Miradi ya utajiri wa haraka: Hizi ni ishara tano kwamba unatapeliwa

Na The conversation

Get-rich-quick schemes

Chanzo cha picha, shutterstock

Jukwaa la Uchumi Ulimwenguni linaripoti kwamba mzozo wa gharama ya maisha unaathiri watu kote ulimwenguni. Pamoja na kupanda kwa bei ya vyakula na mafuta, inazidi kuwa vigumu kujiweka sawa kifedha. Zaidi ya hayo, mishahara haiendani na mfumuko wa bei, na kufanya kuwa ngumu zaidi kuweka akiba kujenga utajiri.

Ni katika nyakati kama hizo za ugumu wa kiuchumi na kutokuwa na uhakika wa kifedha ambapo walaghai huwavutia watu kuingia kwenye mipango ya "kutajirika kwa haraka", kutoa njia ya kupata pesa kwa urahisi kwa kuwekeza katika fursa za kifedha "zenye faida kubwa".

Matarajio ya kupata pesa kwa urahisi huvutia wengi, na kila mara kunaonekana kuwa na mpango wa "tajiri-haraka" unaozunguka kwenye WhatsApp au kwenye mitandao ya kijamii ambao unaonekana kuwa halali. Lakini ukweli sivyo.

Utafiti wetu umejielekeza kuangalia mifumo ya kifedha katika nchi zinazoibukia kiuchumi, na tunatetea ushirikishwaji wa kifedha na kuwezesha jamii zilizotengwa kupitia ujuzi wa kifedha na mipango ya kifedha. Tunatumia jukwaa letu la kitaaluma kushirikisha ujuzi wetu kuhusu fedha, ikiwa ni pamoja na mitego ya kawaida ya kifedha 'ya ulaghai' ambayo watu wanapaswa kuepuka.

Miradi ya "Tajiri-haraka" ni mmoja wa mitego hiyo. Pia wakati mwingine huitwa ponzi or pyramid schemes kwa lugha ya kigeni. Miradi hiyo ni aina ya ulaghai wa kifedha. Watu wanaoziendesha huchukua pesa kwa njia ya udanganyifu: upotoshaji wa habari na utambulisho. Wanaahidi faida za kifedha ambazo hazipo.

Hii ni biashara ya pesa kwa mtindo wa kupanda na kuvuna. Unaweka pesa kiasi fulani ambacho kidogo baada ya muda fulani labda wiki ama wiki mbili ama mwezi mmoja na kuvuna kiasi kikubwa cha pesa.

Kwa ufupi ni wanakusanya pesa na kurudisha kwa faida kubwa. Ukisikia unaweka dola 50 baada ya wiki mbili unapata dola 100 lazima ukimbilie. Lakini unapaswa kuziepuka kwa sababu, mara nyingi zaidi, ni biashara za uwongo na za ulaghai.

Kumekuwa na miradi mikubwa ya ulaghai katika kipindi cha miaka 30 iliyopita. Mapema miaka ya 1990, MMM Global - mojawapo ya mipango mikubwa na yenye sifa mbaya zaidi ya miradi hii 'ponzi' - iliwalaghai hadi watu milioni 40, ambao walipoteza wastani wa dola bilioni 10. Miradi ya Ponzi tangu wakati huo imeibuka tena kwa aina tofauti nchini Afrika Kusini, Nigeria, Zimbabwe, Kenya, Ghana na nchi zingine kadhaa za Kiafrika.

Kuna ishara tano za simulizi za mpango wa "tajiri-haraka". Jihadharini nao.

1. Mapato au faida kubwa na ya juu zaidi

Get rich

Chanzo cha picha, Shutterstock

Ukiona kwanza, wanatoa mapato yaliyozidishwa na yaliyo juu ya soko lakawaida la fedha ndani ya muda mfupi, ni ahadi ya hatari kidogo.

Kuna sheria au kanuni muhimu mbili za kifedha linapokuja suala la kuwekeza. Ya kwanza ni kwamba inachukua muda kutengeneza pesa au faida. Kukusanya faida tena kubwa ndani ya muda mfupi kunapaswa kuibua maswali kuhusu mpango huo.

Kanuni ya pili ni: Hakuna uwekezaji usio na hatari au unaoweza kuhakikisha faida kubwa. Daima kuna hatari fulani inakuwepo 'risk'. Uwekezaji unaoahidi faida kubwa huwa hatari sana, ambayo huwafukuza watu wengi ambao wasingetamani kukumbana na hatari hiyo kubwa.

2. Wanachama wapya hushawishiwa na kujiunga katika mpango huo kila uchwao

Kwa kawaida, mipango au miradi au biashara za fedha za aina hii hudumishwa kwa kutegemea uwekezaji wa wanachama wapya kuwalipa wanachama waliopo. Mara tu idadi ya wanachama waliopo inapozidi wanachama wapya, mpango huenda "ukatetereka". na unapoteza faida ulizoahidiwa. Mbaya zaidi unapoteza pesa zote ulizowekeza.

Mpango unapoporomoka, haiwezekani kurejesha pesa ulizopoteza kwa sababu umempa mtu asiyemjua kiufundi (kumbuka, ufafanuzi wa ulaghai wa kifedha unajumuisha uwasilishaji mbaya wa utambulisho wa mtu ama mwanachama mwingine).

3. Utaratibu wa kujiunga ni wa harakaharaka na maelezo duni ya jinsi unavyofanya kazi

Get-rich-quick schemes

Chanzo cha picha, BOT

Kuna uharaka wa kujiunga na mpango na hakuna ufafanuzi wa jinsi mpango huo unavyofanya kazi.

Hii ni tabia ya kawaida ya mpango wa "tajiri-haraka". Kwa kawaida hakuna jibu la wazi kuhusu asili ya mpango huo, mipango inawekeza kwenye nini, jinsi gani inazalisha mapato yake au sifa za shirika.

Uwekezaji halali kawaida unakuwa suala lililo wazi na unaweza kuwapa wawekezaji taarifa zote wanazohitaji ili kuwasaidia kuamua kuwekeza ama la. Haishangazi, ukaguzi sahihi wa mipango ya "tajiri-haraka" itafichua asili yao ya ulaghai. Hii ndiyo sababu kila mara kuna uharaka na shuruti ya kufanya ahadi ya haraka ya kifedha kwa kisingizio cha kwamba ni fursa muhimu katika maisha ya kupata utajiri na inakuja mara moja tu.

4. Usajili wake ni wa mashaka

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mamlaka za udhibiti ni muhimu kwa sababu zinafuatilia mienendo ya watoa huduma za kifedha na kuwalinda watumiaji kwa kuzingatia maslahi yao. Ulinzi unaotolewa na wadhibiti wa fedha pia unatia imani katika mifumo ya kifedha.

Mipango ya "Tajiri-haraka" mingi haijasajiliwa na inafanya kazi nje ya mfumo wa mashirika ya udhibiti. Hili huwafanya wawekezaji kuwa katika hatari zaidi ya kupata hasara na hufanya iwe vigumu zaidi kutafuta njia ya kisheria hasara inapotokea.

Kwa mfano nchini Tanzania wengi wa wawekezaji wanalaghaiwa kwa kuonyeshwa namba ya mlipa kodi (TIN) ambayo haimaanishi chochote kuhusu biashara ya utoaji wa fedha au kutambulika kwa kusajiliwa kama Kampuni (BRELA) lakini hiyo haitoshi kwa sababu kuna mamlaka za udhibiti wa masuala ya kifedha na kuwa na leseni inayostahili. Walaghai wengi wanaishia kutoa TIN namba na leseni pengine ya kazi tofauti na wanayofanya.

Uwekezaji halali nchini Afrika Kusini na hata nchi kama Tanzania, Kenya na Uganda, kwa mfano hutolewa na watoa huduma za kifedha walioidhinishwa na kudhibitiwa na Mamlaka ya Maadili ya Sekta ya Fedha. Unaweza kutafuta mtoa huduma yeyote wa kifedha aliyeidhinishwa kwenye tovuti ya mamlaka has akwa nchi kama Afrika Kusini na ukampata.

5. Wanatumia ushuhuda zaidi wa wanachama waliotangulia

Get-rich-quick schemes

Chanzo cha picha, NRB

Hii ni ishara muhimu, mara nyingi ukiona wanatumia shuhuda kutoka kwa wanachama waliopo ambao wamepata pesa nyingi kukuza mpango huo jiulize maswali mara mbilimbili.

Katika hatua za awali, mpango huwa unawalipa wale ambao wamewekeza mapema, na wanachama hawa wanahimizwa kushiriki kutoa shuhuda ama habari za utajiri wao, shuhuda ambazo husambaa sana na kwa haraka ili kukuza mpango huo.

Lakini hii ni mbinu inayotumiwa kujenga imani kwamba wewe pia unaweza kupata mapato makubwa na kutajirika. Miradi hii sio endelevu na haina maadili kwani mtu mmoja anatajirika kupitia kwa mtu mwingine kudanganywa. Mara nyingi wanachama wachache wa mwanzo mwanzo kabisa huneemeka kwa mgongo wa wanachama wengine wapya wanaojiunga.

Mipango mizuri sana kuaminika kabisa

Ukweli ni kwamba utajiri wowote unatokana na mkakati mzuri wa uwekezaji na maamuzi yanayofanywa kwa wakati. Ahadi yoyote ya "kutajirika haraka" inapaswa kushughulikiwa inavyostahili. Hatimaye itafichua asili yake ya ulaghai. Kutambua ishara za mipango ya "tajiri-haraka" kunaweza kukuokoa kutokana na shida ya kifedha isiyo ya lazima.

Daima ni wazo nzuri kufanya uchunguzi wako mwenyewe kabla ya kuweka fedha zako katika uwekezaji wowote. Jaribu kutafuta taarifa sahihi kutoka kwenye mamlaka za udhibiti kuona uhalali wake. Usijiingize tu bila kujua uhalali na uhakika wa fedha zako unazowekeza.