Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Bilionea ahukumiwa kifo kwa ulaghai wa dola bilioni 44 nchini Vietnam
Ilikuwa ni kesi ya kuvutia zaidi kuwahi kutokea nchini Vietnam, ikihusisha mojawapo ya ulaghai mkubwa zaidi wa kibenki ambao Vietnam haijawahi kuona.
Ndani ya ukumbi mzuri wa mahakama ya tangu enzi ya ukoloni katika Jiji la Ho Chi Minh, mfanyabiashara wa Kivietinamu mwenye umri wa miaka 67 alihukumiwa kifo siku ya Alhamisi kwa kuibia pesa katika moja ya benki kubwa zaidi nchini humo kwa kipindi cha miaka 11.
Truong My Lan alipatikana na hatia ya kuchukua dola za Kimarekani bilioni 44 – kama mkopo kutoka benki ya Saigon Commercial. Hukumu hiyo inamtaka arejeshe dola bilioni 27, pesa ambayo waendesha mashitaka wanasema ni ngumu kurejeshwa.
Watu 2,700 waliitwa kutoa ushahidi, huku waendesha mashtaka 10 na mawakili wapatao 200 wakihusika. My Lan ni miongoni mwa wanawake wachache waliohukumiwa kifo katika nchi hiyo.
Ushahidi ulikuwa katika masanduku 104 yenye uzito wa tani sita. Washtakiwa wengine 85 walishtakiwa na Truong My Lan, ambaye alikana kufanya makosa.
Truong My Lan ni nani?
Truong My Lan anatoka katika familia ya Wasino-Vietinamu katika Jiji la Ho Chi Minh. Alianza kama mchuuzi sokoni, akiuza vipodozi na mamake.
Kisha alianza kununua ardhi na mali baada ya Chama cha Kikomunisti kuanzisha kipindi cha mageuzi ya kiuchumi, mwaka 1986. Kufikia miaka ya 1990, alikuwa anamiliki hoteli kubwa na mikahawa.
Kufikia 2011, Truong My Lan alikuwa mfanyabiashara mashuhuri katika Jiji la Ho Chi Minh, na aliruhusiwa kuunganisha benki tatu ndogo, kuwa benki moja kubwa ya Saigon Commercial.
Sheria ya Vietnam inakataza mtu yeyote kumiliki zaidi ya 5% ya hisa katika benki yoyote. Lakini waendesha mashitaka wanasema Truong My Lan anamiliki zaidi ya 90% ya Saigon Commercial.
Walimshutumu kwa kutumia mamlaka yake kuteua watu wake kama wasimamizi, na kisha kuwaamuru waidhinishe mamia ya mikopo kwa makampuni ya kuuza mafuta anayoyadhibiti.
Kulingana na waendesha mashtaka, katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia Februari 2019, aliamuru dereva wake atoe dong trilioni 108 za Kivietinamu, zaidi ya bilioni 4 kutoka benki, na kuzihifadhi katika chumba chake cha chini ya ardhi.
Kiasi hicho cha pesa, zote zikiwa katika noti kuu ya Vietnam, zinakuwa na uzito wa tani mbili.
Pia alishutumiwa kwa kuhonga ili kuhakikisha mikopo yake haichunguzwi. Mmoja wa wale waliohongwa ni mkaguzi mkuu katika benki kuu, alishutumiwa kupokea hongo ya dola milioni 5.
Lakini kwa nini alilaghai kwa muda mrefu? Afisa wa zamani wa Marekani mwenye uzoefu na Vietnam, David Brown anaamini, mwanamke huyo alilindwa na watu mashuhuri ambao wametawala biashara na siasa katika Jiji la Ho Chi Minh kwa miongo kadhaa.
Changamoto kwa Chama Kikuu
Kesi hiyo ilikuwa ya kushangaza zaidi katika kampeni ya kupinga ufisadi iliyoongozwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti, Nguyen Phu Trong.
Trong mwenye itikadi za kihafidhina aliyezama katika nadharia ya Umaksi, alianza kampeni hiyo mwaka 2016 baada ya kushitaka hatamu.
Kampeni hiyo imeshuhudia marais wawili na manaibu waziri mkuu wawili wakilazimishwa kujiuzulu, na mamia ya maafisa kuadhibiwa au kufungwa jela.
Akiwa na umri wa miaka 79, mkuu wa chama cha Kikomunist cha Vietnam, Nguyen Phu Trong yuko katika hali mbaya ya kiafya, na atalazimika kustaafu katika Kongamano lijalo la chama 2026, na kupisha viongozi wapya.
Amekuwa mmoja wa makatibu wakuu waliokaa muda mrefu na mwenye mafanikio makubwa zaidi, akirudisha mamlaka kwa chama katika kiwango ambacho hakijaonekana tangu mageuzi ya miaka ya 1980.
Chini ya uongozi wake chama hicho kimejiwekea malengo makubwa ya kufikia hadhi ya nchi tajiri ifikapo 2045. Hiki ndicho kinachochochea ushirikiano wa karibu zaidi na Marekani.
Hata hivyo ukuaji wa Uchumi nchini Vietnam bila shaka unaenda sambamba na ongezeko la ufisadi. Na kupambana na ufisadi kupita kiasi, kuna hatari ya kuzima shughuli nyingi za kiuchumi.
Tayari kuna malalamiko kwamba urasimu umeongezeka, kwani viongozi wanakwepa maamuzi ambayo yanaweza kuwahusisha katika kesi ya ufisadi.
Le Hong Hiep, wa kituo cha masomo ya Vietnam cha Yusof Ishak huko Singapore anasema, “changamoto ni kuwa, mbinu za kukuza uchumi zimegemea kwenye vitendo vya rushwa kwa muda mrefu. Ufisadi umekuwa grisi iliyofanya mitambo ifanye kazi. Wakisimamisha grisi, mambo yanaweza yasifanye kazi tena."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah