Mazishi ya Malkia ni saa ngapi? Nani atavaa sare za kijeshi? Na maswali mengine

Chanzo cha picha, Reuters
Mazishi ya Malkia yatafanyika lini?
Mazishi yatafanyika Jumatatu 19 Septemba saa 7:00 mchana kwa saa za Afrika ashariki. Mazishi yatafanyika Westminster Abbey - kanisa la kihistoria ambapo wafalme na malkia wa Uingereza wanatawazwa.
Mazishi ya serikali ni nini?
Mazishi ya serikali kwa kawaida hufanyika kwa ajili ya mfalme au malkia na hufuata sheria kali za itifaki. Msafara wa kijeshi hubeba jeneza hadi ukumbi wa Westminster, na hufuatiwa na ibada pale Westminster Abbey au Kanisa Kuu la St Paul.
Mara chache, mazishi ya serikali yanaweza pia kufanywa kwa "watu wengine mashuhuri". Watu mashuhuri waliofanyiwa maziko ya aina hii ni pamoja na Sir Isaac Newton, Lord Nelson, Duke wa Wellington na Lord Palmerston.
Mazishi ya mwisho ya kiserikali yalikuwa yale ya Sir Winston Churchill tarehe 30 Januari 1965. Mazishi ya kiserikali ya Mfalme George VI, babake Malkia, yalifanyika tarehe 15 Februari 1952.
Mazishi mengine yaliyoshirikisha mambo mengi ya mazishi ya serikali yalifanyika kwa ajili ya Diana, binti mfalme wa Wales, mwaka wa 1997 na Mama wa Malkia mwaka wa 2002.
Baroness Thatcher alifanyiwa mazishi ya sherehe yenye heshima kamili za kijeshi katika Kanisa Kuu la St Paul mwaka wa 2013.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ninawezaje kutazama mazishi?
Matangazo ya mazishi ya Malkia yatakuwa sehemu ya matangazo yatakayoonyeshwa na BBC pamoja na taarifa zake kwenye tovuti za idhaa mbalimbali za BBC na BBC Radio kwa siku nzima. Mitandao mingine pia inatarajiwa kutangaza tukio hilo, na itaonyeshwa kwenye skrini kubwa katika miji mingi kote Uingereza.
Kina nani wataruhusiwa kuvaa sare za kijeshi?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kasri la Buckingham lilithibitisha kuwa ni washiriki wanaofanya kazi tu kutoka Familia ya Kifalme ambao wana vyeo vya kijeshi ndio watavaa sare wakati wa kuhudhuria matukio matano yaliyoandaliwa kuashiria kifo cha Malkia.
Hii inamaanisha mmoja wa watakaovaa sare hizo za jeshi ni Mfalme Charles. Duke wa Sussex hatafanya hivyo.
Nani mwingine atahudhuria mazishi?

Chanzo cha picha, PA Media
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Viongozi na watu mashuhuri kutoka Uingereza na kote ulimwenguni wataungana na familia ya Kifalme huko Westminster Abbey. Wanachama kadhaa wa familia za kifalme kutoka kote Uulaya - ambao wengi wao walikuwa jamaa wa damu wa Malkia - wanatarajiwa kuhudhuria.
Hao ni pamoja na Mfalme Philippe wa Ubelgiji na Malkia Mathilde, Mfalme Willem-Alexander na Malkia Maxima wa Uholanzi na Mfalme Felipe na Malkia Letizia wa Hispania, pamoja na washiriki wa familia za kifalme za Norway, Uswidi, Denmark na Monaco.
Rais wa Marekani Joe Biden amethibitisha kuhudhuria maziko hayo, kama ilivyo kwa Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese, Waziri Mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern na Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau.
Viongozi wengine wa dunia wanaotarajiwa kushiriki ni pamoja na Mfalme wa Japani Naruhito, Taoiseach Micheal Martin wa Ireland, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier na Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen.
Imeelezwa kuwa rais Xi wa China amealikwa, lakini haijabainika iwapo atahudhuria. Rais wa Urusi Vladimir Putin hajaalikwa, na wala hakuna wawakilishi kutoka Afghanistan, Belarus, Myanmar, Syria au Venezuela.
Malkia atazikwa wapi?

Safari ya mwisho ya jeneza la Malkia itakuwa huko St George's Chapel, kwenye kasri la Windsor Castle. Kutakuwa na huduma ya ya mwisho ya kumuombea itakayowakutanisha wanafamilia ya Kifalme, ambayo pia itaonyeshwa kwenye televisheni. Hii itaisha kwa jeneza kuteremshwa ndani ya Royal Vault. Baadaye mchana, katika ibada ya binafsi, jeneza litazikwa katika kanisa la kumbukumbu la King George VI, ndani ya St George's Chapel.
Je, shule, maduka, baa na biashara zitafungwa?
Haki ya kuwa na likizo sio ya moja kwa moja. Serikali inasema inawahimiza "waajiri kujibu kwa uangalifu maombi kutoka kwa wafanyikazi wanaotaka kuchukua likizo".
Hata hivyo, maduka makubwa na wafanyabiashara kote Uingereza wametangaza kuwa watafunga milango yao kama ishara ya heshima siku ya mazishi yake.
Shule pia zinatarajiwa kusalia kufungwa. Upasuaji na baadhi ya huduma za afya zinaweza kufungwa. Madaktari wengine wa meno hawataonana na wagonjwa, na hospitali zingine zimeghairisha miadi ya kawaida kwa sababu ya kuitumia siku hiyo kutoa heshima.
Walakini, mamlaka zimetahadharisha na kuwamabia wahakikishe wagonjwa wanaweza kupata huduma ya dharura inapohitajika.
Pesa ya Uingereza itabadilika?
Mamlaka hazijasema ni lini itaanza kutolewa sarafu yenye kichwa cha Mfalme Charles III. Noti za benki zilizo na picha za Malkia pia zitaondolewa kidogo kidogo na hatua kwa hatua, lakini noti na sarafu zote zitasalia kuwa halali. Benki ya Uingereza itatoa notisi nyingi kama hilo litabadilika.












