baada ya mashambulizi ya pager, na kwa sasa Hezbollah inakabiliwa na changamoto kubwa.
Nchini Lebanon kuna kutoridhika kwa baadhi ya wafuasi juu ya ukosefu wa fedha za ujenzi baada ya uharibifu, huku serikali mpya ya nchi hiyo ikiapa kulipokonya silaha kundi hilo.
Katika nchi jirani ya Syria, kuondolewa madarakani kwa utawala wa Bashar al-Assad kumevuruga njia inayotumiwa na Iran, kwa usambazaji wa silaha na pesa. Iran ni mfadhili mkuu wa Hezbollah.
Nilitembelea jamii za kusini mwa Lebanon ambazo ziliharibiwa na mashambulizi ya Israel, na nikaona uungaji mkono kwa Hezbollah unaonekana haujapungua. Lakini maoni ya wachache, wanaounga mkono kundi hilo, wanasema kuingia vitani lilikuwa ni kosa, na wanatilia shaka mustakabali wa kundi hilo kama jeshi.
Hezbollah, au Chama cha Mungu, kiliundwa katika miaka ya 1980 ili kukabiliana na uvamizi wa Israel nchini Lebanon wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Lebanon. Hadi leo, moja ya malengo yao rasmi ni kuiharibu Israel.
Vita vya mwisho kati ya Israel na Hezbollah vilikuwa mwaka 2006, ambavyo vilifuatiwa na utulivu wa miaka mingi. Ghasia zilizuka tena mwaka 2023 baada ya Hamas kuishambulia Israeli Oktoba 7, na kuua watu wapatao 1,200 na kuwakuchua wengine 250 mateka.
Wakati Israel ilipoanza kuishambulia Gaza kwa mabomu, Hezbollah ilianza kurusha makombora katika eneo la kaskazini mwa Israel, ikisema inawaunga mkono Wapalestina. Israel ilijibu kwa mashambulizi ya angani kusini mwa Lebanon, na maelfu ya watu walilazimika kukimbilia pande zote za mpaka.
Mashambulizi ya pager, ulikuwa mwanzo wa kulipuka kwa vita. Siku moja baadaye, walkie-talkies zilizotumiwa na kikundi hicho kwa mawasiliano, pia zililipuka ghafla. Nilikuwa kwenye mazishi ya baadhi ya waathiriwa wa pager wakati mlipuko mkubwa ulipotokea.
Wanachama wa Hezbollah, wakiwa wamekata tamaa, walituomba tuzime kamera au simu zetu, kwani hakuna aliyejua ni kitu gani kingine kingeweza kulipuka.
Wiki zilizofuata, Israel ilifanya mashambulizi ya mabomu bila kuchoka na uvamizi wa ardhini kusini mwa Lebanon. Nchini kote, karibu watu 4,000 waliuawa na karibu wengine 18,000 kujeruhiwa.
Kwa Hezbollah, mzozo ulionekana kuwa mbaya. Viongozi wakuu wa kundi hilo waliuawa, wapiganaji wake wengi waliuawa na sehemu kubwa ya silaha zake kuharibiwa.
Miongoni mwa waliofariki ni Hassan Nasrallah, aliyekuwa mkuu wa Hezbollah kwa zaidi ya miaka 30, aliuawa katika mashambulizi makubwa ya anga kwenye makao makuu ya siri ya kundi hilo chini ya ghorofa huko Dahieh.
Mwishoni mwa Novemba, wakiwa wamepigwa vibaya, kundi hilo lilikubaliana usitishaji wa mapigano ambayo kimsingi ilikuwa ni kama kujisalimisha.
Gharama ya Vita
Kulingana na Benki ya Dunia, gharama za ujenzi wa Lebanon katika maeneo yote yaliyoathiriwa zinakadiriwa kuwa dola za kimarekani bilioni 11 (£8.5bn). Moja ya changamoto kwa Hezbollah ni kutoa msaada wa kifedha kwa watu walioathiriwa na vita, msaada ambao ni muhimu ili kuwaweka wafuasi pamoja nao.
Wale waliopoteza nyumba zao wamepokea dola 12,000 za kulipia kodi ya mwaka mzima. Lakini kundi hilo halijaahidi kutoa pesa za kujenga upya kile kilichoharibiwa au kutoa fidia kwa biashara zilizoharibiwa.
Iran, mfadhili wa Hezbollah, ni mojawapo ya vyanzo vikuu vya fedha, silaha na mafunzo ya kundi hilo. Lakini washirika wa kimataifa wa Lebanon wanataka nchi hiyo kukata msaada wowote wa kifedha kutoka Iran, ili kuweka shinikizo zaidi kwa Hezbollah.
Pia wanasema hakutakuwa na msaada ikiwa serikali ya Lebanon haitachukua hatua dhidi ya Hezbollah. Pamoja na kundi hilo kudhoofika kijeshi, wakosoaji wa Hezbollah wanaona hii fursa ya kipekee ya kulipokonya silaha.
Lakini Alia mwanamke mwenye umri wa miaka 37, na mama wasichana wawili ambaye nyumba yake na biashara yake vimeharibiwa, katika mji wa mpakani wa Kafar Kila, anasema: "Hatutaki msaada wowote unaokuja na masharti kuhusu silaha zetu...Hatutawaruhusu kuchukua utu wetu, heshima yetu, kuchukua silaha zetu kwa ajili tu kujenga nyumba. Tutajenga wenyewe."
Haishangazi kwamba wafuasi wa Hezbollah wanasalia kuwa imara. Kwa wengi, kundi hili ni sehemu ya msingi ya maisha yao, na utambulisho wao. Lakini uwezo wa Hezbollah unaonekana umepungua.
Kabla ya vita, jeshi lake lilikuwa na nguvu zaidi kuliko jeshi la kitaifa la Lebanon. Kambi imara katika bunge. Hilo lina maana hakuna uamuzi mkubwa ambao ulifanyika bungeni bila ridhaa ya Hezbollah.
Kwa sababu ya mfumo wa kisiasa wa Lebanon, kundi hilo lina uwakilishi serikalini. Kwa ufupi, Hezbollah imekuwa na uwezo wa kuidhibiti serikali, na imefanya hivyo mara nyingi.
Lakini vita hivyo vimepunguza nafasi yao. Mwezi Januari, bunge la Lebanon lilimchagua rais mpya, mkuu wa zamani wa jeshi Joseph Aoun, baada ya mvutano wa miaka miwili ambao wakosoaji wanaitupia lawama Hezbollah.
Hapo awali, wabunge wa Hezbollah na washirika wake walikuwa wakitoka nje ya ukumbi wakati wa kura. Lakini baada ya kujeruhiwa vibaya na watu wake wakihitaji msaada, hawawezi tena kuzuia mchakato wa kupatikana rais, ambao ulionekana kuwa muhimu ili kufungua baadhi ya misaada ya kimataifa.
Katika hotuba yake ya kuapishwa, Aoun aliahidi kulifanya jeshi la Lebanon kuwa ndio pekee wenye silaha nchini humo. Hakuitaja Hezbollah, lakini kila mtu alielewa ujumbe huo.
Hatima ya Hezbollah
Huenda mustakabali wa Hezbollah uko mikononi mwa Iran. Moja ya sababu za Iran kuwaunga mkono Hezbollah nchini Lebanon, ilikuwa ni kuzuia shambulio lolote la Israel hasa kwenye vituo vyake vya nyuklia. Hili kwa sasa limeondoka.
Makundi mengine yanayoungwa mkono na Iran katika kanda, sehemu ya kile inachokiita Mhimili wa Upinzani, pia yamedhoofishwa kwa kiasi kikubwa, ikiwa ni pamoja na Hamas huko Gaza na Houthis nchini Yemen.
Na kuanguka kwa utawala wa Assad nchini Syria kumekatiza njia ya ardhini ya Iran ya kuelekea Lebanon - kwa Hezbollah. Hata kama Iran itaamua kuwapa silaha tena Hezbollah, haitakuwa rahisi.
Nasrallah amerithiwa na Naim Qassem, naibu wake wa zamani, ambaye haonekani kuwa mwenye haiba au ushawishi. Mara kwa mara, uvumi huibuka juu ya kuzozana huko ndani.
Kama sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano, Hezbollah ilikubali kuondoa silaha na wapiganaji wake kutoka kusini mwa Lebanon, na afisa wa kidiplomasia wa Magharibi aliniambia kundi hilo limefanya hivyo kwa kiasi kikubwa.
Israel ilitakiwa kuondoa wanajeshi wake, lakini bado wapo, ikisema inahitajika kuziweka salama jumuiya zake za mpakani. Jeshi la Israel pia limefanya mashambulizi ya anga kwenye maeneo linayoyahusisha na Hezbollah. Lebanon inasema uwepo wa Israel katika ardhi ya Lebanon na mashambulizi yake ni ukiukaji wa makubaliano.
Majadiliano kuhusu kupokonywa silaha Hezbollah yanaweza kuwa magumu na marefu. Chanzo kinachofahamu kundi hilo kiliniambia mojawapo ya mjadala juu ya silaha za Hezbollah, kama makombora ya masafa marefu, ni kuwekwa chini ya udhibiti wa serikali, wakati wapiganaji wake, wanaokadiriwa kuwa elfu kadhaa, wanaweza kuunganishwa katika jeshi la Lebanon.
Adam, majeruhi wa pager, sasa amerejea kazini kama muuguzi. Hafanyi tena kazi usiku, kwa kuwa haoni vizuri. Mlipuko huo pia uliacha majeraha kichwani na kifuani. Yeye, kama wengi, bado anaamini katika lengo la kundi na kazi zake.
Imetafsiriwa na Rashid Abdalah