Je, mpango wa Trump wa kulifungua tena gereza la Alcatraz utawezekana?

Muda wa kusoma: Dakika 4

Rais wa Marekani Donald Trump ametilia mkazo pendekezo lake la kulifungua tena gereza la Alcatraz, katika kisiwa kidogo katika ghuba ya San Francisco.

Gereza la Alcatraz - maarufu kama "Rock (mwamba)" – limeachwa kutumiwa kama gereza kwa miongo kadhaa sasa. Kwa sasa ni eneo la kihistoria linalotembelewa na mamilioni ya watalii kila mwaka.

Rais wa Marekani anasema anaamini gereza hilo linaweza kutumika tena kuwahifadhi wafungwa hatari, ili kuimarisha sheria na utulivu nchini Marekani.

Historia ya Alcatraz

Lipo kwenye kisiwa kilicho umbali wa maili 1.25 (km 2) kutoka San Francisco, awali Alcatraz ilijengwa kama ngome ya ulinzi ya jeshi la majini, na mwanzoni mwa karne ya 20 ngome hiyo ilijengwa upya na kufanywa kuwa gereza la kijeshi.

Mwaka 1934, lilibadilishwa rasmi kuwa gereza la shirikisho - Gereza la Shirikisho la Alcatraz – na kuwekwa wafungwa mashuhuri akiwemo jambazi Al Capone, Mickey Cohen na George "Machine Gun" Kelly, miongoni mwa wengine.

Gereza hilo lilikuwa miongoni mwa magereza mashuhuri sana nchini Marekani wakati huo, na lilihesabiwa kama gereza usiloweza kutoroka kwa sababu ya mkondo mkali wa maji na baridi kali katika ghuba ya San Francisco.

Gereza hili pia lilifanywa kuwa maarufu kutokana na sinema, ikiwemo sinema ya 1979 maarufu ya Escape from Alcatraz, ambayo inasimulia tukio la kutoroka kwa wafungwa mwaka 1962.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Magereza ya Shirikisho (BOP), gereza hilo lilikuwa na gharama za uendeshaji karibu mara tatu ya gharama za magereza mengine ya serikali. Kwa hiyo lilifungwa na Mwanasheria Mkuu Robert Kennedy mwaka 1963.

Kisiwa hicho na gereza sasa ni eneo la makumbusho linaloendeshwa na National Park Service. Zaidi ya watu milioni 1.4 hutembelea kila mwaka.

Donald Trump sio rais wa kwanza kufikiria kulifungua tena gereza hilo.

Mwaka 1981, Alcatraz kilikuwa ni kimoja kati ya vituo 14 vilivyoorodheswa na utawala wa Reagan kuhifadhi wakimbizi wapatao 20,000 ambao walikimbia kutoka Cuba na kuingia Florida.

Pendekezo hilo la kutumia eneo hilo lilikataliwa kwa sababu ya thamani yake kama eneo la kitalii la kihistoria na kukosekana kwa vifaa vya kutosha.

Trump na Alcatraz

Katika ujumbe wake katika mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, tarehe 4 Mei, Trump alisema kwa mara ya kwanza ameiagiza serikali yake kufungua tena na kupanua matumizi ya gereza hilo, akisema "kwa muda mrefu sana Marekani imekuwa ikikumbwa na wahalifu waovu, wakorofi na wanaorudia kufanya uhalifu."

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House siku iliyofuata, Trump alisema, Alcatraz "inawakilisha sheria na utaratibu."

"Tunahitaji sheria na utulivu katika nchi hii," alisema. "Kwa hiyo tutalitazama gereza hilo. Baadhi ya watu watanya kazi hiyo kwa bidi sana."

Licha ya kusema kuwa anaona ni wazo "zuri", lakini pia alikiri kwamba gereza hilo kwa sasa ni "jumba kubwa" ambalo "limejaa kutu na limeoza."

Mkuu wa uhamiaji wa Trump, Tom Homan, pia aliwaambia waandishi wa habari kwamba Alcatraz linaweza kuwa "chaguo" kwa "ajili ya usalama wa umma na vitisho kwa usalama wa kitaifa."

Linaweza kufunguliwa tena?

Mara tu baada ya maoni ya Trump, msemaji wa idara ya haki Chad Gilmartin alisema katika taarifa kwamba BOP "inafanya kazi kulijenga upya na kulifungua gereza la Alcatraz ili kutumika kuimarisha sheria na utulivu."

Lakini wataalamu na wanahistoria wa magereza wameonyesha mashaka makubwa iwapo mpango huo unawezekana.

"Kusema ukweli, mwanzoni nilifikiri ni mzaha," Hugh Hurwitz, aliyewahi kuwa kaimu mkurugenzi wa BOP kati ya Mei 2018 na Agosti 2019, aliiambia BBC. "Sio rahisi kufikiria kuwa unaweza kulitengeneza. Itabidi ulibomoe na kuanza upya."

Bw Hurwitz alitaja masuala kadhaa kuhusu kituo hicho, ikiwa ni pamoja na majengo ambayo "yanaanguka," na vyumba ambavyo "mtu wa futi sita hawezi kusimama."

"Hakuna kamera. Hakuna uzio," aliongeza.

Jolene Babyak, mwandishi na mwanahistoria wa Alcatraz ambaye aliishi huko akiwa mtoto wakati baba yake akiwa msimamizi wa gereza, anasema:

"Wakati huo, maji taka yote ya watu 500 au zaidi yalitupwa kwenye maji ya ghuba. Siku hizi inabidi yasafirishwe. Sio jambo linalowezekana hata kidogo. Lakini limevutia mawazo ya kila mtu."

Gereza hilo lilipofungwa 1963, BOP ilisema - gharama ya kuendesha gereza hilo ilikuwa ni wastani wa dola 10 na 13 kwa kila mfungwa, ikilinganishwa na gharama ya dola 3 na 5 katika magereza mengine. Sababu kubwa ya gharama hiyo ni chakula na vifaa vilivyohitaji kupelekwa kwa boti.

Katika magereza ya leo ya shirikisho, gharama kwa kila mfungwa ni kati ya dola 120 na 164 - ikimaanisha kwa gharama za leo kuendesha gereza za Alcatraz inaweza kupanda hadi dola 500 kwa kila mtu.

Gereza la Alcatraz linaweza kushikilia wafungwa 340 tu linapojaa.

"Ilikuwa ghali sana kuweka mfungwa huko," anasema John Martini, mwanahistoria ambaye alitumia miaka kadhaa Alcatraz kama mlinzi.

"Kimsingi ni gofu. Hata msingi una matatizo makubwa. Watahitaji maji, umeme, joto, na usafi wa mazingira. Hayo yote kwa sasa hayafanyi kazi."

"Maoni ya Trump ni mkanganyiko mwingine tu katika historia isiyo ya kawaida ya Alcatraz," anasema Martini.