Tunachokijua kuhusu makubaliano ya Israel na Hamas juu ya mateka

    • Author, Yolande Knell & David Gritten
    • Nafasi, BBC NEWS

Israel na Hamas wamefikia makubaliano ya kuachiwa mateka 50 wanaoshikiliwa Gaza katika siku nne za usitishwaji wa mapigano.

Makubaliano hayo pia yanahusisha kuachiliwa huru wanawake na vijana wa Kipalestina 150 wanaoshikiliwa katika jela za Israel na kuongezwa kwa misaada ya kibinadamu kuingia Gaza.

Awali makubaliano hayo yalipaswa kuanza kufanya kazi saa 04:00 asubuhi siku ya Alhamisi, lakini afisa wa ngazi ya juu wa Israel anasema mateka hawataachiliwa hadi ifike Ijumaa.

Rais wa Marekani, Joe Biden alisema makubaliano hayo yatakomesha mateso kwa mateka hao. Pia amesema "itapunguza mateso kwa familia zisizo na hatia za Wapalestina."

Serikali ya Israel iliapa kuendelea na vita vyake vya kuikongoa Hamas na kuwarudisha mateka wengine zaidi ya 200 ambao wanamgambo hao iliwateka nyara wakati wa shambulio la kuvuka mpaka kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba na kuua watu 1,200.

Hamas - inayotambulika kama kundi la kigaidi na Israel, Marekani na mataifa mengine ya Magharibi ilisema - mpango huo utawapa Wapalestina muda wa kupona baada ya mashambulizi makali ya anga na ardhini ya Israel - serikali yake huko Gaza inasema yameua zaidi ya watu 14,000.

Mateka gani wataachiliwa?

Baada ya mazungumzo kuendelea hadi mapema Jumatano asubuhi, serikali ya mseto ya Israel hatimaye ilitia saini makubaliano haya.

Taarifa kutoka ofisi ya Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu ilitangaza wanawake na watoto 50 wataachiliwa kwa muda wa siku nne, wakati mapigano yakiwa yamesitishwa.

Vilevile, ilitoa motisha kwa Hamas kuachilia mateka zaidi, ikisem, "kuachiliwa kwa kila mateka 10 wa ziada - kutapelekea kuongezwa siku moja ya ziada ya kusitisha mapigano."

Kifungu hicho ni muhimu kwa familia za mateka, baadhi yao waliiambia BBC - hawakutaka kuona makubaliano nusu.

Mateka 50 wanaotarajiwa kuachiliwa katika makundi manne ya watu 12, watakuwa raia wa Israel au wenye uraia pacha, na huenda wasiwe raia wa kigeni.

Hakuna orodha ya majina imechapishwa, lakini afisa mkuu wa Marekani aliwaambia waandishi wa habari, raia watatu wa Marekani - akiwemo Avigail Idan mwenye umri wa miaka mitatu, ambaye wazazi wake waliuawa Kibbutz Kfar Aza - watakuwa miongoni mwao.

Afisa mkuu wa Israel alisema Jumanne mchana Hamas huenda pia ikawaachilia bila masharti raia 26 wa Thailand wanaoaminika kuwa miongoni mwa mateka.

Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) imesema iko tayari kusimamia uwachiliwa huo, kama wafanyakazi wake walivyofanya wakati Hamas ilipowaachilia wanawake wawili wenye uraia pacha wa Israel na Marekani na wanawake wengine wawili raia wa Israel.

Vikosi vya Israel vilivyoingia Gaza vilimuokoa mwanajeshi mmoja wa kike na kupata miili ya mateka wengine wawili wa kike - mwanajeshi na raia.

Serikali ya Israel ilisema "itaendeleza vita ili kuwarejesha nyumbani mateka wote, na kuwaondoa Hamas na kuhakikisha hakutakuwa na tishio la kiusalama kwa Israel kutoka Gaza."

Hamas inasema nini?

Taarifa ya Hamas ilitoa maelezo kuhusu makubaliano hayo iliyoyaita "hudna," yaani mapatano ya muda - shughuli zote za ndege zisizo na rubani na ndege za mashambulizi za Israel zitasimama kwa siku nne kusini mwa Gaza.

Lakini upande wa kaskazini - ambao umekuwa lengo kuu la operesheni za Israel za kuisambaratisha Hamas - hali hiyo itadumu kwa masaa kadhaa tu kila siku.

Wanajeshi wa Israel na vifaru wanatarajiwa kusalia katika maeneo yao ndani ya Gaza wakati wa mapumziko ya siku nne, lakini taarifa ya Hamas ilisema vikosi vya Israel havitashambulia au kumkamata mtu yeyote.

Makubaliano hayo yataruhusu malori 200 ya misaada, meli nne za mafuta na malori manne yaliyobeba gesi kuingia Gaza kupitia kivuko cha Rafah cha Misri kwa kila siku nne.

Israel ilikata umeme na maji, na kusitisha usafirishaji wa chakula, mafuta na bidhaa nyingine kwenda Gaza ili kulipiza kisasi shambulio la Hamas.

Imeruhusu mizigo 1,399 ya vifaa vya kibinadamu kuingia Gaza kupitia Misri mwezi uliopita, ikilinganishwa na wastani wa mizigo 10,000 kila mwezi kabla ya vita, kulingana na UN.

Ingawa mpango huo utawaruhusu watu wa Gaza kutoka kaskazini na kwenda kusini, lakini hautaruhusu maelfu ya watu waliokimbia makazi yao kutoka kaskazini kurejea nyumbani.

Wafungwa wa Kipalestina

Hamas inasema makubaliano hayo pia yatawafanya wafungwa 150 wa Kipalestina - wanawake na watoto - kuachiliwa huru na Israel.

Taarifa ya serikal ya Israel haikulitaja hilo, lakini Jumatano asubuhi wizara yake ya sheria ilichapisha orodha kwa Kiebrania ya wafungwa 300 wanaostahili kuachiliwa kama sehemu ya makubaliano hayo - kwa kuzingatia uwezekano kwamba Hamas itakubali kuwaachilia huru mateka 50 zaidi.

Orodha hiyo inajumuisha wavulana 123 wenye umri wa kati ya miaka 14 na 17, msichana mmoja mwenye umri wa miaka 15, wanaume 144 wenye umri wa miaka 18, na wanawake 32 wenye umri kati ya miaka 18 na 59. Wengi wao wamewekwa rumande wakisubiri kusomewa mashtaka ya kurusha mawe na kujaribu kuua.

Sababu ya orodha hiyo kuchapishwa ni kutokana na utaratibu wa kisheria nchini Israeli. Kabla ya kuachiliwa kwa mfungwa yeyote, raia wa Israel lazima waruhusiwe kukata rufaa kwenye Mahakama ya Juu ya Israel.

Israel kwa sasa inawashikilia takribani Wapalestina 7,000 wanaotuhumiwa au kuhukumiwa kwa kuvunja sheria, kulingana na mashirika ya kutetea haki za binaadamu ya Israel na Palestina.

Wapalestina wapatao 3,000 wanaripotiwa kukamatwa katika Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki, ambako ghasia zimeongezeka tangu tarehe 7 Oktoba.

Kauli ya Hamas ilimalizia kwa kusema mpango huo unalenga "kuwatumikia watu wetu na kuimarisha ushupavu wao mbele ya adui."

Pia ilionya, "vidole vyetu vinasalia kwenye kifyatulio, na wapiganaji wetu washindi wataendelea kuwa macho kutetea watu wetu na kushinda uvamizi."

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah