Je, unataka uraia wa visiwa vya Caribbean?

    • Author, Gemma Handy
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Mataifa matano ya visiwa katika eneo la Caribbean - Antigua and Barbuda, Dominica, Grenada, St Kitts and Nevis, na St Lucia - hutoa uraia kwa uwekezaji (CBI) wa hadi dola za kimarekani $200,000 (£145,000).

Nunua nyumba, na pia utapata pasipoti inayompa mmiliki viza ya bure kwa nchi 150 ikijumuisha Uingereza na eneo la Schengen la Ulaya.

Kwa matajiri, kukosekana kwa ushuru katika visiwa hivyo, kama vile ushuru wa faida ya mtaji na urithi, na wakati mwingine mapato, ni mvuto mwingine mkubwa kwao.

Huko Antigua, madalali wa nyumba wanatatizika kukidhi ukubwa wa mahitaji, anasema Nadia Dyson, mmiliki wa Maeneo ya Anasa. "Hadi 70% ya wanunuzi wote kwa sasa wanataka uraia, wengi wao wanatoka Marekani," ameiambia BBC.

"Hatuzungumzi nao kuhusu siasa, lakini hali ya kisiasa isiyo tabirika [nchini Marekani] hakika ni sababu.

"Wakati kama huu mwaka jana, wote walikuwa wanunuzi wa kawaida. Lakini sasa wote wanasema 'nataka nyumba yenye uraia'. Hatujawahi kuuza nyumba nyingi sana kama muda huu."

“Baadhi ya wanunuzi wanatazamia kuhamia kama makazi yao ya kudumu, Bi Dyson anasema, na kuongeza: "Wachache tayari wamehamia."

Ukraine, Uturuki, Nigeria na China ni miongoni mwa mataifa mengine ya waombaji wa mara kwa mara, inasema kampuni ya Uingereza ambayo ina ofisi duniani kote inayoshughulikia masuala ya uwekezaji na uhamiaji, Henley & Patners.

Inaongeza kuwa maombi ya jumla yameongezeka kwa 12% tangu robo ya nne ya 2024.

Pia unaweza kusoma

Sababu za Kuhama

Kila kitu kutoka vurugu za bunduki hadi chuki dhidi ya Wayahudi, hayo yanawaweka Wamarekani kwenye hali mbaya, kulingana na mshauri wa kampuni hiyo Dominic Volek.

"Karibu 10-15% ya wanaohama. Ni kutokana na sera ya bima dhidi ya chochote wanachokijali. Na kuwa na uraia wa pili ni mpango mzuri wa kujilinda," anaelezea.

Bw Volek anasema urahisi wa kusafiri wa pasi za kusafiria za Caribbea hutoa naftuu kwa wafanyabiashara, na pia zinaweza kutoa faida ya usalama.

Vizuizi vya kusafiri wakati wa COVID, vilileta "mshtuko mkubwa" kwa watu matajiri waliozoea kusafiri kwa uhuru kwenye ndege zao binafsi, na kusababisha kuongezeka kwa maombi ya kuhamia Carrebbia. Na maombi yaliongezeka tena baada ya uchaguzi wa Marekani wa 2020 na 2024.

"Kuna wafuasi wa chama cha Democrats ambao hawampendi Trump lakini pia Republican ambao hawaipendi Democrats," anasema Volek.

"Katika miaka miwili iliyopita hatukuwa na ofisi nchini Marekani, na sasa tuna ofisi nane katika miji yote mikubwa, na nyingine mbili au tatu zitafunguliwa katika miezi ijayo."

Robert Taylor, kutoka Halifax nchini Canada, alinunua nyumba huko Antigua ambako anapanga kuishi baada ya kustaafu baadaye mwaka huu.

"Nilichagua Antigua kwa sababu ina fukwe nzuri, watu wake ni marafiki sana na pia kuna hali ya hewa nzuri kwa sehemu ya baadaye ya maisha yangu."

Wakosoaji wa mpango huu

Mwaka 2012 serikali ya wakati huo ya Antiguan ilitangaza kutoa paspoti hizo kama njia ya kuimarisha uchumi unaodhoofika, lakini wengine wanakosoa hilo.

Waandamanaji waliingia mitaani kulaani, anasema aliyekuwa Spika wa Bunge Gisele Isaac. "Kulikuwa na hisia ya utaifa; watu walihisi tunauza utambulisho wetu. Kwa ufupi, hawakuwa na elimu na jambo hilo.”

Viongozi wa mataifa mengine ya Carrebbia ambayo hayatoi paspoti hizo pia wamekuwa wepesi kukosoa, ikiwa ni pamoja na Waziri Mkuu wa St Vincent and Grenadines Ralph Gonsalves. Hapo awali alisema uraia haupaswi kuwa "bidhaa ya kuuza."

Kimataifa, kuna hofu kwamba mpango huo unaweza kuwasaidia wahalifu kujificha.

Umoja wa Ulaya umetishia kuondoa viza ya bure kwa nchi za Carrebbia zinazoendesha mpango huo, huku Marekani ikileza wasiwasi juu ya uwezekano wa miradi hiyo kutumika kama njia ya kukwepa kulipa kodi na uhalifu wa kifedha.

Msemaji wa Tume ya Ulaya ameiambia BBC, "inafuatilia" mpango huo, na imekuwa katika mazungumzo na mamlaka za nchi hizo tangu 2022.

Anasema tathmini inayoendelea inatafuta kuthibitisha kama uraia kwa uwekezaji unajumuisha "matumizi mabaya ya mfumo wa viza za bure kwa nchi hizo kuingia Ulaya, na kama kuna uwezekano wa kusababisha hatari za usalama kwa Ulaya."

Utetezi wao

Kwa upande wao, mataifa matano ya Carrebbia yamejibu kwa hasira madai kwamba hayafanyiki vya kutosha kuwachunguza waombaji.

Waziri Mkuu wa Dominica Roosevelt Skerrit ameelezea mpango wa CBI wa nchi yake "ni wa uwazi", na kuongeza serikali inafanya kazi kwa bidii kuhakikisha uadilifu.

Serikali inasema mauzo ya pasipoti yameongeza zaidi ya $1bn tangu kuanzishwa kwa mpango huo mwaka 1993, kulipia miundombinu muhimu ikiwa ni pamoja na hospitali ya kisasa.

Huko St Lucia, Waziri Mkuu Philip J Pierre anasema kisiwa hicho kinazingatia viwango vya juu vya usalama ili kuhakikisha CBI haisaidii shughuli haramu bila kukusudia.

Mataifa madogo ya Carrebbia yenye rasilimali duni, yanategemea zaidi utalii. Mapato kupitia mpango wa CBI husaidia katika kupambana na majanga ya asili hadi kuandaa mipango ya kitaifa ya pensheni.

Waziri Mkuu wa Antigua, Gaston Browne alisema pesa zilizokusanywa zimeitoa nchi yake kwenye ukingo wa kufilisika katika muongo mmoja uliopita.

Kando na kununua nyumba, njia zingine za kupata uraia wa Carrebbia ni kupitia uwekezaji, ambao kwa kawaida hujumuisha mchango wa mara moja kwa hazina ya maendeleo ya kitaifa.

Katika kukabiliana na shinikizo la kimataifa, visiwa hivyo vimejitolea kuchukua hatua mpya za kuimarisha usimamizi, ikiwa ni pamoja na kuanzisha mdhibiti wa kikanda ili kuweka viwango, kufuatilia uendeshaji na kuhakikisha utaratibu unafuatwa.

Zaidi ya hayo, kanuni sita zilizokubaliwa na Marekani ni pamoja na kuimarishwa kwa uhakiki, ukaguzi wa mara kwa mara, usaili wa lazima kwa waombaji wote, na kuondolewa kwa mwanya ambao hapo awali uliwezesha mwombaji aliyekataliwa na nchi moja kutuma maombi katika nchi nyingine.

Siku hizi, mauzo ya pasipoti huchangia 10-30% ya Pato la Taifa la visiwa hivyo.