Kwa nini Wafilipino wanafunga ndoa katika makanisa yaliyofurika na maji?
Ilikuwa ni tukio ambalo ungetarajia kuona kwenye harusi.
Jamaika Aguilar, akiwa amemshika babake mkono, alitembea kanisani na kuelekea madhabahuni, akiwa amevalia nguo nyeupe yenye kamba ndefu iliyofanana na fahari ya kanisa la baroque ambako sherehe ilifanyika.
Tofauti pekee kati ya sherehe hii na harusi ya kawaida ilikuwa kwamba bibi harusi na wageni wake wote walikuwa ndani ya maji, kwa sababu baada ya dhoruba na mvua kubwa ya masika, kanisa zima lilifurika.
Lakini wenzi hao hawakuruhusu jambo hilo lizuie ndoa yao, wakisema hali ilikuwa "ngumu, lakini tuliangazia mambo muhimu.
Picha za harusi hiyo katika Kanisa la Baraswain kaskazini mwa Manila, mji mkuu wa Ufilipino, zilisambaa haraka kwenye mitandao ya kijamii, na kuwa mfano mwingine wa ustahimilivu wa Wafilipino katika kukabiliana na maafa.
Lakini cha kufurahisha, hii haikuwa mara ya kwanza kitu kama hiki kutokea. Miaka miwili mapema, wanandoa wengine walitembea kwenye njia iliyofurika na maji ndani ya kanisa moja wakati huo huo wa mwaka. Na mnamo 2018, wanandoa wengine walifunga ndoa katika kanisa lililojaa maji katika mkoa wa Bulacan, kaskazini mwa Manila.
Harusi hizi zilizofanyika ndani ya maji si hadithi tu bali ni mfano wa hivi punde zaidi wa tatizo kubwa la mafuriko linaloendelea kuwakumba mamilioni ya watu, likichochewa na uchakavu wa mifumo ya maji taka, upangaji mbaya wa miji na matukio ya hali ya hewa yanayozidi kuongezeka mara kwa mara.

Chanzo cha picha, Barasoain Church
Harusi, mafuriko na antibiotics
Kwa bibi-harusi huyu mwenye umri wa miaka 27, sehemu ngumu zaidi ya harusi ilikuwa usiku uliopita, wakati alipaswa kuamua ikiwa ataendelea na sherehe au la.
Waandalizi wa harusi walikuwa wamewaonya kuwa mvua ingenyesha zaidi.
"Ulikuwa wakati muhimu zaidi kwetu. Je, tughairi sherehe na kupanga upya? Kwangu ulikuwa uamuzi wa 50/50 na nilikuwa nikifikiria kughairi sherehe hiyo," aliambia BBC.
Lakini mwisho, waliamua kufanya sherehe hiyo.
"Ilikuwa ngumu sana, lakini tuliangazia kile ambacho kilikuwa muhimu sana: uhusiano wetu na watu wanaotupenda," bwana harusi Jade Rick Verdio, 27. Aliongeza kuwa wote walikuwa na "furaha sana" baada ya sherehe.
Moja ya mambo ya kwanza waliyofanya kama wanandoa ilikuwa kununua tembe za doxycycline kutoka kituo cha afya cha eneo hilo na kumeza.
Kidonge hiki ni dawa ya kuzuia magonjwa yanayosababishwa na mafuriko mijini, kama vile homa ya mpunga, ambayo huathiri ini.

Chanzo cha picha, Barasoain Church
Na saa chache tu baada ya sherehe ya harusi, ibada ya mazishi ilifanyika katika kanisa moja lililofurika la Barraswain, huku jeneza jeupe likiwekwa mbele ya madhabahu.

Chanzo cha picha, Barasoain Church
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kimbunga Wifa, kinachojulikana kama Krisin nchini Ufilipino, ni kimbunga cha tatu nchini humo mwaka huu.
Kwa sababu ya eneo la kijiografia la Ufilipino katika Bahari ya Pasifiki, ambapo mifumo hii ya hali ya hewa huunda, nchi hiyo ni mojawapo ya maeneo yaliyo hatarini zaidi duniani kukumbwa na dhoruba za kitropiki.
Karibu dhoruba 20 za kitropiki hutokea katika eneo hilo kila mwaka, nusu ya dhoruba hizo huathiri moja kwa moja nchi.
Watu sita wameripotiwa kupoteza maisha na makumi ya maelfu kuyahama makazi yao kutokana na mafuriko tangu mvua za masika kuanza mwishoni mwa juma lililopita.
Na inaonekana hakuna dalili ya hali ya hewa ya dhoruba kupungua. Vimbunga vingine viwili vinatarajiwa kuikumba Ufilipino baadaye mwezi huu. Vimbunga vikali na hatari zaidi kawaida hupiga mwishoni mwa mwaka, kabla ya Krismasi.
Mafuriko ya sasa yanakuja siku chache kabla ya hotuba ya kila mwaka ya Rais wa Ufilipino Ferdinand Marcos Jr. kwa bunge la Congress siku ya Jumatatu, na mipango yake ya mpango wa kukabiliana na mafuriko wa miaka mingi inatarajiwa kuvuta hisia za umma.
Katika kilele cha mvua kubwa mwanzoni mwa wiki, Marcos alisitisha maandalizi na utangazaji wa hotuba yake baada ya picha za wafanyikazi wa serikali wakiweka mabango yake kwenye nguzo za taa huko Manila kuzua wimbi la hasira ya umma mtandaoni.
Wakosoaji walisema rasilimali za serikali zinapaswa kulenga kushughulikia majanga, sio kutangaza maonyesho ya kisiasa.
Marcos ambaye alikuwa Washington kufanya mazungumzo ya makubaliano ya kibiashara na Rais wa Marekani Donald Trump, alisema amehakikisha mashirika ya kukabiliana na majanga yanaandaliwa kabla ya kuondoka nchini humo.

Chanzo cha picha, Reuters
Ni nini husababisha mafuriko ya mara kwa mara?
Sehemu kubwa ya mafuriko ilionekana katika eneo kubwa la jiji la Manila, lenye idadi ya zaidi ya watu milioni 13.
Manila ni mojawapo ya miji mikuu yenye watu wengi zaidi duniani, na utupaji taka ni changamoto kubwa. Kutokusanywa na kutupwa isivyofaa kwa takataka huchafua njia za maji na kuziba mifumo ya mifereji ya maji.
Kulingana na Manuel Bonoan, katibu wa kazi za umma katika utawala wa Marcos, mafuriko yanasababishwa na mfumo wa maji taka wa Manila uliozeeka na usiotosha", ambao ulianza mwanzoni mwa miaka ya 1900.
Bw. Bonoan alisema kuwa baada ya zaidi ya karne moja ya matumizi, asilimia 70 ya mtandao huo wa maji taka ulifunikwa na udongo na kuzibwa.
Dkt. Mahar Lagmi, mhadhiri wa jiolojia katika Chuo Kikuu cha Ufilipino na mtaalamu wa kukabiliana na majanga, alisema kwenye mitandao ya kijamii kwamba mafuriko hayo kwa kiasi fulani yalisababishwa na ujenzi wa barabara kwenye njia za asili za maji.
Dkt. Lagmi alikuwa amesema hapo awali katika makala kwamba ili kutatua tatizo la mafuriko, mambo mbalimbali lazima yazingatiwe, ikiwa ni pamoja na mawimbi katika Ghuba ya Manila, uwezekano wa dhoruba kuwasili, na uwezekano wa mabwawa ya karibu kuharibika.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla













