Mfumo wa Urusi wa S-400: Marekani yaikataza Uturuki kuununua lakini yairuhusu India.. kwanini?

Wiki iliyopita, Baraza la Wawakilishi la Marekani lilipitisha marekebisho ya sheria inayoipa India kibali maalum cha kununua mifumo ya ulinzi kutoka Urusi. Chini ya masharti makali ya sheria hii iitwayo 'Counting America's Adversaries Through Sanctions Act' au 'CAATSA', ununuzi wa vifaa vya ulinzi kutoka Urusi, Iran na Korea Kaskazini umepigwa marufuku.

Ingawa saini ya Rais wa Marekani bado itahitajika kutekeleza ruhusa hii maalum kwa India kuwa sheria, hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa inaiondoa India dhidi ya vikwazo, haswa kwa kununua mfumo wa ulinzi wa makombora wa S-400 kutoka Urusi.

S-400 ni mfumo wa hali ya juu wa ulinzi wa kombora kutoka ardhini hadi angani uliotengenezwa na Urusi.

India ilinunua mfumo huu wa ulinzi kutoka Urusi mnamo 2018 kwa $ 5 bilioni na tangu wakati huo kulikuwa na uvumi kwamba Marekani inaweza kuiwekea vikwazo India chini ya CAATSA.

Chini ya sheria hiyo hiyo, Marekani ilipiga marufuku mshirika wake wa NATO Uturuki kununua mfumo huo wa S-400.

Lakini ni kwanini Marekani iliiruhusu India kununua silaha hiyo?

Wachambuzi wanaita makubaliano hayo kuwa ishara muhimu ya kisiasa kwa India na ulimwengu wote, wakisema inamaanisha kuwa Amerika inaona India kama nguvu kuu ya kudhibiti Uchina, pamoja na mahitaji ya ulinzi ya India.

Sushant Singh, mtaalamu wa masuala ya ulinzi na kimkakati, anasema kwamba makubaliano hayo yanaonesha kuwa Marekani inaithamini India kiasi kwamba iko tayari kuendelea nayo hata kwa gharama ya kufanya makubaliano ambayo imefanya kwa Uturuki.

Mbali na Uturuki, Marekani pia imeipiga marufuku China kununua mfumo huo wa kutoka kwa Urusi , lakini kutokana na kuongezeka kwa ukaribu kati ya Marekani na India katika miaka ya hivi karibuni, Vikwazo dhididi ya India kununua silaha hiyo kungesababisha matatizo katika uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Ikumbukwe kwamba India ni mshirika muhimu wa ulinzi na kiuchumi wa Marekani.

Mtaalamu wa masuala ya ulinzi Rahul Bedi anasema kwamba kwa Marekani, 'makubaliano haya ya kutoiwekea vikwazo ilikosa pingamizi.

"Ni hakika kwamba mfumo wa ulinzi wa makombora wa S-400 utasaidia India kuboresha kwa kiasi kikubwa uwezo wake wa ulinzi, haswa wakati ambapo India iko katika mzozo tata wa mpaka na Uchina," anasema. Mbali na hayo, Marekani pia ina wasiwasi kuhusu kuimarika kwa China, ambayo ni moja ya sababu kuu ilioifanya kuiruhusu India kununua silaha hiyo.

"Marekani inataka kudhibiti Uchina na inaamini kuwa India inaweza kuchukua jukumu hilo muhimu."

Sushant Singh anasema kuwa 'Marekani haitaki kuipoteza India kwa vyovyote vile ili kuweza kushindana na China.'

"Kinachofanya uamuzi wa makubaliano kuwa muhimu zaidi ni kwamba Marekani na mataifa mengine ya Magharibi yanapinga uvamizi wa Urusi nchini Ukraine." Uchina, kwa upande mwingine, imeingia katika mzozo na India na kwa sasa inaonekana kama inaiunga mkono Urusi.

"Nadhani Urusi ni adui wa muda wa kati kwa Marekani na China ni adui wa muda mrefu na India iko katika nafasi nzuri ya kijiografia kukabiliana na China," anasema Bedi.

Ingawa makubaliano haya bado hayajatiwa saini na Rais wa Marekani, marufuku chini ya 'CAATSA' ingeiweka India katika hali ngumu hususana kuhusu uhusiano wake na Marekani.

Uungwaji mkono wa pande mbili kwa makubaliano haya kutoka kwa vyama vyote viwili vikuu vya kisiasa vya Marekani kunaonyesha kutambuliwa kote nchini kwa ukweli kwamba India ni mshirika muhimu wa taifa hilo na kwamba mahitaji ya ulinzi ya India yanatimizwa. Ni muhimu kuelewa.

 Sushant Singh anasema, 'Hii ni hatua ya ndani ya kisiasa ya Marekani ambayo inaonyesha kwamba licha ya kile kinachotokea na Urusi, hatua hii ina uungwaji mkono na pande mbili tofauti nchini Marekani.'

Kuiamini Marekani

Uamuzi wa Marekani wa kutoa kibali kwa India katika 'CAATSA' umekuja wakati muhimu ambapo Marekani na mataifa mengine ya Magharibi yanaipinga Urusi kwa sababu ya vita vya Ukraine.

Katika hali hii ya kisiasa ya kimataifa, India sio tu kwamba inaonyesha kusita kwenda kushirikiana na * nchi za magharibi, lakini pia inanunua mafuta kutoka Urusi.

