Waasi wa DR Congo waapa kuingia hadi mji mkuu Kinshasa

Maelezo ya video, Je chimbuko la vita vya mashariki mwa DRC ni nini?
    • Author, Barbara Plett-Usher & Basillioh Rukanga
    • Nafasi, BBC News
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Kiongozi wa waasi ambaye wapiganaji wake wameuteka Goma, mji mkubwa zaidi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ameapa kuendelea na mashambulizi hadi mji mkuu, Kinshasa.

Corneille Nangaa, ambaye anaongoza muungano wa makundi ya waasi ambayo yanajumuisha M23, alisema lengo lao kuu ni kupindua serikali ya Rais Félix Tshisekedi.

Taarifa ambazo hazijathibitishwa zinasema waasi wanaoungwa mkono na Rwanda kwa sasa wanasonga mbele kuelekea Bukavu, jiji la pili kwa ukubwa katika eneo la mashariki lenye utajiri wa madini, licha ya wito wa kimataifa wa kusitisha mapigano.

Katika hotuba ya televisheni baada ya kuanguka kwa Goma, Tshisekedi alisema "mwitikio wa nguvu na ulioratibiwa" ulikuwa unaendelea ili kutwaa tena eneo kutoka kwa waasi.

"Tunawahakikishia jambo moja: Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo haitaruhusu kufedheheshwa au kupondwa. Tutapigana na tutashinda," alisema Jumatano jioni.

Mapigano hayo yamewalazimu takribani watu 500,000 kuondoka kwenye makazi yao, na kuzidisha hali mbaya ya kibinadamu, kwa mujibu wa UN.

Siku ya Alhamisi, Nangaa aliwatambulisha waasi hao kama wasimamizi wapya wa Goma, akiwaambia waandishi wa habari kwamba ndio wamekita mizizi katika eneo hilo

Tangu mapigano yalipoongezeka wiki iliyopita, umeme na usambazaji wa maji katika jiji hilo umekatika, na chakula ni kichache.

Waasi wamejitangaza kuwa mamlaka mpya ya uongozi huko Goma

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Tutaendeleza maandamano ya ukombozi hadi Kinshasa," Nangaa aliongeza.

Wachambuzi wanasema mashambulizi kama haya yasingewezekana kutokana na ukubwa wa nchi, Kinshasa iko umbali wa kilomita 2,600 (maili 1,600). Hata hivyo, ilitokea mwaka 1997, wakati majeshi yanayoungwa mkono na Rwanda yalipomwondoa madarakani kiongozi wa muda mrefu Mobutu Sese Seko.

Maoni ya Nangaa yataongeza hasira mjini Kinshasa, ambayo imeishutumu nchi jirani ya Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi, na hata kuwa na wanajeshi wake mjini Goma.

Rwanda pia inakabiliwa na upinzani wa kimataifa, licha ya kukanusha uungwaji mkono wa moja kwa moja wa kijeshi.

M23, kundi kuu la waasi katika muungano huo, linaongozwa na Watutsi wa kabila, na linasema lilichukua silaha kulinda haki za kundi la walio wachache nchini DR Congo.

Rais wa Rwanda Paul Kagame pia ni Mtutsi, na anaituhumu serikali ya DR Congo kuwahifadhi wanamgambo wa Kihutu waliohusika katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda.

Maji yamekatwa mjini Goma

Chanzo cha picha, AFP

Umoja wa Mataifa na jumuiya ya kikanda ya kusini mwa Afrika Sadc wana walinda amani mashariki mwa nchi hiyo, lakini walishindwa kuzuia mashambulizi ya waasi.

Walinda amani kutoka kaunti kadhaa wameuawa katika mzozo huo, huku wanajeshi wa Afrika Kusini wakiathirika zaidi ya13.

Siku ya Jumatano, Kagame alisema Rwanda iko tayari kwa makabiliano na Afrika Kusini ikiwa itahitajika, kufuatia madai ya Rais Cyril Ramaphosa kwamba wapiganaji wa M23 na vikosi vya Rwanda ndio waliohusika na vifo hivyo.

Katika taarifa yenye maneno makali kwenye mtandao wa X, Kagame alimshutumu Ramaphosa kwa kupotosha mazungumzo yao ya faragha.

"Ikiwa Afrika Kusini inataka kuchangia katika suluhisho la amani, hilo ni jambo zuri , lakini Afrika Kusini haina nafasi ya kuchukua jukumu la msuluhishi wa amani au mpatanishi. Na kama Afrika Kusini itapendelea mapambano, Rwanda itashughulikia suala hilo katika muktadha huo siku yoyote," alisema.

Kurushiana maneno huko kunaashiria kuongezeka kwa mvutano kati ya mataifa hayo mawili, ambayo uhusiano wake umekuwa dhaifu kwa miaka kadhaa.

Ramani

Viongozi wa nchi za Kusini mwa Afrika wanatarajiwa kufanya mkutano wa kilele siku ya Ijumaa, huku Kagame akisema kikosi chao cha kikanda sio kikosi cha kulinda amani na hakina nafasi katika hili.

Kwa upande mwingine, Tshisekedi alitoa heshima zake kwa wanajeshi wa Sadc waliouawa "wakipigana pamoja nasi", pamoja na walinda amani wa Umoja wa Mataifa.

Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na nchi zikiwemo Marekani na China zote zimetoa wito kwa vikosi vya Rwanda kuondoka DR Congo.

Uingereza na Ujerumani ni miongoni mwa nchi wafadhili ambazo zimetishia kuondoa misaada yao kwa Rwanda kufuatia mashambulizi ya kundi la M23.

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza David Lammy amesema Jumatano kwamba £32m ($40m) za misaada ya kila mwaka ya nchi mbili ziko hatarini, wakati Ujerumani imefuta mazungumzo ya misaada na nchi hiyo.

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga