Je, Marekani inamlenga nani kwa mashambulizi yake nchini Iraq?

Fighters lift flags of Iraq and paramilitary groups, including al-Nujaba and Kataib Hezbollah, during a funeral in Baghdad for five militants killed a day earlier in a US strike in northern Iraq, on 23 December 2023

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kumekuwa na ongezeko la mashambulizi kati ya makundi yanayoungwa mkono na Iran nchini Iraq na Marekani tangu kuanza kwa vita huko Gaza.
    • Author, Feras Kilani na Haider Ahmed
    • Nafasi, BBC Arabic
    • Akiripoti kutoka, Baghdad

Marekani imefanya mashambulizi ya anga kwenye vituo vitatu vya wanajeshi wanaoungwa mkono na Iran nchini Iraq. Ilisema mashambulizi hayo "yalikuwa ni jibu la moja kwa moja kwa mfululizo wa mashambulizi yaliyozidi" dhidi ya vikosi vya Marekani na vya kimataifa nchini Iraq na Syria.

Jibu limekuwa nini?

Serikali ya Iraq imelaani vikali mashambulizi ya Marekani. Msemaji wa Waziri Mkuu wa Iraq Mohammed Shia al-Sudani alisema "yalikiuka wazi" uhuru wa nchi yake. Marekani ilisema mashambulizi yake "sawa" yalilenga "makundi yenye uhusiano na Iran".

Nani alihusika katika mashambulizi kwenye vituo vya Marekani?

Kataib Hezbollah, au Brigedi za Chama cha Mungu, ilikuwa moja ya makundi matatu yaliyohusika katika mashambulizi kwenye kambi za Marekani nchini Iraq na baadaye kulengwa na Marekani. Ni wanamgambo wenye nguvu wa Shia wa Iraq wanaopokea msaada wa kifedha na kijeshi kutoka Iran.

Kundi hili pia linaaminika kuwa na uhusiano mkubwa na Kikosi cha Quds cha Iran, kitengo cha operesheni za ng'ambo cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Nini chimbuko la vurugu?

Makundi yanayoungwa mkono na Iran nchini Iraq yanasema mvutano wa eneo hilo unatokana na vita vya Gaza, kufuatia shambulio la Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba. Iran inaunga mkono Hamas huku Marekani ikiiunga mkono Israel.

Tangu wakati huo, jeshi la Marekani limekuwa likishambuliwa angalau mara 151 nchini Iraq na Syria, Pentagon ya Marekani au Idara ya Ulinzi inasema, kwa kawaida kwa mchanganyiko wa roketi na ndege zisizo na rubani za njia moja.

Marekani ina wanajeshi 2,500 nchini Iraq na 900 katika nchi jirani ya Syria wanaolenga kuzuia kuzuka tena kwa wanamgambo wa Islamic State.

Makundi yanayoungwa mkono na Iran yanasisitiza uamuzi wao wa kushambulia vituo vya Marekani nchini Iraq unafanywa ndani ya nchi, bila ushawishi wowote kutoka Tehran.

Hata hivyo, pia wanasema wanafanya kazi chini ya mwamvuli mmoja nchini Iraq, Syria, na Lebanon, chini ya jina la 'Axis of Resistance'.

Wataalamu wanasema mhimili huu unatumika kama chombo kimojawapo cha shinikizo la Iran katika eneo hili.

People attend the funeral ceremony of the member of Popular Mobilisation Forces (PMF, Hashd al-Shaabi) militia who was allegedly killed in a US airstrike in the Iraqi city of Babylon on 26 December 2023, in Baghdad, Iraq

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wanachama wa Popular Mobilization Forces (PMF), sehemu ya serikali ya Iraq, pia wanauawa katika mashambulizi ya Marekani.

Vipi kuhusu makundi mengine yanayoiunga mkono Iran nchini Iraq ya zamani na ya sasa?

Kubwa zaidi liliwahi kuwa Popular Mobilization Forces (PMF). Iliundwa na wanamgambo wengi wa Shia ambao waliungana kusukuma Islamic State kutoka Iraq.

Awali PMF ilikuwa chombo tofauti na kilionekana kama kinachoiunga mkono Iran, lakini kikawa kitengo cha kijeshi chini ya udhibiti wa jeshi la Iraqi mnamo 2016.

Je, serikali ya Iraq inasemaje?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Serikali ya Iraq inasema mashambulizi ya Marekani yanalenga vituo vyake vya kijeshi na pia kuwaua wanachama wa PMF. Inatoa ulinganisho kati ya hatua za Marekani nchini Iraq na mateso yanayoendelea Gaza.

"Kanda hiyo tayari inakabiliana na hatari ya kuongezeka kwa migogoro, athari za uvamizi wa Gaza, na matokeo ya vita vya kuwaangamiza watu wa Palestina," alisema Meja Jenerali Yehia Rasool, msemaji wa waziri mkuu wa Iraq , katika taarifa.

"Wakati mataifa makubwa, ikiwa ni pamoja na Marekani, yalikaa kimya kuhusiana na uhalifu huu, tunaona Marekani ikiingia kwenye vitendo vya uchokozi vya kulaaniwa na visivyo na msingi dhidi ya ardhi ya Iraq na mamlaka ya kitaifa."

Taarifa za umma kando, nyuma ya pazia, serikali ya Iraq inajaribu kupatanisha na kupunguza mvutano kati ya makundi yanayoungwa mkono na Iran na Washington, lakini haijafanikiwa hadi sasa.

Waziri Mkuu wa Iraq pia anatuma ujumbe mseto kuhusu iwapo Marekani inapaswa kukomesha uwepo wake wa kijeshi nchini Iraq ambako Washington imetuma wanajeshi wake tangu uvamizi wake wa 2003.

Imetafsiriwa na Yusuf Jumah