Mchambuzi Ajay Shukla anasema wakati wa hatua hii ni wa kushangaza. "Siwezi kusema ni ajabu au kwamba ni muhimu, lakini inajulikana wakati ambapo Urusi imeingia katika vita na Ukraine inayoungwa mkono na Marekani," anasema.

Lakini wataalam wengi wanaamini kwamba ulikuwa uamuzi ambao ulipaswa kutimizwa kesho, ikiwa sio leo. Hii ni kwa sababu India na Urusi zina uhusiano wa kitamaduni katika sekta ya ulinzi.

India inanunua 60-70% ya vifaa vyake vya ulinzi kutoka Urusi. Licha ya juhudi za kubadilisha uagizaji wa silaha kutoka nje na kuendeleza teknolojia asilia, jeshi la India bado linategemea sana Urusi.

Wataalamu wanasema kwamba Marekani inaelewa kuwa si rahisi kwa India kugeuka kutoka kwa Urusi, kwa kuzingatia vipengele vyote hivi.

Kuipiga marufuku Uturuki na kuiruhusu India - Kwanini?

Wakati Marekani imeamua kuiondolea India vikwazo dhidi ya ununuzi wake wa mfumo wa makombora wa ulinzi wa S-400 kutoka Urusi, imeiwekea marufuku mshirika wake wa NATO Uturuki kwa sababu hiyo hiyo.

Wakati vikwazo vilipowekwa kwa Uturuki, ilikuwa katika harakati za kununua ndege za kivita za F-35 kutoka Marekani. Marekani ina wasiwasi kuwa kombora hilo la S-400 linaweza kusababisha uhamisho usioidhinishwa wa teknolojia kwenda Urusi.

Shukla anasema kuwa Marekani haikufanya makubaliano yoyote (kwa Uturuki) kwa sababu, kulingana na yeye, teknolojia inayotumiwa katika ndege za kivita za F-35 ingevurugwa au pengine kutatuliwa na mfumo wa ulinzi wa S-400.

Wataalamu wanaamini kuwa Marekani haina wasiwasi kama huo katika kesi ya India.

Shukla anasema kuwa Marekani inakubali mahitaji ya India ya S-400. Pia ni kukiri imani kati ya India na Marekani kwamba India itafanya kila linalowezekana kuzuia teknolojia muhimu kuhamishiwa kwa Warusi.

Lakini kwa Uturuki, kuwa mwanachama wa NATO kumefanya mambo kuwa magumu zaidi.

Sushant Singh anasema kwamba 'CAATSA' ilikuja kuadhibu Urusi na sio nchi zingine.

"Uturuki iliadhibiwa kwa sababu ni mwanachama wa NATO na kama mwanachama wa NATO ilikuwa na upatikanaji wa teknolojia zote za ulinzi na vifaa ambavyo nchi nyingine, ikiwa ni pamoja na India, ambayo ni washirika wa mkataba wa Marekani," anasema.

Je, hii itasababisha mabadiliko makubwa katika ulinzi wa anga ya India?

Mfumo wa kombora wa S-400 uliotengenezwa na Urusi ni moja ya mifumo bora zaidi ya ulinzi wa anga ulimwenguni. Hii bila shaka itaimarisha uwezo wa ulinzi wa India, lakini je utaisaidia India kwenye mpaka wake na China?

Wataalamu wana maono tofauti.

Sushant Singh anaamini kuwa mfumo huu hautakuwa na athari kubwa inapokuja kwa China. "Lakini inapokuja kwa Pakistan, utakuwa na athari kubwa kwa sababu hizi ni zana za hali ya juu na zenye ufanisi mkubwa," anasema.

"Silaha hii itaipa India ambayo haina ndege za kivita faida kubwa na muhimu ,katika vita vya angani," anasema.

Walakini, wasiwasi mkubwa wa India kwa sasa ni Uchina, ambayo pia waiswasi huo uko na Marekani.

Rahul Bedi anaamini kuwa mfumo huo hautabadilika sana kwa Pakistan kwani suala kuu la Pakistan ni Kashmir, ambalo limekuwa likiendelea kwa miaka mingi, lakini anaonya kuwa linaweza kufanya mambo kuwa magumu kwa India kwenye mpaka wa China.

Kwa upande mwingine, Urusi tayari imetoa mfumo wa ulinzi wa S-400 kwa China. India imetia saini makubaliano ya kununua mifumo mitano ya makombora ya S-400 kutoka Urusi, lakini hadi sasa ni mfumo mmoja tu wa S-400 ambao umefikishwa nchini China, ambao unaripotiwa kuwa kwenye mpaka wa magharibi wa India.

Vita vya Urusi na Ukraine vimeripotiwa kutatiza uwasilishaji wa agizo lililosalia kwani Urusi kwa sasa inaishambulia Ukraine.

Bedi anasema kuwa India ilipaswa kupokea sehemu ya agizo hilo mnamo Juni, ambayo bado haijafika. "Kwa kweli, uwezo wa Warusi kuiwasilisha unatia shaka kwa sababu sehemu na mifumo ya S-400 inaagizwa kutoka nchi za Magharibi ambazo zina uhusiano na Marekani," anasema.

Ingawa faida halisi ya mfumo huu wa ulinzi bado iko mbali, ni wazi kwamba India imefanikiwa sana kupata masilahi yake kutoka kwa nchi zote mbili.