Mzozo wa DRC: Mawaziri wa ulinzi, wakuu wa majeshi SADC kutua DRC

g

Chanzo cha picha, SADC

Maelezo ya picha, Wakuu wa nchi za SADC
Muda wa kusoma: Dakika 3

Na Florian Kaijage

BBC Swahili News Dar es Salaam

Mkutano wa dharura wa wakuu wa nchi za jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika umeagiza kutumwa mara moja kwa mawaziri wa ulinzi na wakuu wa ulinzi kwa nchi zinazochangia wanajeshi nchini DRC, ili kuhakikisha wanajeshi wa ujumbe wa SADC katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (SAMIDRC) wako salama na kuwezesha kuwarejesha nyumbani mara moja wanajeshi waliofariki na wale waliojeruhiwa.

Hilo ni moja ya maazimio yaliyomo katika taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya kikao kilichofanyika Harare, Zimbabwe hapo Ijumaa ili kujadili hali mapigano makali huko mashariki mwa DRC kati ya wapiganaji wa kundi la waasi wa M23 wanaodaiwa kusaidiwa na Rwanda na vikosi vya jeshi la DRC kiasi cha waasi kuudhibiti mji wa Goma makamo makuu ya jimbo la Kivu Kaskazini. Mara kadhaa Rwanda imekuwa ikikanusha madai hayo.

Unaweza pia kusoma:
g

Chanzo cha picha, SADC

Maelezo ya picha, Meja Jenerali Monwabisi DYAKOPU, SAMIDRC alitembelea Kituo Kikuu cha Uendeshaji cha Sake, Masisi ili kusimamia oparesheni na kuwatia moyo wanajeshi walio mstari wa mbele.

Viongozi hao licha ya kutofafanua kuhusu ujumbe wa mawaziri wa Ulinzi na wakuu wa majeshi, wametoa salamu za rambirambi kwa DRC, Malawi, Afrika Kusini, na Tanzania kuhusiana na wanajeshi waliopoteza maisha katika mashambulizi ya hivi karibuni huko Sake, Mashariki mwa DRC, wakiwa chini ya SAMIDRC, na kuwaombea uponaji wa haraka waliojeruhiwa.

Taarifa ilifafanua kuwa wakuu hao wa nchi walipokea ripoti za karibuni zaidi kuhusu hali ya usalama inayoendelea mashariki mwa DRC na kubainisha masikitiko kuhusu mashambulizi ya hivi karibuni ya kundi la M23 na Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) dhidi ya vikosi vya Serikali ya DRC, ujumbe wa SADC katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (SAMIDRC), na raia katika maeneo mbalimbali ya Kivu Kaskazini.

Mkutano huo ulieleza kusikitishwa na hali kwamba mashambulizi ya hivi karibuni yameendelea kuzorotesha hali ya usalama na kibinadamu nchini DRC na kutaka kurejeshwa mara moja kwa huduma muhimu kama vile maji, umeme, njia za mawasiliano na njia za usambazaji wa chakula na bidhaa nyingine muhimu.

Mkutano huo umelaani vikali mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa SAMIDRC yaliyofanywa na M23 wanaoendesha shughuli zao Mashariki mwa DRC kwani vitendo hivyo vilikiuka usitishaji mapigano uliosimamiwa na mchakato wa Luanda tarehe Julai 30, 2024 na kudhoofisha amani na usalama wa DRC na eneo la SADC.

g

Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/Shutterstock

Maelezo ya picha, Wapiganaji wa M23
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Viongozi hao walikumbusha uamuzi wake wa Mei 2023 wa kupeleka ujumbe wa kulinda amani nchini DRC ili kuunga mkono matakwa yake ya amani na usalama na kulinda uadilifu wa eneo lake. Katika suala hili, Mkutano huo ulibainisha kuwa malengo haya bado hayajafikiwa.

Mkutano huo ulisisitiza kuunga mkono juhudi za kidiplomasia za kupata suluhu la amani kwa mzozo wa Mashariki mwa DRC kupitia mchakato wa Luanda, unaoongozwa na João Lourenço, Rais wa Angola na mtetezi mkubwa wa Umoja wa Afrika wa amani na maridhiano barani Afrika na mchakato wa Nairobi, ukiongozwa na Rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta.

Pia ulitolewa wito wa kufanyika kwa Mkutano wa haraka wa pamoja wa wakuu wa nchi za SADC na wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ili kujadiliana kuhusu hali ya usalama nchini DRC kama ilivyopendekezwa na mkutano wa 24 wa wakuu wa nchi za Jumuiya hiyo wa Januari 29, 2025.

Mkutano huo wa kilele umeipa mamlaka Troika, ambacho ni chombo cha SADC kuhusu siasa, ulinzi na ushirikiano wa usalama, kushirikisha pande zote za serikali na zisizo za kiserikali kwenye mzozo, kuhusu mchakato wa kusitisha mapigano ili kulinda Maisha ya watu na kuwezesha mtiririko mzuri wa misaada ya kibinadamu kwa watu na jamii zilizoathiriwa na vita.

Kikao hicho kiliwahimiza viongozi wa kisiasa na kidiplomasia ambao ni wahusika katika mzozo huo kushiriki katika juhudi zilizoratibiwa za mazungumzo, ikiwa ni pamoja na kuunga mkono mchakato wa Luanda, MONUSCO na wengineo, ili kurejesha amani na usalama Mashariki mwa DRC.