Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tetemeko la ardhi la Uturuki na Syria: 'Jambo baya zaidi ni kuwa daktari katika hali hii'
"Nilipomtazama mtoto huyu machoni niliathirika sana," anasema Dkt Ahmed al-Masri. "Sijui kwanini lakini aliponitazama tu, nilianza kulia."
Ilikuwa zaidi ya saa 30 baada ya tetemeko kubwa la ardhi Jumatatu na alikuwa amechoka.
Yeye na daktari mwingine mmoja tu walikuwa wakiwatibu watu wengi waliojeruhiwa waliokuwa wakiletwa katika hospitali yao huko Afrin, mji unaoshikiliwa na upinzani kaskazini-magharibi mwa Syria.
Kisha, Mohammed mwenye umri wa miaka saba alifika, akiwa emeokolewa kutoka chini ya vifusi vya nyumba yao iliyoporomoka.
Waokoaji walimkuta akiwa amelala kando ya mwili wa baba yake ambaye alikuwa amepondwa hadi kufa pamoja na mama yake na ndugu zake.
"Jinsi yule mvulana alivyokuwa akitutazama, nilihisi kama anatuamini, alijua kuwa sasa yuko kwenye mikono salama," Dkt Masri ananiambia katika mawasiliano ya programu ya Zoom.
"Lakini pia nilihisi ana nguvu nyingi, kana kwamba alikuwa amevumili maumivu ya majeraha yake. Ni nini kinachofanya mtoto wa miaka saba kuwa na nguvu na uvumilivu?"
Dkt Masri ni daktari wa upasuaji mkazi katika Hospitali ya Al-Shifa, ambayo inapata usaidizi wake kutoka kwa Jumuiya ya Madaktari ya Marekani ya Syria (SAMS), shirika la hisani. Anasema ilipokea zaidi ya wagonjwa 200 mara baada ya tetemeko hilo
.Kijana mwingine aliyenusurika na mbaye aliletwa na waokoaji alikuwa mvulana wa miezi 18.
Dkt Masri alimchunguza na kugundua kuwa yuko sawa. Lakini alitambua kwamba wazazi wa mvulana huyo hawakuwa pamoja naye.
“Ghafla nilimuona baba yake akimkimbilia na kumshika huku akilia na kulia,” anasema.
"Baba aliniambia mtoto huyu ndiye pekee aliyenusurika katika familia yake. Wengine wa familia walikuwa wamelazwa kwenye korido, wakiwa wamekufa."
Dkt Masri anasema wafanyakazi katika hospitali hiyo walishangazwa na ukubwa wa janga hilo, huku "mawimbi" ya wagonjwa wakifika wote mara moja.
"Sijawahi kufikiria kuwa tetemeko la ardhi linaweza kusababisha uharibifu mkubwa kama huu, linaweza kusababisha idadi hii ya wagonjwa."
Cha kusikitisha ni kwamba amezoea kushughulikia na matukio makubwa.
Mnamo mwaka wa 2013, alikuwa akifanya kazi katika hospitali ya muda wakati makombora yenye sumu ya neva sarin yalirushwa katika vitongoji kadhaa vinavyoshikiliwa na upinzani vya mji mkuu, Damascus. Mamia ya watu waliuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa.
"Wakati huo, tulifunzwa na kutayarishwa, kama madaktari kwa hafla kama hiyo," Dkt Masri anasema. "Tuliweza kujipanga haraka. Lakini katika hali hii hatukujitayarisha. Hali hii ni mbaya zaidi."
Kufuatia tetemeko la ardhi la Jumatatu, yeye na wenzake huko Afrin walishughulikia wagonjwa ambao walionekana kujeruhiwa kidogo hapo awali.
"Yalikuwa majeraha ambayo unadhani sio makubwa, lakini mtu anahitaji kukatwa kiungo," anasema. "Hatuna uwezo katika hospitali zetu kukabiliana na maafa ya aina hii."
"Jambo baya zaidi ni kuwa daktari katika mazingira haya. Unaposhindwa kuokoa mgonjwa au kupunguza maumivu ya mtu - hilo ndilo jambo baya zaidi unaweza kuhisi."
Alipokuwa akiwatibu wagonjwa, Dkt Masri pia alilazimika kufikiria iwapo familia yake mwenyewe ilikuwa salama kwa sababu usambazaji wa umeme na mtandao vyote vilikuwa hafifu.
Wazazi wake na kaka zake wanaishi umbali wa mita mia chache tu kutoka hospitali, lakini mke wake na watoto wanaishi mpakani katika mji wa kusini mwa Uturuki wa Gaziantep, ambao ulikuwa karibu na kitovu na pia uliathirika vibaya.
"Hisia mbaya zaidi unayoweza kuwa nayo wakati wa machafuko kama haya ni kutojua ikiwa familia yako na wapendwa wako wako sawa."
"Tulikuwa tukiwaangalia wagonjwa kwa macho mawili - moja kutathmini majeraha yao, na lingine kuona ikiwa mgonjwa ni mwanafamilia au la."
Pumzi ya ahueni ilisheheni pale kaka yake alipokimbilia hospitali kumhakikishia Dkt Masri kuwa familia yake yote iko salama. Pia alifanikiwa kupata mapumziko mafupi katika hospitali hiyo.
"Nilipolala wakati huo, nililala sana tu," anasema. "Kuna wakati nilihitaji mtu wa kunishikilia ili niendelee kufanya kazi."
Kisha Dkt Masri aliweza kuondoka kazini na kupata kifungua kinywa na familia yake. Anatumai hatimaye anaweza kusafiri kumwona mke wake na watoto huko Gaziantep.
Anasema pia alikwenda kumtazama Mohammed siku iliyofuata na kumuuliza mtoto huyo wa miaka saba iwapo anamtambua.
"Ndiyo, wewe ndiye daktari uliyeokoa maisha yangu," Mohammed alijibu.