Ligi Kuu England: Timu gani itapoteza wachezaji wengi wanaokwenda Afcon?

k

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Bryan Mbeumo wa Manchester United na Arthur Masuaku wa Sunderland wote wanatarajiwa kushiriki Afcon
Muda wa kusoma: Dakika 5

Kombe la Mataifa ya Afrika linaanza mapema kuliko kawaida mwaka huu - huku vilabu 14 vya Ligi Kuu England vikiwa vimeathiriwa na wachezaji wanaoelekea nchini Morocco.

Mashindano hayo yanaanza tarehe 21 Desemba hadi 18 Januari.

Wachezaji wanapaswa kuripoti Jumatatu, Desemba 15 - lakini kocha wa Manchester United Ruben Amorim amesema klabu yake inafanya mazungumzo ili kuruhusu wachezaji wao wa kimataifa wa Afcon kucheza dhidi ya Bournemouth usiku huo.

Wachezaji hao wanaweza kukosa hadi mechi sita, au katika baadhi ya matukio saba, za Ligi Kuu England - pamoja na mechi za Kombe la FA na Kombe la Carabao - ikiwa watafika fainali.

Hatua za makundi zinaisha tarehe 31 Desemba, kwa hivyo timu zitakazoondolewa mapema zitakosa nusu ya mechi hizo.

Sunderland itapoteza wachezaji wengi zaidi kwenye mashindano hayo, huku Arsenal, Aston Villa, Bournemouth, Chelsea, Leeds na Newcastle zikiwa hazina wachezaji wanaokwenda Afcon.

Pia unaweza kusoma

Mchezaji Mmoja

Brighton

Brighton lazima iendelee bila kiungo wa kati wa Cameroon Carlos Baleba, ambaye ameanza karibu kila mechi katika klabu hiyo msimu huu.

Gambia ya Yankuba Minteh haikufuzu.

Crystal Palace

Pigo kubwa kwa Crystal Palace ni kuondoka kwa winga wa Senegal Ismaila Sarr, ambaye amefunga mabao manane katika mashindano yote msimu huu.

Wachezaji watatu ambao hawakuchaguliwa Afcon. Beki wa Morocco Chadi Riad, kiungo wa Mali, Cheick Doucoure na hawajacheza katika klabu tangu Januari kufuatia majeraha makubwa ya goti.

Mshambuliaji Christantus Uche, aliyefunga dhidi ya Shelbourne katika Ligi ya Europa Conference, ni mchezaji wa kimataifa wa Nigeria lakini hakuchaguliwa.

Sarr atakosa robo fainali ya Kombe la Carabao dhidi ya Arsenal Desemba 23.

Liverpool

Liverpool walio katika nafasi ya nane watampoteza mchezaji mmoja tu kwa Afcon.

Mohamed Salah, ambaye amefunga mabao matano hadi sasa katika msimu mgumu, hakika atakuwa kwenye kikosi cha Misri.

Wachezaji Wawili

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Brentford

Brentford itakuwa na wachezaji wawili watakaocheza Afcon - akiwemo mchezaji mmoja wa kikosi cha kwanza.

Dango Ouattara, atachezea Burkina Faso. Mshambuliaji huyo aliyesajiliwa kwa pauni milioni 42.5 amefunga mabao matatu kwa Bees.

Kiungo Frank Onyeka - ambaye amecheza dakika 88 pekee kwenye ligi msimu huu - ataichezea Nigeria.

Wolves

Wolves, walio chini kabisa kwenye Ligi Kuu na bila ushindi, watapoteza wachezaji wawili.

Beki Emmanuel Agbadou anaelekea kuichezea Ivory Coast, huku Tawanda Chirewa wa Zimbabwe, ambaye hajaichezea Wolves msimu huu, naye akiondoka.

Mshambuliaji wa Nigeria Tolu Arokodare hajachaguliwa. Marshall Munetsi wa Zimbabwe pia hakuchaguliwa licha ya kucheza mechi 13 za ligi kuu msimu huu, akifunga bao moja.

Beki wa pembeni wa Cameroon, Jackson Tchatchoua, naye hakutajwa.

Chirewa hajaichezea Wolves msimu huu, lakini wengine wote ni wachezaji wa kawaida wa kikosi cha kwanza.

West Ham

West Ham watapoteza mabeki wao wote wawili wa pembeni kwa wiki chache.

Beki wa kulia Aaron Wan-Bissaka atajiunga na DR Congo na beki wa kushoto El Hadji Malick Diouf yuko kwenye kikosi cha Senegal.

Tottenham Hotspur

Tottenham inatarajiwa kuwa na viungo wawili wa kati wanaokwenda Afcon - Yves Bissouma wa Mali na Pape Matar Sarr wa Senegal.

Bissouma hajaichezea Spurs msimu huu na alifanyiwa upasuaji wa jeraha la kifundo cha mguu mwezi Oktoba.

Nottingham Forest

Nottingham Forest ina wachezaji wawili ambao wataondoka kwenda Afcon.

Kiungo Ibrahim Sangare yuko kwenye kikosi cha Ivory Coast, na mlinzi Willy Boly.

Beki wa pembeni Ola Aina na mshambuliaji Taiwo Awoniyi hawakuchaguliwa na Nigeria. Aina hajacheza tangu alipofanyiwa upasuaji wa misuli ya paja Septemba - na Awoniyi hajawa kwenye kikosi mwaka huu.

Manchester City

City inayofukuzia ubingwa ina wachezaji wawili wanaokwenda Afcon, lakini hakuna hata mmoja wao aliyecheza sana msimu huu kutokana na jeraha.

Mshambuliaji wa Misri Omar Marmoush ameanza michezo miwili ya Ligi Kuu, naye beki wa kushoto wa Algeria Rayan Ait-Nouri akicheza michezo mitatu.

Everton

Everton itawapoteza wachezaji wawili wa kikosi chao cha kwanza, wote ni Senegal - mshambuliaji Iliman Ndiaye mwenye mabao manne na kiungo Idrissa Gueye.

Beki chipukizi Adam Aznou hajajumuishwa katika kikosi cha Morocco tangu alipohamia kutoka Bayern Munich.

Beto ni mchezaji wa kimataifa wa Guinea-Bissau lakini hawakufuzu.

Wachezaji Watatu

Manchester United

Mshambuliaji wa Cameroon Bryan Mbeumo na wachezaji wawili ambao wamecheza kama beki wa kulia - Amad Diallo wa Ivory Coast na Noussair Mazraoui wa Morocco - wote wanaelekea Afcon.

Burnley

Burnley itawakosa wachezaji watatu kwenye mashindano hayo.

Beki wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza chini ya umri wa miaka 21, Axel Tuanzebe, atachezea timu ya DR Congo.

Mshambuliaji Lyle Foster ataiwakilisha Afrika Kusini, huku kiungo mchezeshaji Hannibal Mejbri akiiwakilisha Tunisia.

Fulham

Fulham itashuhudia wachezaji watatu wakijiunga na kikosi cha Nigeria.

Kiungo Alex Iwobi na mlinzi Calvin Bassey wamecheza kila mchezo kwenye ligi msimu huu, huku winga Samuel Chukwueze akionyesha kiwango cha juu katika mechi za hivi karibuni, akifunga mabao mawili dhidi ya Manchester City mwezi Desemba.

Sunderland (6)

Kifurushi cha kushangaza cha msimu huu, Sunderland iliyo nafasi ya nne itakuwa timu iliyoathiriwa zaidi hadi sasa ikiwa na wachezaji sita wanaotarajiwa kuondoka.

Wachezaji hao ni winga wa Morocco Chemsdine Talbi, beki wa Msumbiji Reinild, mshambuliaji wa Burkina Faso Bertrand Traore na wachezaji wawili wa DR Congo Arthur Masuaku na Noah Sadiki.

Kiungo wa kati wa Senegal Habib Diarra pia amechaguliwa, lakini amekuwa nje tangu Septemba kutokana na jeraha.

Winga wa Ivory Coast Simon Adingra na Blondy Nna Noukeu wa Cameroon wote walishindwa kuitwa.

Wengi wao ni wachezaji wa kawaida wa kikosi cha kwanza, huku wakicheza mechi 50 za Ligi Kuu msimu huu.

Mohammed Kudus atapatikana kwa klabu yake kwa sababu Ghana ilishindwa kufuzu.

Ambazo hazitopoteza wachezaji

Aston Villa

Mshambuliaji wa Ivory Coast Evann Guessand ametajwa kama mchezaji wa akiba kwa ajili ya mashindano hayo, kwa hivyo mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 anatarajiwa kwenda Afcon.

Hata hivyo, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 ameanza mechi sita pekee za Ligi Kuu - kwa hivyo Villa itakuwa na uhakika wa kucheza bila yeye ikiwa atakwenda Afcon.

Bournemouth

Bournemouth haitaathiriwa na Afcon. Kiungo mshambuliaji Amine Adli alikosa kujiunga na kikosi cha mwisho cha Morocco. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 ameanza mechi tatu pekee za Ligi Kuu tangu alipowasili msimu huu wa joto.

Kwa bahati nzuri kwa bosi Andoni Iraola, mchezaji wake nyota Antoine Semenyo, Ghana, haikufuzu kushiriki mashindano hayo.

Newcastle

Mshambuliaji wa DR Congo Yoane Wissa, aliyesajiliwa msimu wa joto kutoka Brentford, aliumia goti lake akiwa katika majukumu ya kimataifa mwezi Septemba na akarejea Desemba 6.

Alikosa nafasi ya kuchaguliwa na Congo, ikimaanisha kuwa hawatakuwa na wachezaji kwenye mashindano hayo.