Uchaguzi wa Marekani 2024: Harris amvuruga Trump katika mdahalo muhimu

dfc

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Anthony Zurcher
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Donald Trump na Kamala Harris wamekutana kwa mara ya kwanza kwenye jukwaa la mdahalo wa urais huko Philadelphia Jumanne usiku.

Walipeana mikono, lakini sio kwa urafiki.

Katika dakika 90 za patashika, Harris mara kwa mara alimshambulia rais huyo wa zamani kwa mashambulizi binafsi ambayo yalimtoa Trump kwenye mstari.

Harris amezungumzia mwenendo wa Trump wakati wa ghasia za Capitol, na maafisa waliohudumu katika utawala wake ambao wamekuwa wakosoaji wa wazi wa kampeni zake mara kwa mara na kumuacha Trump katika hali ngumu.

Sehemu kubwa ya mdahalo huu, Harris alimuweka mpinzani wake wa chama cha Republican katika mazingira ya kutoa utetezi kuhusu mwenendo na maoni yake ya zamani. Trump akalazimika, kuinua sauti yake mara kwa mara na kutikisa kichwa chake.

“Wamarekani wanapaswa kwenda kwenye mkutano wa Trump,” Harris alisema wakati wa swali la mapema kuhusu uhamiaji. "Watu huanza kuondoka kwenye mikutano mapema kutokana na uchovu na kuchoka," alisema.

Shambulizi hilo ni wazi lilimkera rais huyo wa zamani, kwani alitumia sehemu kubwa ya jibu lake - kwenye mada ya uhamiaji ambayo ni moja ya eneo lake kuu la nguvu - kutetea ukubwa wa mikutano yake na kumdharau mikutano ya Harris.

Trump alikwenda mbali zaidi hadi katika ripoti iliyokanushwa kwamba wahamiaji wa Haiti katika mji wa Springfield, Ohio, walikuwa wakiteka nyara na kula wanyama wa majumbani wa eneo hilo.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Iwapo midahalo ina kushinda na kupoteza, ni mgombea yupi anayetumia vyema masuala ambayo yanampa nguvu - na kutetea hoja au kukwepa maeneo yenye udhaifu kwake - Jumanne usiku ulikuwa ni usiku wa makamu wa rais.

Katika mada za uchumi na utoaji mimba zilipojadiliwa. Uchunguzi wa maoni ya umma unaonyesha Wamarekani wengi hawajafurahishwa na jinsi utawala wa Biden - ambao Harris ni mwanachama muhimu - ulivyoshughulikia mfumuko wa bei na uchumi

Lakini Harris aligeuza mada hiyo na kuzungumzia ushuru uliopendekezwa na Trump, na kuuwita ni “kodi ya mauzo ya Trump” na kisha akaleta mradi wa 2025, mpango huru wenye utata wa utawala wa baadaye wa Republican.

Kama ilivyokuwa huko nyuma, Trump alijitenga na mradi huo na kutetea mpango wake wa ushuru, akibainisha kuwa utawala wa Biden ulikuwa umeweka ushuru mwingi katika muhula wake wa kwanza wa urais. Zilikuwa hoja halali, lakini zilimzuia kumkosoa makamu wa rais juu ya mfumuko wa bei na bei za bidhaa.

Kuhusu uavyaji mimba, Trump alitetea jinsi alivyoshughulikia suala hilo, akisema Wamarekani katika nyanja mbalimbali walitaka sheria ya utoaji mimba ya Roe v Wade ibatilishwe na Mahakama ya Juu - kauli ambayo kura za maoni haziiungi mkono. Alihangaika kueleza msimamo wake na jibu lake wakati fulani lilikuwa la kukurupuka.

Harris, wakati huo huo, alichukua fursa hiyo kutoa kauli ya hisia kwa familia ambazo zimekabiliwa na matatizo ya ujauzito na hazijaweza kupata huduma ya uavyaji mimba katika majimbo ambayo yamepiga marufuku utaratibu huo - majimbo yenye "marufuku ya Trump ya utoaji mimba," kama alivyoyaita Harris.

"Ni matusi kwa wanawake wa Marekani," alihitimisha.

Ulikuwa ni ujumbe uliopangwa kwa uangalifu katika eneo ambalo ana faida kuliko Trump.

Mbinu ya Harris

dcx

Chanzo cha picha, Getty Images

Wakati mdahalo ukiendelea, Harris alimuweka Trump kwenye mashambulizi na kejeli, ambazo angeweza kupuuza lakini inaonekana alilazimika kujibu.

Wakati mmoja, Harris aliulizwa juu ya maoni yake ya uchumi aliyo achana nayo zamani, wakati wa kampeni yake ya urais iliyoshindwa 2019.

Rais wa zamani badala ya kumkosoa makamu wa rais juu ya maoni yake yanayobadilika – kuonesha udhaifu wake wa wazi - alifungua majibu yake kwa kuzungumza juu ya "sehemu ndogo" ya pesa aliyochukua Harris kutoka kwa baba yake.

Kuhusu kujiondoa Afghanistan, eneo jingine dhaifu kwa Harris, makamu wa rais alihamisha mazungumzo na kuyapeleka kwenye mazungumzo ya Trump na maafisa wa Taliban na kuwaalika Camp David. Ilikuwa ni mbinu ambayo ilijirudia na ilionekana kufanya kazi vizuri.

Wa-republican tayari wanalalamika kuhusu kile wanachosema ni upendeleo ambao wasimamizi wa ABC, David Muir na Linsey Davis, waliuonyesha kwa Harris. Wote wawili walimrudisha nyuma Trump na kukagua madai ya uongo aliyoyatoa mara kadhaa.

Mwishowe, hata hivyo, yalikuwa ni majibu ya Trump na shauku ya kuchukua na kula chambo chochote ambacho Harris alikiweka katika mdahalo wa jioni.

Wakati wowote mpinzani wa Harris alipokuwa akizungumza, Harris aliweka sura ya mshangao au kutokuamini. Trump, kwa upande wake, alikuwa na sura ya kukasirika zaidi.

Timu ya kampeni ya Harris ilikuwa haijaamua hapo awali ikiwa itakubali mjadala mwingine. Mara tu baada ya huu kumalizika, waliitisha mjadala wa pili wa urais kabla ya Novemba.

Hiyo pekee inaonyesha jinsi Wana-demokratic walivyoona namna Jumanne usiku ilivyokwenda kwa Harris.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah