'Sisi ni nchi ya nyama ya ng'ombe, lakini tunaweza kununua kuku pekee'

Na James Menendez na Alba Morgade

BBC Buenos Aires

Argentina wakati mmoja ilikuwa moja ya nchi tajiri zaidi duniani, tajiri kuliko Ufaransa au Ujerumani, na sehemu kubwa ya utajiri huo ulijengwa kwa mauzo ya nyama ya ng'ombe, hawa Uingereza. Lakini hiyo ilikuwa zaidi ya miaka 100 iliyopita.

Sasa, kutokana na msukosuko mkubwa wa kiuchumi, imekwama katika nafasi ya 70 kiuchumi, kulingana na takwimu za hivi punde kutoka Benki ya Dunia.

Na idade kubwa ya watu hapa hawana uwezo wa kula nyama ya ng'ombe ambao bado wanazurura kwenye nyasi zenye rutuba zinazojulikana kama Pampas. Watu kama Oriana na Samir, wanandoa vijana wenye umri wa miaka 20 na ushee wanaoishi katika kitongoji duni cha mji mkuu Buenos Aires.

"Ni vigumu sana," Oriana anasema. "Unajiuliza mara kwa mara - 'nitaishi vipi?'. Sisi ni nchi ya nyama ya ng'ombe, lakini tunakula kuku tu kwa sababu ni nafuu."

Hata kula kuku ni mara moja moja wakati unataka kujifurahisha. Mwaka jana, mfumuko wa bei ulipanda hadi 211%, kiwango cha juu zaidi katika miongo mitatu. Katika mwezi wa Disemba pekee, bei iliongezeka kwa zaidi ya 25%.

Familia inaishi kwenye nyumba ndogo ya gorofa na binti yao mdogo Chiara, na pia wazazi wa Samir na kaka yake. Kulipa bili ni wasiwasi wa mara kwa mara. Gharama za chakula, na pia kodi, umeme na usafiri zinaendelea kupanda kila wakati.

Samir ni dereva wa usambazaji wa mizigo aliyejiajiri, lakini mzozo wa kiuchumi umewafanya kupunguza mahitaji sana. Mapato yake hayawezi kuendana na mfumuko wa bei.

Zaidi ya hayo, ana wasiwasi juu ya kuongezeka kwa ukosefu wa usalama mitaani, kwani watu wanazidi kukata tamaa. "Wanaweza kukuua kwa ajili ya simu yako tu," anasema.

Angalau 40% ya watu wanaishi katika umaskini, kulingana na takwimu rasmi za hivi punde za serikali. Wengi wanashuku kuwa takwimu halisi ni kubwa zaidi.

Wote wawili Oriana na Samir walimpigia kura kiongozi mpya wa Argentina Javier Milei, mwanasiasa wa chama cha Liberal chenye itikadi kali za kulia mwenye nywele za nyingi, ambaye aliibuka kutoka nyuma katika uchaguzi wa mwaka jana na kushinda kwa zaidi ya 55% ya kura.

"Anaelewa matatizo ya watu," anasema Samir, "Nafikiri yeye ndiye kile Argentina inachohitaji... ili kukabiliana na mfumuko wa bei."

Wengine hawana uhakika sana. Claudio Paez alikuwa mfanyabiashara aliyefanikiwa akiwa na maduka 12 ya bidhaa mbali mbali yakiwemo ya mboga.

Sasa ameshuka hadi mbili tu kwani gharama za uendeshaji wa maduka na kuporomoka kwa mapato ya wateja kulisha katika mapato yake. Na anatarajia mambo kuwa mabaya zaidi, sio bora zaidi.

"Matatizo ya kiuchumi yakiendelea kwa miezi mitatu zaidi, nitakuwa taabani na sitaweza kugharamia safari zangu," anasema.

Watu zaidi na zaidi nchini Ajentina wanalazimika kujiboresha ili kuishi. Sio mbali na duka moja la Claudio, gari dogo limeegeshwa kando ya barabara, buti likiwa limerundikwa juu na trei za mayai.

Bei nafuu, ya $1 (79p) kwa mayai kadhaa, imevutia foleni. Lakini mwenye gari hakawii kwa muda mahali hapa kwa muda kwani polisi wanaweza kumkuta.

Barabara za Buenos Aires bado zinaweza kupambwa kwa usanifu wa kifahari wa maendeleo ya Karne ya 19 nchini humo, lakini pia zimejaa wachuuzi wa mitaani, waendeshaji programu za usafirishaji na teksi zisizo rasmi.

Uchambuzi wa takwimu rasmi za Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Salta unaonyesha kuwa sekta isiyo rasmi inaajiri karibu nusu ya wafanyakazi nchini Argentina.

Kwa kuongezea, watu wachache hulipa ushuru wowote wa mapato kutokana na sheria iliyopitishwa na serikali iliyopita, kabla ya uchaguzi. Na hiyo ni habari mbaya kwa nchi ambayo kimsingi imeporomoka kiuchumi na inahitaji sana kuzalisha mapato.

Argentina inatumia zaidi ya mapato yake, na tayari inadaiwa kiasi kiasi kikubwa cha pesa: kwa sasa, inadaiwa takriban $44bn kwa Shirika la Fedha la Kimataifa, na kuifanya kuwa mdeni mkubwa zaidi wa shirika hilo.

Rais Milei anasema ana majibu ya mzozo wa kiuchumi. Akiwa mchumi mwenye taaluma, yeye ana imani na masoko huria yasiyodhibitiwa na hali duni. Katika kampeni, alipata usikivu mwingi kwa kupinga kile alichokiita ‘’msumeno halisi hewani’’, kuashiria kujitolea kwake katika kupunguza gharama.

Pia aliahidi kufanya mabadiliko katika benki kuu na kuondoa sarafu ya ndani ya nchi - peso - kabisa, na badala yake kuanzisha matumizi ya dola ya Marekani. Mawazo hayo yote mawili kwa sasa yamekwama, si haba kwa sababu serikali yenyewe ina uhaba wa dola.

Badala yake, Rais Milei ameshusha thamani ya peso kwa nusu ili kuongeza ushindani. Na amepunguza idadi ya wizara za serikali kwa kiasi sawa.

Na, pamoja na mapendekezo mengi yanayojulikana kama mswada wa "Omnibus" ambayo kwa sasa ameyapeleka mbele ya Congress, sasa ni zamu ya matumizi ya umma.

"Kwa miaka 30 iliyopita," anasema mchambuzi Sergio Berensztein, "tumekuwa tukichapisha pesa kama wazimu, ndiyo maana tuna mfumuko mkubwa wa bei. Sasa, kwa mara ya kwanza, tuna rais ambaye anaelewa tatizo."

Suluhu pekee, anasema Bw Berensztein, ni kujaribu kusawazisha bajeti, jambo ambalo serikali iliahidi kufanya ifikapo mwisho wa mwaka huu. Lakini itakuwa "mbaya", anaongeza.

Unaweza pia kusoma:

Na hivyo inakuwa suala la siasa. Bw Milei anaweza kuwa na mamlaka ya kibinafsi kutoka kwa wapiga kura, lakini hana wingi wa kura katika Bunge la Congress.

Chama chake, Freedom Advances, kilishinda 15% tu ya viti katika uchaguzi wa wabunge wa 2021. Zaidi ya hayo upo upinzani wenye nguvu katika sura ya vyama vya wafanyakazi nchini humo.

Waliitisha mgomo mkuu wiki iliyopita na kuandaa maandamano makubwa kote nchini. Makumi ya maelfu ya watu waliingia barabarani katika maandamano.

Juan Cruz Díaz kutoka kampuni ya ushauri, Cefeidas Group, ana wasiwasi kuwa athari ya mabadiliko yanayopendekezwa inaweza kuwa mbaya sana. "Wengi wa watu waliompigia kura Javier Milei walitaka mabadiliko," anasema. "Lakini hiyo haimaanishi kuwa wanaunga mkono mbinu hii ya uchumi huria na serikali."

Wiki ijayo, Congress itapiga kura ikiwa itaidhinisha mpango wa rais. Hakuna uhakika kuwa itapitishwa. Na hata hivyo, hakuna hakikisho kwamba hatua zitaleta tofauti yoyote kwa kiwango cha mfumuko wa bei. Na hatimaye, hilo ndilo jambo pekee ambalo ni muhimu kwa watu wengi hapa.

Bw Díaz anaamini kuwa rais ana "miezi michache" tu ya kubadilisha mambo na watu kuanza kujisikia vyema. Huenda fungate ya kisiasa ya Bw Milei ikawa fupi sana.

Unaweza pia kusoma:

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa Yusuf Jumah