Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vita vya Ukraine: Mkuu wa Wagner alishtumu jeshi la Urusi kwa 'usaliti' katika vita vya Bakhmut
Mkuu wa jeshi la kibinafsi la Urusi Wagner anasema kuwa jeshi lake halipati silaha zinazohitajika kutoka Moscow, huku likiwa katika harakati ya kuchukua udhibiti wa mji wa Bakhmut.
Mji huo wa mashariki umeshuhudia mapigano makali ya miezi kadhaa, huku Wagner na wanajeshi wa kawaida wa Urusi wakijaribu kuuteka.
Lakini mkuu wa Wagner Yevgeny Prigozhin anasema ukosefu wa risasi wa jeshi lake unaweza kuwa "urasimu wa kawaida au usaliti".
Rais wa Ukraine na makamanda wa kijeshi wamekubali kuimarisha ulinzi wao dhidi ya Bakhmut.
Urusi imeonekana kudhamiria kuuteka mji huo kwa miezi kadhaa, lakini wachambuzi wengi wanasema imekuwa tuzo ya mfano katika vita na ina thamani ndogo ya kimkakati.
Ushindani unaoonekana kati ya mamluki hao na jeshi la kawaida la Urusi unaonekana kushika kasi katika wiki za hivi karibuni, na hii si mara ya kwanza kwa Bw Prigozhin kuishutumu wizara ya ulinzi ya Urusi kwa kuwanyima risasi inazohitaji.
Katika chapisho la mtandao wa kijamii siku ya Jumapili, Bw Prigozhin alisema hati zilitiwa saini tarehe 22 Februari, huku risasi zikitarajiwa kutumwa kwa Bakhmut siku inayofuata.
Lakini nyingi hazikuwa zimesafirishwa, alisema, kabla ya kusema inaweza kuwa hatua ya makusudi.
Na katika ishara zaidi ya mpasuko huo, Jumatatu Bw Prigozhin alisema mwakilishi wake hakuweza kufikia makao makuu ya kamandi ya kijeshi ya Urusi. Haijulikani ni wapi makao makuu yapo.
Bw Prigozhin alisema ilikuja baada ya kumwandikia mkuu wa "operesheni maalum ya kijeshi" ya Urusi, Valery Gerasimov, kuhusu "umuhimu wa haraka wa kupatiwa risasi".
Kando, katika video iliyopakiwa siku ya Jumamosi - lakini ikionekana kurekodiwa mnamo Februari - Bw Prigozhin alisema watu wake wanahofia kwamba "wanatumiwa" kama kisingizio cha kuadhibiwa iwapo Urusi itashindwa katika vita vyake nchini Ukraine.
"Tukirudi nyuma, tutaingia katika historia kama watu waliochukua hatua kuu ya kushindwa vita," alisema.
"Na hili ndilo tatizo hasaukosefu wa risasi. Haya si maoni yangu, bali ya wapiganaji wa kawaida...
"Itakuwaje iwapo wao [mamlaka ya Urusi] wanataka kututumia , wakisema kwamba sisi ni walaghai - na ndiyo sababu hawatupi risasi, hawatupi silaha, na hawaturuhusu kuajiri wafungwa? "
Katika video ya Jumamosi, Bw Prigozhin pia alisema wanajeshi wa Urusi walio mstari wa mbele watashindwa bila wanajeshi wake
Alisema kwamba wapiganaji wa Wagner walikuwa wakilikabili jeshi zima la Ukrainekwa kuliharibu" na kulinyima nafasi ya kuangazia sehemu zingine za mbele.
Wanajeshi wa Ukraine huenda walirudi nyuma kidogo mashariki mwa Bakhmut, Taasisi ya Utafiti wa Vita (ISW) ilisema Jumatatu.
Lakini iliongeza kuwa Ukraine ilikuwa "inaendelea kusababisha hasara kubwa" kwa vikosi vya Urusi.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema makamanda wa kijeshi wa nchi yake wanaunga mkono kuendelea kwa operesheni za kutetea na kuimarisha nyadhifa huko Bakhmut.
Katika taarifa yake, ofisi ya rais Zelensky ilisema kuwa ilifanya mkutano na Valery Zaluzhny, mkuu wa majeshi ya Ukraine, na Oleksandr Syrsky, kamanda wa vikosi vya ardhini vya nchi hiyo.
Walizungumza "kuunga mkono kuendelea kwa operesheni ya ulinzi na kuimarisha zaidi nafasi zetu huko Bakhmut".
Siku ya Jumamosi, naibu meya wa Bakhmut aliambia BBC kwamba kulikuwa na mapigano mitaani kati ya vikosi vya Urusi na Ukraine.
Hata hivyo Oleksandr Marchenko amesema wanajeshi wa Urusi bado hawajapata udhibiti.
"Hawana lengo la kuokoa jiji... lengo lao pekee ni kuua watu na mauaji ya halaiki ya watu wa Ukraine," Bw Marchenko aliambia kipindi cha Today.