Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jinsi wanawake hawa vikongwe walivyokabiliana na historia ya ukoloni na kushinda
- Author, Kaine Pieri
- Nafasi, BBC News
- Akiripoti kutoka, London
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Wakati dunia inaadhimisha siku ya wanawake, Machi 8 kila mwaka. wako wanawake wengi wamefanya makubwa katika maisha yao.
Marie-José Loshi aliondolewa na kutenganishwa na familia yake akiwa na umri wa miaka minne, wakati Congo ilipokuwa koloni la Ubelgiji, kusafirishwa umbali wa zaidi ya kilomita 600 na kupelekwa katika kituo cha Kikatoliki cha watoto yatima na kulelewa miongoni mwa watu asio wajua.
"Hatua hiyo iliathiri sana maisha yetu," ajuza ambaye sasa ana umri wa miaka 76 anasema, "tuliporwa utoto na ujana wetu."
Marie-José ni mmoja kati ya maelfu ya watoto ambao walitenganishwa na kimfumo na familia zao na serikali na kuwekwa katika taasisi zinazosimamiwa zaidi na kanisa Katoliki kwa misingi ya asili yao.
"Nilijihisi mpweke, nilikuwa nikilia... nilichukuliwa kwa nguvu kutoka kwa mama yangu na kupelekwa mahali ambapo wale tuliokuwa pamoja hawakuzungumza lugha yangu.
Jambo pekee tulilokuwa nalo sawa ni kwamba sote tulikuwa watoto waliozaliwa kutokana na wazazi wa Kiafrika na Wazungu," Marie-José Loshi anakumbuka.
Miongo kadhaa baadaye, yeye na wanawake wengine wanne waliokulia katika kituo hicho cha Kikatoliki cha watoto wameshinda vita vya kihistoria vya kutaka kulipwa fidia.
Lakini bado wanauguza makovu yaliyotokana na maisha yao ya zamani
Uamuzi wa kihistoria
Monique Bitu Bingi, Léa Tavares Mujinga, Noëlle Verbeken, Simone Ngalula na Marie-José Loshi waliwasilisha kesi yao mahakamani mwaka wa 2021 kuishinikiza serikali ya Ubelgiji kuwalipa fidia kwa madhila waliyopitia utotoni mwao.
Ilikuwa ni kesi ya kwanza nchini Ubelgiji kuangazia maelfu ya watoto waliozaliwa na walowezi wa kizungu na wanawake weusi wa eneo hilo ambao waliondolewa kwa lazima kutoka kwa familia zao katika miaka ya 1940 na 1950.
Mnamo Desemba, Mahakama ya Rufaa ya Brussels ilibatilisha uamuzi wa awali wa mahakama ambayo ilipata muda mwingi ulikuwa umepita kwa wao kustahili kulipwa fidia.
Mahakama ya Rufaa iliamua kwamba hatua za serikali ni uhalifu dhidi ya ubinadamu - "mpango wa kutafuta na kuwateka nyara watoto waliozaliwa na mama mweusi na baba mzungu" - kwa hivyo kuondoa sheria yoyote ya mapungufu.
Majaji walielezea utekaji nyara huo kama "tendo lisilo la kibinadamu la mateso".
"Uamuzi huu ni wa kihistoria. Ni mara ya kwanza kwa mahakama ya Ubelgiji kutambua uhalifu dhidi ya ubinadamu kwa jambo lililotokea wakati wa ukoloni.
Hii inaweka historia -sio tu kwa Ubelgiji, lakini uwezekano kwa mataifa yenye nguvu za kikoloni duniani kote," anasema Michèle Hirsch, mmoja wa mawakili wa wanawake hao watano.
''Uamuzi huo hautambui pekee masaibu ya wanawake hawa watano; pia inatambua uhalifu uliotekelezwa na utawala wa Ubelgiji,'' anasema.
Wanawake hawa walikuwa wanaitisha malipo ya paundi 41,400, kwasababu endapo wangeshindwa kwa kesi hii ingewabidi kufidia serikali ombi lao la mapema.
Lakini kwa Marie-José kesi hii sio kupata fidia.
Sawia na wanawake wengine, kiwewe chake amekifanya siri na kutoelezea watoto na wajukuu wake.
''Tunaishi maisha yaliyojaa soni'' anasema.
''Hatungeweza kusimulia watoto wetu maisha ya fedheha kama hayo. Tunamshukuru wakili wetu, tulipata faraja na ukakamavu wa kutoa ushahidi.''
"Kutengwa kwa utambulisho
Mwaka 2019, serikali ya Ubelgiji iliomba msamaha rasmi kwa takriban waathiriwa 20,000 waliolazimishwa kutengana na familia zao katika taifa kwa sasa inaitwa DRC, pamoja na Burundi na Rwanda.
Sio rahisi kujua idadi kamili ya watoto chotara walioathiriwa na sera ya ukoloni ya Ubelgiji, pamoja na familia ambazo hazijahesabiwa zilizoathiriwa, anasema mwana anthropolojia na mtafiti mkuu katika makavazi ya Ubelgiji katikati mwa Afrika, Dkt. Bambi Ceuppens.
"Nchini Rwanda na Burundi, watoto waliletwa katika shule za bweni kwa utaratibu zaidi kuliko ilivyokuwa Congo," anasema.
Dkt. Ceuppens anasema hii ilitokana na ukubwa wa nchi hizo, kuwa ndogo na zenye watu wachache kuliko wakati huo wa Congo ya Ubelgiji.
Pamoja na kuhamisha watoto ndani kwa ndani, serikali pia ilihamisha watoto hadi Ubelgiji, na mara nyingi kubadilisha majina yao na kutenganisha mandugu kisha kutowapa uraia wa Ubelgiji wanapobaleghe.
Dkt Ceuppens anakumbuka kesi moja iliyohusisha kaka wawili, waliohamishwa nyumbani kwao na kulelewa katika mikoa tofauti ya Ubelgiji mmoja akiwa na uwezo wakuzungumza kiholanzi na mwenzake kifaransa.
Walipofika miaka ya sitini walitafutana na kukutana.
Hii ilikuwa mikakati iliyotekelezwa na mamlaka, kulingana na Dkt.Ceuppens, ikilenga kustawisha utawala wa ukoloni.
''Kupitia mtazamo wa ukoloni, mwanamke mwafrika akijifungua mtoto chotara, ilionekana kama alitelekwa kwa utambulisho.
Kila mtoto chotara alionekana kama ushahidi kwamba ubaguzi wa rangi haungeweza kudumishwa.
Wavulana walionekana kuwa waasi watarajiwa; wasichana kama waliokusudiwa maisha ya ukahaba," anasema.
"Ushindi kwa watu waliotawaliwa na wazungu kote duniani"
Kwa wakili Michèle Hirsch, uamuzi huu wa mahakama una uwezekano wa kesi kama hizi kujitokeza.
''Huu ni ushindi wa watu waliotawaliwa na wazungu kila mahali,'' anasema.
''Waathiriwa wa sera hii ya Ubelgiji, na maelfu waliopitia masaibu kama yale wateja wangu walipitia wanaweza kutafuta haki mahakamani.''
''Pia tunapaswa kutambua kuwa wengi wao wametangulia mbele za haki, lakini wameacha vizazi? Pia kuna kanuni ambayo inaweza kuruhusu vizazi vya waathiriwa kutafuta haki.''
Hirsch ametaka serikali ya Ubelgiji kuidhinisha sheria sawia na ile ya Australia au Canada ya sera za kulipa fidia ambayo waathiriwa wengi wamefidiwa kufuatia watoto wao kutenganishwa na familia zao.
Hirsch pia anasema alihamasishwa na mjadala wa ulipaji fidia nchini Australia na Canada, anaamini kesi hii huenda ikashinikiza Ubelgiji pamoja na wakoloni wa awali kuzindua sera kama hizi.
Lakini anasema hukumu ya kesi hii pia itasaidia sana katika utungaji wa sheria.
Suala la kesi hii ilitajwa ya uhalifu dhidi ya ubinadamu, ikipindua sheria ya mipaka, inamaanisha aina nyingine za uhalifu uliofanywa na serikali za kikoloni pia zinaweza kusababisha fidia, bila kujadili ni miaka mingapi iliyopita zilifanyika.
Unyanyapaa bado unaendelea
Kwa Antoinette Uwonkunda, unyanyapaa hasa baada ya sera za ukoloni bado unashuhudiwa.
Ushirikiano wake, Métis du Monde, (watu chotara kote duniani) iliyoko Ubelgiji na ilianzishwa kusaidia watu ambao ni machotara katika taifa la Rwanda.
Kundi hili husaidia watu chotara na kuwaunganisha na makavazi ambayo wanaweza kufuatilia familia na nasaba zao na pia huchangisha fedha za kufadhili masomo ya wanafunzi.
Uwonkunda anasema moja ya sababu ya kuanzisha kitengo cha Métis du Mondeni kwasababu alishuhudia wakoloni wakitenganisha watoto machotara na familia zao.
"Nilikulia kusini mwa Rwanda karibu na taasisi za katoliki ambazo zilichukua watoto hawa.Nakumbuka nikiskia taarifa namna wazazi walipoteza watoto wao ambao walisafirishwa hadi Ubelgiji na nakumbuka nikijiuliza kwanini ifanyike hivyo?,'' anasema.
Kama vile wanaharakati wengi, Uwonkunda alifurahia aliposikia uamuzi wa mahakama.
''Hili linafaa kuwa funguo, sijali na Ubelgiji haina chaguo bali kuanza kujiuliza maswali yaliyotokea enzi za ukoloni,'' anasema.
''Kuna watu wengi wamepitia madhila sawia kama wanawake hawa na hatutakaa tuzubae hili litupite.''
Kwa Uwonkunda, ambaye ni chotara, kuna mengi yanapaswa kufanywa kwa watu kama yeye hasa wanaoishi mashinani na wanaopitia unyanyapaa.
''Watu huniuliza ninawezaje kuzungumza lugha ya asilia'', kisha anacheka, ''kwahivyo jambo muhimu ambalo huambia watu chotara walioko Rwanda kuwa hili ni taifa lako na unapaswa kuwa huru na kuridhia kuishi.''
Akiongea wiki chache baada ya uamuzi wa mahakama ya Ubelgiji, Marie-José anaunga mkono hatua hiyo.
''Nina tiririkwa na machozi nikisema haya lakini unyanyapaa tuliopitia kwakuwa sisi ni chotara imetufikisha hapa.Hatuhisi tunakubalika, sisi sio waafrika au wazungu, hatuna mahali tunahisi tunatambulika kikamilifu,'' anasema.
''Tunatembea kwakujiamini na siri tuliokuwa tukiificha sasa iko wazi. Watu wakitufanyia dhihaka au wakitushangilia, hatujali.Tulifanya kile tungeweza,kwasababu mzigo uliokuwa umetuandama tumeutua baada ya uamuzi huu.''
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid