Bowen: Iran ilitaka kufanya uharibifu wa kweli wakati huu lakini jibu la Israeli huenda likawa kali

Muda wa kusoma: Dakika 3

Jeremy Bowen

Mhariri wa Kimataifa, BBC News

Iran ilipoishambulia Israel mwezi wa Aprili, ilionekana kana kwamba ilikuwa inajenga hoja - lakini Iran ilitoa taarifa ya shambulio hilo kwa jinsi ilivyotekeleza, na kila kitu kilipigwa risasi kutoka angani na walinzi wa Israel na Marekani.

Wakati huu ni tofauti. Wairani walionekana kuwa na lengo la kutaka kufanya uharibifu mkubwa na walikuwa wakikuchukua hatua kali zaidi.

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran lilitoa tangazo likisema kwamba wanalipiza kisasi mauaji ya viongozi waandamizi wa Hamas na Hezbollah, na kuonya kwamba iwapo Israel italipiza kisasi, nayo itajibu.

Mara ya mwisho, Joe Biden alimwambia Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu - "Kuchukua ushindi", usifanye jibu kubwa - na hawakufanya. Wakati huu huko Israeli hali ni tofauti sana.

Unaweza Pia Kusoma

Tazama ujumbe wa Twitter wa waziri mkuu wa zamani Naftali Bennet jana usiku, akitumia lugha kali sana, akisema: "Hii ni fursa kubwa zaidi katika miaka 50 ya kubadilisha sura ya Mashariki ya Kati." Alikuwa akisema kuwa Israel inapaswa kuvilenga vifaa vya nyuklia vya Iran, ili "kulemaza kabisa utawala huu wa kigaidi".

Sasa yeye si waziri mkuu (ingawa anapendekezwa sana kuwa kiongozi wa baadaye, kwa hiyo alikuwa akitoa hoja ya kuonyesha kuwa yeye ni mgumu) lakini inaonyesha hali fulani katika nchi.

Sitafutilia mbali uwezekano mashambulizi ya Israeli kwa chochote kwa sasa - maeneo ya nyuklia, vifaa vya petroli-kemikali, chochote ambacho kinaweza kusababisha uharibifu kwa uchumi wa Irani.

Hali siku zote ilikuwa kwamba Iran ilikuwa na ulinzi wa mbele katika umbo la Hezbollah huko Lebanon, ikiwa na safu kubwa ya silaha za hali ya juu, za kutumiwa, kwa nadharia, ikiwa Iran na vifaa vyake vya nyuklia vitashambuliwa.

Lakini katika wiki kadhaa zilizopita, Israel imelikata kichwa shirika la Hezbollah, na kuharibu nusu ya silaha zake, kulingana na mamlaka za Marekani na Israel; na kuivamia Lebanoni.

Uzuiaji wa Iran, unaweza kusema haupo tena - umevunjwa vipande elfu moja. Kwa hivyo nadhani Waisraeli wanajisikia huru zaidi kuchukua hatua. Na Joe Biden anahamisha kundi jingine la meli za kivita hadi katika bahari ya Mediterania, akiwaashiria Wairani kwamba ukiipiga Israel, utaipiga Marekani pia.

Hii ndiyo sababu watu walikuwa wakizungumza kuhusu hofu ya vita kuenea: ukosefu wa utulivu, mtikisiko unaotokana na kila kitu ambacho kimekuwa kikitokea - sasa tunaona mengi yakifanyika na inaacha nafasi ndogo sana ya diplomasia kwa wakati huu.

Unaweza Pia Kusoma

Imetafsiriwa na Yusuf Jumah