Vita vya Ukraine: Kwa nini Bakhmut ni muhimu kwa Urusi na Ukraine?

Kwa zaidi ya kipindi cha miezi saba , mji huu mdogo wa viwanda mashariki mwa Ukraine umekuwa ukishambuliwa na vikosi vya Urusi.

Kulingana na naibu meya wake, Oleksandr Marchenko, kuna raia elfu chache tu waliobaki wakiishi katika makazi ya chini ya ardhi bila maji, gesi au nguvu za umeme. "Jiji linakaribia kuharibiwa," aliambia BBC. "Hakuna jengo hata moja ambalo halijaguswa katika vita hivi."

Sasa kwa nini Urusi na Ukraine zinapigania mjii huu ulioharibiwa na mabomu?

Kwa nini pande zote mbili zinatoa maisha ya wanajeshi wengi kushambulia na kuulinda mji huu katika vita vilivyodumu kwa muda mrefu kuliko vita vingine vyote katika vita hivi?

Wachambuzi wa kijeshi wanasema Bakhmut ina thamani ndogo ya kimkakati. Sio mji wa ngome au kituo cha usafiri au kituo kikuu cha watu. Kabla ya uvamizi huo, kulikuwa na watu wapatao 70,000 wanaoishi huko. Jiji hilo lilijulikana zaidi kwa migodi yake ya chumvi na jasi na kiwanda kikubwa cha divai. Halina umuhimu wowote wa kijiografia. Kama afisa mmoja wa Magharibi alivyosema, Bakhmut ni "tukio moja dogo la kimbinu katika mstari wa vita wa kilomita 1,200".

Na bado Urusi inapeleka rasilimali kubwa za kijeshi kuuchukua mji huo. Maafisa wa nchi za Magharibi wanakadiria kati ya wanajeshi 20,000 na 30,000 wa Urusi wameuawa au kujeruhiwa hadi sasa ndani na karibu na Bakhmut.

Ukraine imepata hasara kubwa - kama vile mwanajeshi huyu aliyezikwa huko Lviv - katika utetezi wake wa Bakhmut.

Kremlin inahitaji ushindi, wa kuigwa. Ni muda mrefu tangu msimu wa joto wakati vikosi vya Urusi viliteka miji kama Severodonetsk na Lysychansk. Tangu wakati huo faida ilizopata zimekuwa za kuongezeka polepole.

Kwa hivyo Urusi inahitaji mafanikio makubwa ya kujiuza kwa wanaounga mkono Kremlin nyumbani. Serhii Kuzan, mwenyekiti wa Kituo cha Usalama na Ushirikiano cha Ukraine, aliambia BBC: "Wanapigana na misheni ya kisiasa, sio ya kijeshi tu. Warusi wataendelea kutoa maelfu ya maisha ili kufikia malengo yao ya kisiasa."

Makamanda wa Urusi pia wanataka kuichukua Bakhmut kwa sababu za kijeshi. Wanatumai inaweza kuwapa njia ya kupata faida zaidi za kimaeneo. Kama Wizara ya Ulinzi ya Uingereza ilivyosema mwezi Desemba, kuteka jiji hilo "kungeruhusu Urusi kutishia maeneo makubwa ya mijini kama vile Kramatorsk na Sloviansk".

Na kisha kuna swali la kikundi cha mamluki cha Wagner ambacho kiko katikati ya mashambulizi hayo.

Kiongozi wake Yevgeny Prigozhin ameweka hatarini sifa yake, na ile ya jeshi lake la kibinafsi, juu ya kuuteka mji wa Bakhmut. Alitarajia kuonyesha kwamba wapiganaji wake wanaweza kufanya vizuri zaidi kuliko jeshi la kawaida la Urusi. Ameajiri maelfu ya wafungwa na wengi wao wamekuwa chakula cha mizinga ya Ukraine ..

