Uchambuzi: Mashtaka 34 ya uhalifu dhidi ya Donald Trump ni yapi?

Wiki iliyopita, tulifahamu kwamba Donald Trump alikuwa ameshtakiwa kwa uhalifu.

Sasa tunajua rais huyo wa zamani wa Marekani anakabiliwa na makosa 34 ya kughushi rekodi za biashara.

Ingawa rekodi za uwongo kwa kawaida huchukuliwa kama makosa madogo, Bw Trump anashutumiwa kwa kutenda makosa ya jinai.

Hiyo inaashiria uhalifu mkubwa zaidi, ambao unaweza kujumuisha kifungo jaji atatoa hukumu hiyo kamili.

"Kimsingi, kesi hii leo ni ya madai kama kesi zetu nyingi," Wakili wa Wilaya ya New York, Alvin Bragg alisema kuhusu mashtaka ambayo ofisi yake imeleta dhidi ya rais huyo wa zamani.

"Madai kwamba kuna mtu alidanganya, tena na tena, ili kulinda maslahi yao na kukwepa sheria ambazo sote tunawajibika.

"Bw Trump - ambaye alikana mashtaka yote - alisisitiza baada ya kutoka nje ya mahakama kwamba hakuna kesi ya kujibu.

"Hakuna kitu kilichofanyika kinyume cha sheria!" alichapisha kwenye tovuti yake ya mtandao wa kijamii.

Hiyo, hata hivyo, itakuwa kwa majaji kuamua. Wakati huo huo, haya ni maelezo ya hatia ya kihistoria ya jinai ya kwanza kabisa ya rais wa zamani.

Mashtaka yote 34 yanahusiana na malipo ya pesa kunyamazisha mtu

Donald Trump anakabiliwa na mashtaka 34 ya uhalifu wa kughushi rekodi za biashara katika mashtaka ya kiwango cha kwanza.

Mashtaka hayo yote yanahusiana na malipo ya dola 130,000 ya wakili Michael Cohen kwa mwigizaji nyota wa filamu za ngono Stormy Daniels kabla ya uchaguzi wa 2016 ili kumzuia asizungumzie madai yake kwamba alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Bw Trump mwaka wa 2007.

Kwenye nyaraka za mahakama, Cohen anajulikana kama ‘Lawyer’ A na Stormy Daniels kama ‘Woman 2’.

Mstari wa kwanza wa Taarifa ya Ukweli, hati iliyoambatana na shtaka, inaelezea kesi ya mashtaka: Mshtakiwa DONALD J. TRUMP alighushi mara kwa mara na kulaghai rekodi za biashara za New York ili kuficha tabia ya uhalifu ambao ulificha taarifa za uharibifu kwa umma uliokuwa unapiga kura wakati wa uchaguzi wa urais 2016.

Madai ya kuficha ukweli dhidi ya Trump yasemekama kutokea alipokuwa rais

Kesi iliyowasilishwa mahakamani New York dhidi ya Bw Trump inategemea jinsi Cohen alivyofidiwa kwa kufanya malipo hayo ya kunyamazisha ukimya.

Mnamo 2017, baada ya kuwa rais, Bw Trump alikutana na Cohen katika Ikulu ya White House.

Muda mfupi baadaye - na kwa muda wa miezi 10 - Bw Trump alianza kutuma hundi kutoka kwa wadhamini wanaoshughulikia mali yake, na baadaye kutoka kwa akaunti yake ya benki binafsi hadi kwa Cohen.

Hundi hizo zilisajiliwa kama "ada za kisheria," lakini Cohen anasema, kwa kweli, zilikuwa malipo ya kunyamazisha ukweli.

Kesi ya upande wa mashtaka inasema: Rekodi za malipo, zilizotunzwa na kudumishwa na Shirika la Trump, zilikuwa rekodi za uwongo za biashara za New York. Ki ukweli, hakukuwa na makubaliano yaliyosalia, na ‘Lawyer A’ hakuwa akilipwa kwa huduma za kisheria zilizotolewa mwaka wa 2017. Mshtakiwa alisababisha rekodi za biashara za mashirika yake kughushiwa ili kuficha tabia yake ya wengine ya uhalifu.

Kutoka kosa la kawaida hadi la jinai

Bw Bragg anadai kuwa Bw Trump alighushi hali halisi ya malipo hayo kwa sababu malipo hayo yalifanywa ili kuunga mkono uhalifu.

Ingawa malipo ya-fedha peke yake si haramu, kutumia pesa kusaidia kampeni ya urais lakini kutoifichua nia kunakiuka sheria ya fedha ya kampeni ya serikali.

Cohen alipatikana na hatia ya ukiukaji kama huo kwa kutofichua malipo yake kwa Bi Daniels.

Kwa kumfidia Cohen kwa kufanya malipo hayo, Bw Bragg anadai, Bw Trump anahusishwa na kitendo hicho cha uhalifu - na inafanya kughushi rekodi ya biashara kuwa kosa kubwa zaidi.

Watetezi wa Bw Trump wanahoji kuwa hiyo ni sehemu ya kisheria, na kwamba hatua hii inachochewa kisiasa.

'Mtindo wa tabia ya uhalifu'

Bw Bragg anataja mifano mingine miwili ya malipo ya kunyamazisha ukimya katika kampeni ya Bw Trump. Malipo haya, anasema, yanaunga mkono kesi ya mashtaka kwamba Bw Trump alijua malipo yake kwa Cohen yalikuwa sehemu ya jaribio haramu la kushawishi uchaguzi wa urais wa 2016.

"Mshtakiwa alipanga njama na wengine ili kushawishi uchaguzi wa urais wa 2016 kwa kutambua na kununua taarifa hasi kumhusu ili kuzuia uchapishaji wake na kunufaisha matarajio ya uchaguzi ya mshtakiwa," Taarifa ya Ukweli ya mashtaka inadai. "Ili kutekeleza mpango huo usio halali, washiriki walikiuka sheria za uchaguzi na kuweka na kusababisha kuongeza taarifa za uongo katika rekodi za biashara za mashirika mbalimbali huko New York."

Katika kisa kimoja, mlinda mlango aliyesema alijua Bw Trump alikuwa na mtoto nje ya ndoa alipokea $30,000. Katika lingine, mwanamke wa pili aliyedai kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Bw Trump alipokea $150,000. Bw Trump amekanusha uhusiano huo.

Malipo haya yalitoka kwa jarida la udaku la National Enquirer na mchapishaji wake wa wakati huo, David Pecker, ambaye Bw Bragg anasema alishirikiana na Bw Trump kunyamazisha habari zinazoweza kuweka wazi ukweli halisi. Kama zawadi, hati ya mashtaka inabainisha, Bw Pecker alipokea mwaliko wa kuapishwa kwa Bw Trump.