Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uchaguzi wa DR Congo:‘Kama ungekuwa uamuzi wetu, tungepiga kura kupata amani’
Na Mercy Juma akiwa Goma & Samba Cyuzuzo akiwa Nairobi
Baada ya waasi waliokuwa na silaha nzito kuzunguka kijiji chake kidogo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Musa Bi alitembea kwa miguu kwa siku saba na watoto wadogo sita hadi alipofika katika kambi ya wakimbizi inayosimamiwa na Umoja wa Mataifa.
Akiwa na umri wa miaka 42 amejawa na wasiwasi, kwa kutojua hatima ya mumewe na watoto wengine wawili, kwani familia ilitengana katika ghasia zilizofuatiwa na kusonga mbele kwa waasi wa M23.
Hafikirii sana kuhusu uchaguzi wa urais wa tarehe 20 Disemba - na wakati mzozo unaotokea karibu naye unatawala kampeni, hakutakuwa na upigaji kura katika maeneo kadhaa ya jimbo la Kivu Kaskazini anakoishi kwa sababu ya ghasia zinazoendelea huko.
"M23 walikuja. Walikuwa wakipigana na askari wetu [wa serikali]. Tulianza kukimbia na wale ambao hawakuweza kukimbia, waliuawa," anaieleza BBC.
Baada ya kubahatika kunusurika , Bi na watoto wake walilala katika vijiji vingine hadi walipofika kwenye kambi ya Bushagala na kwa mara nyingine tena walilazimika kulala nje mahali pa wazi, mara nyingi kwenye mvua.
Wakati BBC ilipokutana nao, walikuwa kwenye kambi iliyopo chini ya Mlima wa volkano wa Nyiragongo kwa siku ya sita, wakisubiri shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi kuwasajili ili wapate hema - na kuweza kupata mgao wa chakula.
Lakini shirika hilo limelemewa na wimbi la wakimbizi wa ndani - ambao ni kati 700 na 1,000 kila siku - kiasi kwamba Bi Bi anasubiri zamu yake kwa subira, huku akitegemea kuwa wale ambao tayari wamejiandikisha chakula chao - ambacho kawaida hutengenezwa kwa unga wa mtama na ulezi - watamgawia pia yeye na wanae wadogo.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa karibu watu milioni saba ni wakimbizi wa ndani nchini DRC, idadi ambayo ni kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa .
Hata hivyo katika kijiji cha Bi karibu na mji wa Masisi, familia yake ilijitosheleza, ikilima chakula katika shamba lao - hadi walipofukuzwa na M23, ambao wako kwenye mashambulizi tena huku kukiwa na mpango wa kikanda wa kusitisha mapigano.
Wapiganaji hao, ambao awali walikuwa waasi wa jeshi la Congo, wanaishutumu serikali kwa kuwatenga watutsi walio wachache nchini humo na kukataa kufanya mazungumzo nao. Wanaichukulia milima inayozunguka eneo la Masisi kama ardhi yao ya asili.
Rais Félix Tshisekedi, ambaye anawania muhula wa pili wa miaka mitano, amekuwa akichochea chuki za utaifa kwa kuwafanya waasi kuwa mstari wa mbele kwa kile anachokiita "malengo ya kujitanua" ya nchi jirani ya Rwanda - na hadi kufikia kiwango cha kumlinganisha rais wa Rwanda na Kiongozi wa Vita vya Pili vya Dunia wa Ujerumani.
"Nitazungumza na Rais wa Rwanda Paul Kagame na kumwambia hivi: kwa kuwa alitaka kuishi kama Adolf Hitler kwa kuwa na malengo ya kupanua maeneo ya nchi yake, ninaahidi ataishia kama Adolf Hitler," Bw Tshisekedi alisema kwenye mkutano wa uchaguzi mashariki mwa nchi hiyo. Ijumaa.
"Hata hivyo, [amekutana] na mtu ambaye amedhamiria kumzuia na kulinda nchi yake."
Bw Kagame hajajibu, lakini msemaji wa serikali ya Rwanda alisema maoni kama hayo ni "tisho kubwa na la wazi".
Rwanda daima imekuwa ikikanusha kuwaunga mkono wapiganaji wa M23, lakini kwa miaka mingi imekuwa ikikosoa mamlaka ya Congo kwa kushindwa kuwapokonya silaha waasi wa kabila la Kihutu - ambao baadhi yao wanahusishwa na mauaji ya kimbari ya Rwanda mwaka 1994.
Mamia ya wanamgambo wanaongezeka katika eneo hilo lenye utajiri wa madini, ambapo jeshi limeshindwa kudhibiti usalama kwa miongo mitatu iliyopita. Makundi yote yenye silaha yanatazama faida kwani madini yanayochimbwa huishia kwenye bidhaa kama vile simu za rununu, magari, ndege na vito.
Katika ishara zaidi ya hamasa ya uzalendo kabla ya uchaguzi, Bw Tshisekedi amekiondoa kikosi cha kulinda amani cha Afrika Mashariki - takriban mwaka mmoja baada ya kukikaribisha.
Hapo awali aliamuru kuondolewa kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa, unaojulikana kwa kifupi Monusco, ambao uliwapeleka wafanyakazi wake 17,000, wakiwemo askari 12,000.
Hii haishangazi kamanda wa wanajeshi wa Umoja wa Mataifa, ambaye anakiri kwamba wameshindwa kuwalinda watu kama Bi Bi dhidi ya waasi.
"Watu wanaposema Monusco haikuwa ikifanya kazi yao wakati mwingine, hawana makosa, lazima tukubali hilo," anasema Luteni Jenerali Otávio Rodrigues de Miranda Filho wa Brazil.
"Changamoto kubwa nilipofika hapa ilikuwa kubadili mawazo ya askari wangu. Kuwapa motisha na kuwafanya waelewe kwamba tunapaswa kuwa makini na kuwa na ufanisi zaidi. Vinginevyo tunapoteza imani ya watu."
Bw Tshisekedi amechanganyikiwa kwamba hakuna iliyoweza kikosi kilichoweza kudhibiti waasi wa M23, aambao sasa wako kilomita 35 tu kutoka Goma, jiji kuu la mashariki lenye wakazi wapatao milioni moja lililopo karibu na Mlima Nyiragongo.
Hii imeongeza matarajio ya Goma kuishia mikononi mwa waasi, kama ambapo walichukua udhibiti wake miaka kumi iliyopita. Hii ilitoa mwanya kwa makubaliano ya amani ya kikanda na kuundwa kwa kikosi cha uingiliaji kati cha Umoja wa Mataifa, kinachoundwa na askari kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc), ili kuwashinda M23 na kuwapokonya silaha.
Wapiganaji hao hatimaye walihamia katika kambi, hasa nchini Uganda. Walianza kujipanga upya miaka miwili iliyopita chini ya milima inayopakana na Rwanda na Uganda - maarufu duniani kwa sokwe na volcano - baada ya malalamiko kwamba mpango huo haukutekelezwa.
Kuchukuliwa na waasi kwa kijiji cha Bi - na mji wa karibu wa Masisi - kunaonyesha nguvu mpya ya waasi.
Huku jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo likiwa halina nafasi ya kupigana peke yake, Bw Tshisekedi anaona Sadc kama dau lake bora zaidi, na ameomba kundi la eneo hilo msaada, kutokana na mafanikio ya awali ya wanajeshi wao.
Umoja huo wenye wanachama 16 - unaojumuisha Afrika Kusini, Tanzania na Angola - umekubali kutuma wanajeshi kama sehemu ya kikosi tofauti cha nguvu, ingawa maelezo ni ya kizungumkuti na haijulikani lini itawasili.
Uamuzi wa Bw Tshisekedi kuamuru kikosi cha Umoja wa Mataifa kuondoka kinafuatia maandamano kadhaa makubwa dhidi yake mjini Goma kutokana na kushindwa kuwarudisha nyuma waasi wa M23.
Lakini baadhi ya watu ambao BBC ilizungumza nao walisema kujiondoa kwao kutawaacha bila ulinzi hata kidogo.
"Wakati wowote waasi wanaposhambulia vijiji na mashamba yetu, tunakimbilia kwenye vituo vya Monusco , kwa ajili ya ulinzi," anasema Elizabeth Ssebazungu kutoka kambi ya Shasha karibu kilomita 30 magharibi mwa Goma.
Hata hivyo, kuondoka kwao hakutakuwa mara moja na kutafanyika kwa awamu, ikiwezekana kwa miaka kadhaa.
Mnamo mwezi wa Januari, wanajeshi wa Pakistan wataanza kuondoka katika jimbo la Kivu Kusini, jambo ambalo linapaswa kuchukua miezi minne.
"Hakuna muda uliowekwa wa awamu ya pili na ya tatu, hadi sasa. Serikali ilituomba kuweka ratiba wazi," Jenerali Otávio anasema.
Hili ni jambo ambalo watu wengi wa eneo hilo hawatambui, hasa kutokana na jinsi wanasiasa wanaofanya kampeni za uchaguzi wanavyoendesha wimbi la chuki dhidi ya Umoja wa Mataifa.
Kwa Bi hafikirii kuhusu uchaguzi , wakati masaibu yao yakiendelea kupuuzwa - licha ya ahadi za uchaguzi.
Maoni yake Bi Bi yanaungwa mkono na wakimbizi wengine katika kambi ya Bushagala, akiwemo Uzima Sadro, ambaye hivi karibuni shamba lake ambalo lilichukuliwa na waasi wa M23.
"Mapambano yetu si mapya. Ni yale yale, mabaya zaidi," anasema.
"Kwa kweli wanasiasa hawatujali na wameshindwa kuleta amani, jambo ambalo sisi ndilo tunalolitaka."
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Yusuf Jumah