Ikiwa hawezi kufanikiwa hapa, basi ushawishi wake wa kisiasa huko Moscow utapungua. Bw Prigozhin anatofautiana na waziri wa ulinzi wa Urusi, Sergei Shoigu, akikosoa mbinu zake na sasa analalamika kutopata risasi za kutosha. Kuna, Bw Kuzan aliyesema, mapambano ya kisiasa kati ya wanaume hawa wawili ni kutafuta ushawishi wa Kremlin "na mahali pa mapambano lao ni Bakhmut na mazingira yake".

Kwa hivyo kwa nini Ukraine imekuwa ikitetea Bakhmut kwa hali na mali , hatua iliowafanya kupoteza maelfu ya wanajeshi katika mchakato huo?

Kusudi kuu la kimkakati ni kutumia vita kudhoofisha jeshi la Urusi. Afisa mmoja wa nchi za Magharibi aliweka wazi: "Bakhmut, kwa sababu ya mbinu za Kirusi, inaipa Ukraine fursa ya pekee ya kuua Wnajeshi wengi wa Urusi."

Vyanzo vya Nato vinakadiria Warusi watano wanakufa kwa kila Mwanajeshi mmoja wa Ukraine huko Bakhmut. Katibu wa usalama wa taifa wa Ukraine, Oleksiy Danilov, anasema uwiano ni wa juu zaidi kati ya saba hadi moja.

Nambari hizi haziwezekani kuthibitishwa. Serhii Kuzan aliiambia BBC: "Maadamu Bakhmut itatimiza kazi yake, kuturuhusu kukandamiza vikosi vya adui, kuharibu mengi zaidi kuliko vile adui anatupa hasara, hadi wakati huo bila shaka tutaendelea kushikilia Bakhmut. " Kwa kuulinda mji huo, Ukraine pia inavizuia vikosi vya Urusi ambavyo vingeweza kutumwa mahali pengine kwenye mstari wa mbele wa vita.

Kama Urusi, Ukraine pia imeupa mji wa Bakhmut umuhimu mkubwa wa kisiasa. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameufanya mji huo kuwa nembo ya upinzani. Alipotembelea Washington mwezi Desemba, aliiita "ngome ya maadili yetu" na alipeana bendera ya Bakhmut kwa Congress ya Marekani. "Mapigano ya Bakhmut yatabadilisha mwelekeo wa vita vyetu vya uhuru na uhuru," alisema.

Kwa hivyo nini kitatokea iwapo Bakhmut itaanguka?

Urusi ingedai ushindi, kipande adimu cha habari njema ili kuimarisha ari. Ukraine ingepata hasara ya kisiasa. Waukraine hawangeweza tena kulia "Tunaimiliki Bakhmut!" kwenye mitandao ya kijamii. Lakini wachache wanaamini kungekuwa na athari kubwa ya kijeshi. Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin alisema: "Kuanguka kwa Bakhmut hakutamaanisha kwamba Warusi wamebadilisha wimbi la vita hivi."

Mick Ryan, mtaalamu wa mikakati na jenerali wa zamani wa Australia, anaamini hakutakuwa na hatua za haraka za Warusi: "Waukraine… watajiondoa katika maeneo ya ulinzi katika maeneo ya Kramatorsk ambayo wamekuwa na miaka minane kujiandaa. Eneo linaloweza kutetewa kuliko Bakhmut. Mafanikio yoyote katika eneo la Kramatorsk yanaweza kuwa ya umwagaji damu kwa Warusi kama kampeni yake ya Bakhmut."

Kwa hivyo labda kilicho muhimu zaidi katika vita vya Bakhmut ni hasara ngapi kila upande umepata na nini ambacho kinaweza kusaidia katika awamu inayofuata katika vita hivi. Je, Urusi imepata hasara nyingi kiasi kwamba uwezo wake wa kuendeleza mashambulizi zaidi utakuwa umedhoofika? Au Ukraine itakuwa imepoteza askari wengi kiasi kwamba jeshi lake litakuwa na uwezo mdogo wa kuanzisha mashambulizi ya baadaye katika majira ya kuchipua?