Viza ya dhahabu ya Trump ni nini na inafanyaje kazi?

Muda wa kusoma: Dakika 5

Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza mipango ya kuanzisha 'viza ya dhahabu' inayogharimu dola za kimarekani milioni 5, ambayo inatoa ukaazi wa kudumu na njia ya kupata uraia kwa raia matajiri kutoka nchi za kigeni.

"Watakuwa watu matajiri na watakuwa na mafanikio, na watakuwa wakitumia pesa nyingi, kulipa kodi nyingi, na kuajiri watu wengi. Tunaamini itakuwa na mafanikio makubwa," Trump alisema katika Ofisi yake siku ya Jumanne.

Howard Lutnick, Waziri wa Biashara wa Marekani, amesema "vixa ya dhahabu" itachukua nafasi ya mpango wa sasa wa viza ya wawekezaji ya EB-5 – mpango ambao hutoa viza kwa wawekezaji wa kigeni.

Pia unaweza kusoma

Trump anapendekeza nini?

Trump alisma, "itakuwa ni viza ya watu wenye pesa."

Huku idadi ya viza za EB-5 zikiwa zimepungua, Trump amependekeza kuwa serikali ya shirikisho inaweza kuuza "viza za dhahabu" milioni 10 ili kupunguza nakisi.

Alipoulizwa na waandishi wa habari ikiwa Warusi matajiri wanaweza kupata viza hiyo, Trump alijibu: "Ndiyo, inawezekana. Ninawajua matajiri wa Kirusi ambao ni watu wazuri sana."

Hata hivyo, Lutnick alisema waombaji wote watafanyiwa uchunguzi wa kina ili kuhakikisha kuwa ni "wananchi wazuri, wa kiwango cha kimataifa."

Pia haijulikani ni muda gani wenye viza ya dhahabu watalazimika kusubiri ili kupata uraia.

Watu wenye 'kadi ya kijani' (green card) - ikiwa ni pamoja na wanufaika wa mpango wa sasa wa EB-5 - kwa kawaida wanapaswa kuishi kama wakazi halali wa kudumu nchini Marekani kwa miaka mitano kabla ya kustahiki uraia.

Congress huamua sifa za uraia wa Marekani, lakini Trump anasema "viza ya dhahabu" hazitahitaji idhini ya bunge.

Maelezo ya mpango huo mpya yatatolewa baada ya wiki mbili, aliongeza.

Kubatilisha mpango wa EB-5

Kulingana na Bw Lutnick, "programu ya EB-5... ilikuwa imejaa upuuzi na ulaghai. Ilikuwa ni njia ya kupata kadi ya kijani ambayo ilikuwa ya bei ya chini. Kwa hivyo rais amesema, badala ya kuwa na aina hii ya programu ya EB-5, tutaoundoa mpango wa EB-5."

Bunge la Marekani lilianzisha mpango wa EB-5 mwaka 1990 ili kuvutia uwekezaji wa kigeni. Hutoa fursa kwa watu binafsi kuwekeza takriban dola milioni 1 katika biashara inayounda angalau nafasi 10 za kazi.

Chini ya mpango huu, wawekezaji hupokea kadi za kijani – na kisha uraia. Kinyume chake, waombaji wengi wa kadi ya kijani husubiri kuanzia miezi hadi miaka kadhaa ili kupata ukaazi wa kudumu.

Mpango wa EB-5 hutoa viza 10,000 kwa mwaka, huku 3,000 zikiwa zimetengwa kwa ajili ya wawekezaji katika maeneo yenye ukosefu mkubwa wa ajira, kulingana na serikali ya Marekani. Madhumuni yake ni "kuchochea uchumi wa Marekani kupitia uundaji wa nafasi za kazi na uwekezaji unaofanywa na wawekezaji wa kigeni."

Katika kipindi cha miezi 12 hadi tarehe 30 Septemba 2022, takriban watu 8,000 walipata viza za wawekezaji, kulingana na Takwimu za Uhamiaji za Idara ya Usalama wa Taifa.

Kwa kuongezea, mwaka 2021, Idara ya Utafiti ya Bunge la Marekani iligundua kuwa viza za EB-5 "zina hatari zaidi ya ulaghai" ikilinganishwa na viza vingine za wahamiaji.

"Hatari hizo zinahusishwa na ugumu wa kuthibitisha kuwa fedha za wawekezaji ni urahisi wa kutokea kwa upendeleo," ilisema ripoti hiyo.

Katika nchi nyingine

Miradi kama hiyo ni ya kawaida duniani kote. Miradi ya "visa ya dhahabu" inawapa wageni matajiri haki ya kuishi na kufanya kazi katika nchi nyingine baada kuweka uwekezaji mkubwa.

Pia kuna mipango ya "pasipoti ya dhahabu", maarufu katika baadhi ya mataifa ya Karibea, watu matajiri hupata haki zote za uraia, ikiwa ni pamoja na haki ya kufanya kazi na kupiga kura katika nchi wanayoomba.

Henley & Partners, kampuni ya ushauri yenye makao makuu nchini Uingereza, inaripoti kuwa zaidi ya nchi 100 hutoa "viza ya dhahabu" kwa watu matajiri, ikiwa ni pamoja na Marekani, Uingereza, Hispania, Ugiriki, Malta, Australia, Canada na Italia.

Lakini, programu hizi zimekuwa chini ya ukosoaji na kuchunguzwa.

"Zinaweza kusaidia kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia uwekezaji wa moja kwa moja, lakini pia zinavutia wahalifu na mafisadi wanaotaka kukwepa mikono ya sheria kwa mapato ya uhalifu yanayofikia mabilioni ya dola," kulingana na ripoti iliyochapishwa na Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo mwaka 2023.

Transparency International, shirika la kimataifa linalofuatilia rushwa katika zaidi ya nchi 100, linasema mpango huo katika nchi za Umoja wa Ulaya, "si kuhusu uwekezaji au uhamiaji – bali ni kuhusu maslahi ya rushwa."

Kumekuwa na ukosoaji kutoka mashirika mbalimbali ya Ulaya. Mwaka 2022, Kamati ya Umoja wa Ulaya kuhusu Uhuru wa Kiraia, Haki na Masuala ya Ndani ilipiga kura ya kupiga marufuku pasi za kusafiria za dhahabu.

Wasiwasi huu umesababisha nchi kadhaa za Ulaya, ikiwa ni pamoja na Uingereza, Uhispania, Uholanzi, na Ugiriki, kupunguza kasi ya programu zao za viza ya dhahabu katika miaka ya hivi karibuni.

Uhispania, kwa mfano, iliondoa programu yake ya "viza ya dhahabu" iliyoundwa 2013 ambayo ilitoa viza kwa wawekezaji walionunua mali yenye thamani ya pauni 500,000 ($525,000) au zaidi. Tarehe ya mwisho ya kutuma maombi ni tarehe 3 Aprili 2025.

Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sánchez alisema mwaka jana nia ya serikali yake ni kufuta mpango ili "kuhakikisha kuwa nyumba ni haki na sio suala tu la biashara."

Utafiti wa viza ya dhahabu kwa Umoja wa Ulaya, uliofanywa na London School of Economics and Political Sciencena na Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani pia ulitilia shaka mantiki ya kiuchumi ya miradi hii, na kuhitimisha kwamba iliwakilisha sehemu "ndogo" tu ya uwekezaji wa kigeni na faida "isiyo na maana" ya kiuchumi.

Uchunguzi wa mtandao wa kimataifa wa waandishi wa habari wa uchunguzi - uliochapishwa Oktoba 2023 pia ulifichua kwamba kanali wa zamani wa Libya anayetuhumiwa kwa uhalifu wa kivita na mfanyabiashara wa Kituruki aliyehukumiwa kifungo nchini Uturuki waliweza kununua pasipoti ya Dominika kupitia mipango hii.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi