Propaganda za serikali ya Urusi zinazotayarisha watu kufikiria kuwa vita vya nyuklia sio jambo baya

Mamlaka ya Urusi imefunga gazeti lake, lakini mwandishi wa habari Dmitry Muratov anakataa kunyamazishwa.

Tunapokutana huko Moscow, mhariri mkuu wa Gazeti la Novaya na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel ana wasiwasi kuhusu jinsi Kremlin itakavyofikia katika makabiliano yake na nchi za Magharibi.

"Vizazi viwili vimeishi bila tishio la vita vya nyuklia," Muratov ananiambia.

"Lakini kipindi hiki kimekwisha. Je, Putin atabonyeza kitufe cha nyuklia au la? Nani anajua? Hakuna anayejua. Hakuna hata mtu mmoja anayeweza kusema kwa uhakika."

Tangu Urusi ilipoanzisha uvamizi wake kamili nchini Ukraine mnamo Februari 2022, vitisho vya nyuklia kutoka Moscow vimekuwa vikali na vya mara kwa mara.

Maafisa wakuu wametoa vidokezo visivyo wazi kwamba mataifa ya Magharibi yanayoipa Ukraine silaha hayapaswi kuweka shinikizo kubwa kwa Urusi.

Siku chache zilizopita, Rais wa Urusi Vladimir Putin alitangaza mipango ya kupeleka silaha za kinyuklia nchini Belarus.

Kisha mmoja wa wasaidizi wake wa karibu, Nikolai Patrushev, alionya kwamba Urusi ina "silaha ya kipekee ya kisasa inayoweza kuharibu adui yeyote, ikiwa ni pamoja na Marekani."

Ujanja na udanganyifu? Au tishio la kuchukuliwa kwa uzito? Muratov amegundua ishara za kuleta wasiwasi ndani ya Urusi.

Propaganda za Serikali

"Tunaona jinsi propaganda za serikali zinavyotayarisha watu kufikiria kuwa vita vya nyuklia sio jambo baya," anasema.

"Kwenye vituo vya televisheni hapa, vita vya nyuklia na silaha za nyuklia vinakuzwa kana kwamba vinatangaza chakula cha wanyama."

"Wanatangaza: 'Tuna kombora hili, kombora lile, aina nyingine ya kombora.' Wanazungumza kuhusu kulenga Uingereza na Ufaransa, na kusababisha tsunami ya nyuklia kukumba Marekani. Kwa nini wanasema hivyo? Ili watu hapa wajitayarishe."

Hivi majuzi, kwenye runinga ya serikali ya Urusi, mtangazaji maarufu wa kipindi cha mjadala alipendekeza kwamba Urusi "inapaswa kutangaza shabaha zozote za kijeshi kwenye eneo la Ufaransa, Poland na Uingereza."

Mtangazaji huyo huyo pia alipendekeza "kutandaza kisiwa kwa nyuklia za kimkakati na kuzindua majaribio au kurusha nyuklia, ili mtu yeyote asikuwe na matumaini ."

Lakini, propaganda za serikali hapa zinaionyesha Urusi kama nchi ya amani, na Ukraine na Magharibi kama wachokozi. Warusi wengi wanaamini hivyo.

"Watu nchini Urusi wamekasirishwa na propaganda," anasema Muratov. "Propaganda ni aina ya mionzi. Kila mtu anaathiriwa nayo, sio tu Warusi."

"Nchini Urusi, propaganda ni chaneli kumi na mbili za Televisheni, makumi ya maelfu ya magazeti, mitandao ya kijamii kama VK [toleo la Kirusi sawa na Facebook] ambayo hutumikia itikadi ya serikali kikamilifu."

"Lakini vipi ikiwa kesho propaganda itaacha ghafla?" Nauliza. "Ikiwa kila kitu kinakwenda kimya? Warusi wangefikiria nini basi?"

Matumaini kwa Vijana

"Kizazi chetu kipya ni kizuri," Muratov anajibu. "Ana elimu ya kutosha. Takriban Warusi milioni moja wameondoka nchini. Wengi wa wale ambao wamesalia wanapinga kabisa kile kinachotokea Ukraine."

"Wanapinga hali ya kuzimu ambayo Urusi imeunda huko."

"Nina hakika kwamba punde tu propaganda zitakapokoma, kizazi hiki, na kila mtu mwenye akili timamu, atazungumza."

"Tayari wanafanya," Muratov anaendelea. "Kesi 21,000 za makosa ya jinai zimefunguliwa dhidi ya Warusi ambao wameandamana. Upinzani uko jela. Vyombo vya habari vimefungwa."

"Wanaharakati wengi, raia na waandishi wa habari wameitwa mawakala wa kigeni."

"Putin uungwaji mkono? Ndiyo, mkubwa. Lakini hawa ni wazee wanaomwona Putin kama mjukuu wao, kama mtu ambaye atawalinda na kuwaletea pensheni kila mwezi na kuwatakia Heri ya Mwaka Mpya kila mwaka. "

"Watu hawa wanaamini kwamba wajukuu wao wanapaswa kwenda kupigana na kufa," anasema.

Mwaka jana, Muratov alipiga mnada Tuzo yake ya Amani ya Nobel ili kukusanya pesa kwa ajili ya watoto wakimbizi wa Ukraine. Yeye hana matumaini kuhusu siku zijazo.

"Kamwe hakutakuwa tena na uhusiano wa kawaida kati ya watu wa Urusi na Ukraine. Kamwe Ukraine haitaweza kukubali janga hili."

"Nchini Urusi, ukandamizaji wa kisiasa dhidi ya wapinzani wote wa serikali utaendelea," aliongeza.

"Tumaini pekee nililonalo ni katika kizazi kipya, wale watu wanaoona ulimwengu kama rafiki, sio adui na ambao wanataka Urusi ipendwe na Urusi kupenda ulimwengu."

"Natumai kizazi hiki kitakuja baada yangu mimi na Putin," anahitimisha Muratov.